Wahariri wa vyombo vya Habari mbalimbali Tanzania walposhiriki semina ya siku mbili ya kuejengeana uwezo, wakiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa JET na wakufunzi.
NA JIMMY KIANGO-AFRINEWS BAGAMOYO
Tanzania na dunia kwa ujumla inapita katika changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabia nchi yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la kasi la shughuli za kibinadamu.
Ongezeko la watu, shughuli za kilimo, ufugaji na matumizi ya kuni na mkaa ni miongoni mwa masuala yanayotajwa kuathiri moja kwa moja mazingira hali inayoleta athari mbalimbali katika dunia.
Taarifa mbalimbali za kitafiti zinaonesha kuwa ukataji wa miti ni sababu kubwa inayochangia uharibifu wa mazingira na kukaribisha kadhia ya mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa mujibu wa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 2021-2023, inakadiriwa kuwa kiasi cha hekta 469,420 za misitu hukatwa kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za kibinadamu ikiwemo kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa hali inayochangia kuongezeka kwa ukame pamoja na athari za kiikolojia.
Mpango kazi wa utekelezaji wa kampeni ya hifadhi na usafi wa mazingira ya mwaka 2021-2026, inaweka wazi kuwa takribani asilimia 16 ya eneo la nchi tayari limegeuka kuwa jangwa.
Hali hii imeifanya dunia kutafuta namna sahihi za mapambano ya kuhakikisha mazingira yanatunzwa na kulindwa kwa gharama yeyote ile lengo likiwa ni kuifanya dunia kuendelea kuwa sehemu salama ya kuishi.
Hata hivyo ufanikishaji wa mapambano haya unahitaji ushiriki wa kila mtu na waandishi wa Habari hasa Wahariri ni watu muhimu kwenye mapambano haya kutokana na kalamu zao kubeba sauti kubwa yenye mawimbi yanayopenya popote pale kwa haraka na kwa muda mfupi.
Ukweli wa hili umekisukuma Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), kupitia Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Julai 18-19,2024, kukutanisha Wahariri wa vyombo vya Habari mbalimbali Tanzania, ili kuwajengea uwezo wa kuripoti kwa ufasaha na kwa uzito wa juu masuala ya uhifadhi na mazingira.
Meneja wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi, mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dk. Elikana Kalumanga,akifafanua jambo mbele ya Wahariri.
Semina hiyo ilifanyika Bagamoyo mkoani Pwani, ambapo Wahariri shiriki walikutanishwa na wataalamu wa uandishi wa Habari zenye tija na wale wa uhifadhi na mazingira.
Pamoja na mambo mengine Wahariri walielezwa kinagaubaga kuwa kupitia kalamu zao wao ndio wanapaswa kuwa wapiga kelele namba moja wa kukemea uharibu wa mazingira wakati wowote unapojitokeza.
Siku ya kwanza ya semina hiyo Julai 18,2024 ilitumiwa vizuri na Mkurugenzi wa Mfuko wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Dastan Kamanzi ambae alikuwa ni mmoja wa wakufunzi.
Kamanzi aliwakumbusha Wahariri kuwa wanayo dhamana ya kuikoa Tanzania katika kadhia hii ya uharibifu wa mazingira na kuwataka kulibeba jukumu hilo kwa uzito unaostahili.
Alisema njia pekee ya kubeba dhamana hiyo ni kuandika Habari za Uhifadhi na mazingira zenye tija kwa jamii ikiwa ni pamoja na kueleza kwa uwazi ukubwa wa tatizo, sababu ya tatizo na namna ya kukabiliana nalo.
“Tunajitahidi kuandika Habari nyingi za Mazingira na Uhifadhi, lakini nyingi kati ya hizo ziko chini ya viwango, hazileti suluhisho katika jambo hili ambalo linaisumbua dunia.
“Wahariri wanapaswa kujua kuwa kalamu zao zina nguvu zaidi ya bunduki au bomu, kalamu zao zinaweza kuleta mabadiliko ya haraka kwenye suala hili tunalopambana nalo sasa, kinachopaswa kufanyika ni kuandika habari zenye tija zilizobeba maeneo yote pamoja na kutoa suluhisho ya jambo husika, wasiishie kwenye kuripoti matukio tu,”alisema Kamanzi.
Somo la Kamanzi halikutofautiana san ana lile lililotolewa Julai 19,2024 na Mhadhiri wa Shule Kuu ya Habari Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Darius Mukiza.
Mhadhiri wa Shule Kuu ya Habari Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Darius Mukiza.
Hata hivyo Dkt. Mukiza yeye alisisitiza zaidi umuhimu wa kuandika Habari za Uhifadhi na Mazingira zinazogusa maeneo yote husika.
Alisema Habari nyingi zinazoandikwa kuhusu masuala ya Uhifadhi na Mazingira pamoja na mabadiliko ya tabia nchi hazishirikishi wataalamu badala yake waandishi wanaripoti matukio zaidi.
“Kama habari za mazingira, uhifadhi na mabadiliko ya tabia nchi zinawahusu wananchi, watalaamu na wadau wengine, tunapaswa kuwapa wote nafasi ya kuzungumza, pia tujihangaishe kutafuta taarifa zaidi za suala lililozungumzwa na chanzo chetu cha habari.
“Wahariri na waandishi wa Habari kwa ujumla, tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuendesha vita ya uharibifu wa mazingira na njia pekee ni kuhakikisha tunaandika Habari zenye taarifa za kutosha na elimishi,”alisema Dkt. Mukiza.
