Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo, akitoa pongezi kwa Wizara ya Nishati, kwa kufanikisha kwa ubora ujenzi wa jengo la wizara hiyo. |
NA MWANDISHI WETU-DODOMA
Ujenzi wa jingo la Wizara ya Nishati unaoendelea katika mji wa kiserikali wa Mtumba, jijini Dodoma umefikia asilimia 94, hatua iliyoifanya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kumwaga pongezi kwa wizara.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, David Mathayo, Machi 20,2025 wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa jengo hilo iliyohusisha Menejimenti ya Wizara na baadhi ya watumishi.
“Tumepita kila mahali katika jengo hilo, kazi nzuri na kubwa imefanyika na mandhari ya ndani na ya nje zote zinavutia sana, nawapongeza sana Wizara ya Nishati kwa kazi hii, zaidi kamati inampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kuwa fedha zinapatikana za kutekeleza ujenzi wa majengo mengi na mazuri ya serikali.” Amesema Mathayo
Aidha amewapongeza viongozi wakuu na Menejimenti ya Wizara ya Nishati kwa kusimamia vyema ujenzi huo na kuhakikisha fedha za mkandarasi zinalipwa kwa wakati wote.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo amewasisitiza wajenzi wa jingo hilo kukamilisha kazi ndogo zilizosalia ili watumishi waweze kuhamia katika jengo hilo mapema.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu, amesema kuwa watumishi wa Wizara ya Nishati wanatarajia kuhamia katika jengo hilo kabla ya mwezi Mei 2025 kwa kuwa kazi kubwa tayari imeshafanyika.
Dkt. Kazungu amesema watumishi wote wakihamia katika jengo kutawazesha watumishi kukaa sehemu moja na kufanya kazi zao kwa ufanisi tofauti na ilivyo sasa ambapo watumishi wamegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni Kikuyu na Mtumba.
0 Comments