Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru. |
NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imefanya mageuzi makubwa ya kiutendaji ndani ya muda mfupi na kufanikiwa kukusanya kiasi kikubwa cha fedha.
TPHPA ilianzishwa kwa sheria ya Bunge namba nne (4) ya mwaka 2020, ikiwa na lengo la kuwa na mfumo wa pamoja wa kisheria wa kusimamia afya ya mimea na matumizi salama ya viautilifu.
Moja ya kazi kubwa ya mamlaka hayo ni kuangalia ubora wa mazao yanayosafirishwa kwenda nje na yanayoingizwa nchini, pamoja na kuangalia ubora wa viuatilifu ambavyo vinatumika kudhibiti visumbufu mbalimbali vya mazao nchini.
Utaalamu huo unafanikishwa na uwapo wa maabara zenye mashine za kisasa zinazokubalika kimataifa, hatua inayoifanya nchini kuweza kuyafikia masoko ya kimataifa.
Hata hivyo tangu kuanzishwa kwake TPHPA imeonekana kutofanya kazi kwa ufanisi hatua iliyomsukuma Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko Oktoba 24,2023 kwa kumteua Profesa Joseph Ndunguru kuwa Mkurugenzi Mkuu.
Mbali na hilo, lakini pia katika kipindi cha miezi mitatu ya Julai-Septemba 2023 mamlaka imeweza kukusanya kiasi cha shilingi 6,143,965,337.61 (bilioni 6.143) ambayo ni sawa na asilimia 95.2 ya makadirio ya makusanyo ya mwaka mzima kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani.
Akizungumza na Wahariri na waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari nchini, leo Machi 13,2024 jijini Dar es Salaam, Prof. Ndunguru alisema anaamini hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha waa 2023/24, mamlaka itaweza kukusanya zaidi ya asilimia 100 ya makadirio hayo.
Amesema ongezeko hilo la makusanyo litaisaidia Mamlaka kuweza kuongeza kiasi cha gawio lake kwa Serikali Kuu kwa asilimia 15 kutoka shilingi 968,165,000.62 walizotarajia hadi shilingi 3,686,379,202.56 kwa mwaka.
“Kwa kipindi cha Oktoba mpaka Desemba 2023 mamlaka imekusanya kiasi cha shilingi 5,352,196,967.04 na kwa kipindi cha Januari mpaka Machi 6,2024 mamlaka imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.7.”alisema.
Hatua hiyo ya haraka iliyofikiwa na TPHPA ilimfanya Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu Februari 20,2024 kuipongeza mamlaka hiyo kutokana na kuongeza ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.
Mchechu aliitembelea makao makuu ya Mamlaka hiyo yaliyopo jijini Arusha, Tanzania. Katika ziara hiyo, Mchechu alipokelewa na kufanya mazungumzo na Prof. Ndunguru na katika mazungumzo yao, Prof. Ndunguru alimueleza Msajili wa Hazina kuhusu mikakati ya mamlaka katika kuboresha utendaji wa mamlaka na ukusanyaji wa maduhuli kwa niaba ya Serikali .
Baadhi ya Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini, walioshiriki mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA |
Mchechu alimpongeza Prof. Ndunguru pamoja na menejimenti ya mamlaka kwa utendaji wenye tija na kimkakati katika kusimamia viuatilifu ikiwa ni sehemu ya kusaidia wakulima na kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula Tanzania.
Aidha, Msajili alionesha kuridhishwa kwake na utendaji wa shirika kuendana na maelekezo aliyoyatoa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akiongea na watendaji wakuu kwenye Kikao kilichofanyika Agosti, 2023. Rais Samia kupitia maono yake ya 4R ameendelea kusisitiza ufanisi na utendaji bora wa mashirika ya umma ili kuhakikisha yanakuwa na manufaa kwa Watanzania kama malengo ya kuanzishwa mashirika hayo yalivyoainishwa.
Mazungumzo ya leo ya Mamkala hayo na Wahariri na Waandishi wa Habari ni muendelezo wa mapinduzi ya utendaji wa masharika ya umma yanayosimamiwa na Msajili wa Hazina.
Nia ya Msajili wa Hazina kwa mashirika yote ni kutaka kujitathmini na kuona namna ambayo wataweza kuleta tija na kuongeza makusanyo kwa nia ya kukuza uchumi wa Tanzania.
Mafanikio haya ya muda mfupi ya TPHPA yamepokelewa kwa mtazamo chanya na uongozi wa AFRINEWSSWAHILI, ambapo umedhamiria kuhakikisha unaleta mfululizo wa Makala zitakazoielezea kwa kina mamlaka haya ambayo yana tija kubwa kwa Watanzania wote.
Ofisa kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akitoa utangulizi kwa Wahariri kwa kile kilichofanywa na TPHPA.
0 Comments