SEKTA BINAFSI NI MLINZI MKUU WA MAZINGIRA NA UHIFADHI
Katika semina hiyo pia Wahariri walielezwa umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi katika ulinzi wa Mazingira na uhifadhi kwa tija. Kwamba kama sekta binafsi itashirikishwa kikamilifu na kuwekeza kwa wingi kwenye masuala ya uhifadhi na mazingira inaweza kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi na watu wanaoweza kulizungumza hili kwa tija, hoja na haja ni Wahariri kupitia kalamu zao.
Meneja wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi, mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dk. Elikana Kalumanga, ndie amelisema hili katika siku ya kwanza ya semina hiyo.
Alisema uchache wa wadau na wawekezaji binafsi waliopo sasa kwenye masuala ya uhifadhi na mazingira umesaidia kuimarishwa kwa shughuli za utalii na utunzaji wa shoroba za wanyamapori nchini.
Amesema Wanyamapori wanaopatikana katika hifadhi za Taifa na maeneo tengufu wamekuwa wakitumika katika shughuli za utalii na uwindaji na hivyo kuipatia nchi mapato ambayo yanatumika katika kuboresha huduma za kijamii, hii ina maanisha kama kutakuwa na uwekezaji mkubwa ni wazi nchi itafaidika zaidi.
“Ikiwa sekta binafsi itashirikishwa kikamilifu inaweza kuendelea kuwa na mchango katika pato la Taif ana hata kazi ya ulinzi wa misitu, hifadhi na mapori tengefu utakuwa ni mkubwa kwa sababu hakuna mtu aliyeweka hela zake atakubali kuharibu mazingira ambao utakuwa ni chanzo cha kutowesha wanyama katika eneo alilowekeza.
“Ni kweli sasa tunakabiliwa na tishio la mabdiliko ya tabia nchi ambayo yanaweza kutowesha viumbe pori tulivyo navyo, lakini kama sekta binafsi itashiriki kikamilifu kwenye biashara ya uhifadhi na mazingira ni wazi maeneo mengi ya hifadhi yatakuwa salama,” amesema Dk. Kalumanga
Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo akifurahia ubora wa semina hiyo iliyokutanisha Wahariri wote walioalikwa.
Amesema ni rahisi kwa mtu aliyeweka fedha zake kwenye uhifadhi kuilinda pesa yake kwa kuhakikisha uhifadhi unakuwa endelevu, kuliko mtu ambae hajawekeza chochote, yeye anaweza kukata miti au hata kuvamia shoroba kwa sababu anadhani hana faida na wanyamapori, aliyewekeza hela zake kibiashara hatakubali kuharibu makazi ya wanyamapori kwa sababu anajua akiharibu ni wazi wanyamapori watatatoweka nay eye hatafanyabiashara.
Hatua ya kujenga uwezo wa kitaasisi wa wadau wa umma na sekta binafsi utakuza ushiriki wa sekta binafsi katika uhifadhi wa viumbe hai na usimamizi wa rasilimali za asili.
“Hatua hiii itasaidia sana kuboresha sera, kanuni, na mazingira ya kuwezesha uhifadhi wa viumbe hai na usimamizi wa rasilimali za asili. Lakini hili huonekana manufaa yake ikiwa sekta binafsi itashirkishwa.
“Lakini yapo manufaa kadhaa ambayo sekta binafsi imeweza kushirikishwa na kuingiza fedha za kigeni zaidi ya dola za Marekani milioni 2. lakini pia wanasaidia katika kutoa utaalamu katika usimamizi wa Rasilimali za Asili, ikiwamo mbinu mpya katika kupambana na ujangili.
“Pia sekta binafsi hujua mifumo ya masoko ya bidhaa kama shanga na nyinginezo na si hilo tu pia husaidia miradi ya jamii kupitia Ushirikiano wa Umma na Binafsi (PPP),” amasema Dk. Kalumanga
Alitolea mfano wa baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakihifadhiwa vizuri kutoka ana uwepo wa sekta binafsi kuwa ni shoroba ya Kwakuchinja iliyoipo wilayani Babati mkoani Manyara.
“Kuirikisha sekta binafsi husaidia ufuatiliaji ,kuongeza usimamizi wenye ufanisi hasa kwenye mikoa yenye changamoto ya kuvamiwa kwa shoroba za wanyamapori .,” amesema
Siku mbili hizo zilitumika kwa ufasaha kufikisha elimu sahihi kwa Wahariri na kwa kauli zao wengi walionesha kuridhishwa na kufurahishwa na kile walichofundishwa.
Mnaku Mbani ni Mhariri wa Biashara wa gazeti la The Guardian, anakiri kuwa mafunzo aliyoyapata ingawa ni ya muda mfupi, lakini yamemsaidia kulijua jukumu lake la kuitumia kalamu yake kuwaalika wawekezaji binafsi kuwa sehemu ya ulinzi wa maliasili kwa kuwekeza kwenye uhifadhi na mazingira.
“Nimejua umuhimu wa sekta binafsi kushiriki katika uhifadhi, ni kweli mtu aliyeweka hela yake nyingi, hawezi kukubali mazingira kuharibiwa kwa sababu anajua wazi ataharibu biashara yake.”
Mhariri wa Maudhui wa Jarida la TZ&BEYOND, Sidi Mgumia nae alisema kuwa semina hiyo imemsaidia kuitambua nafasi yake katika kulea waandishi wa Habari anao wasimamia ili kujua namna sahihi ya kuandika Habari zenye tija kwa jamii.
Salim Said Salim, Mhariri na Mwandishi mkongwe kutoka Zanzibar, amefurahishwa na mafunzo hayo na kuitaka JET na USAID kuhakikisha wanayafanya mara kwa mara ili kuendelea kuwajengea uwezo Wahariri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru amesema lengo la kukutana na Wahariri ni kuwajengea uelewa katika uandishi wa taarifa za uhifadhi na mazingira ili kuleta matokeo chanya kwa jamii.
0 Comments