NA. FATMA JALALA
Swali la msingi si tena kama sheria ipo, bali ni kwa nini matokeo yanabaki chini ya kiwango kilichokusudiwa?
Nani anawajibika katika pengo hilo, na hatua zipi za kimfumo zinahitajika ili kuhakikisha makundi maalum yananufaika kwa vitendo na fursa za ununuzi wa umma?
Tunapozungumzia makundi maalum yanajumuisha wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu. Hawa ndio wanatakiwa kunufaika kwa vitendo na fursa za ununuzi wa umma kupitia upendelea huu kisheria.
Katika muktadha huo, ni muhimu kukumbuka kuwa utekelezaji wa sharti hili si suala la hiari. Hatua yoyote ya kutotekeleza matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ikiwemo kukiuka sharti la kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalum ni kosa la jinai.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 128(2)(d) na 128(2)(f) cha sheria hiyo, mkosaji akitiwa hatiani anaweza kutozwa faini isiyozidi Sh milioni 10, au kifungo kisichozidi miaka mitatu, au adhabu zote mbili kwa pamoja.
Adhabu hiyo imewekwa mahsusi kuimarisha uwajibikaji miongoni mwa watendaji wa taasisi za umma na kuhakikisha kuwa wajibu wa kisheria wa kuyawezesha makundi maalum hauishii kwenye maandishi ya sera pekee.
Kwa maana hiyo, mjadala wa “wapi tumekwama na nini kifanyike” unapaswa kuanzia katika msingi wa uwajibikaji wa kisheria, sambamba na kutafuta suluhisho la kiutendaji litakalogeuza matakwa ya sheria kuwa matokeo yanayoonekana kwa walengwa.
MATAKWA YA SHERIA
Kifungu cha 64(1–3) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma kinazitaka taasisi zinazofanya ununuzi kutenga angalau asilimia 30 ya thamani ya ununuzi wa mwaka kwa ajili ya makundi maalum, kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa.
Hata hivyo, utekelezaji wa sheria hiyo unategemea kwa kiwango kikubwa uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa ngazi za chini, ambao wako karibu zaidi na wanufaika.
UFAHAMU MDOGO
Uchunguzi uliofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, ukihusisha mradi wa ujenzi na ukarabati wa Soko la Tandale, umebaini kuwepo kwa udhaifu katika utekelezaji wa sharti la asilimia 30.
Baadhi ya viongozi na watendaji walikiri kutokuwa na ufahamu wa kina wa matakwa ya sheria hiyo.
Mwanasheria wa Manispaa, Charles Lawisso, aliahidi kupitia sheria hiyo kabla ya kutoa majibu.
Diwani wa Kata ya Tandale, Abdulaziz (jina kamili halikupatikana), alikiri kuwa anasikia sharti hilo kwa mara ya kwanza lakini hajafahamu jinsi linavyofanya kazi.
Mweka Hazina wa Soko la Tandale, Blandina Daniel, alisema wanawake wa soko hilo hawajapatiwa elimu wala fursa husika.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tandale Sokoni, Salum Kaponda, alikiri kuwa elimu ya mfumo wa ununuzi wa umma haijawafikia wananchi kwa kiwango kinachohitajika.
Hali hiyo inaonyesha pengo la mawasiliano na uhamasishaji, linaloweza kuwanyima wanawake na makundi mengine haki yao ya kisheria.
WAJASIRIAMALI WADOGO WANAZIKIMBIA FURSA
Afisa Ununuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Vumilia Tigwela, amekiri changamoto ya uelewa mdogo miongoni mwa walengwa.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) ilitekeleza Sh bilioni 50 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na huduma katika miradi zaidi ya 300.
Kati ya fedha hizo, takribani Sh bilioni 2 pekee ndizo zilizowanufaisha makundi maalum. Kwa hesabu za moja kwa moja, kiwango hicho ni takribani asilimia 4 tu, kikiwa mbali na sharti la kisheria la asilimia 30.
Vumilia ametaja changamoto kuu kuwa ni elimu ndogo na ukosefu wa mitaji.
Wajasiriamali wengi wadogo wana uelewea mdogo sana kuhusiana na mfumo wa NeST na fursa zake kunatokana na ukosefu wa mafunzo maalum kwa makundi lengwa.
NeST ni mfumo wa kielektroniki unaotumika kuomba na kutoa zabuni za serrikali na taasisi zake.
Lakini mbali na changamoto hizo kuu pia masharti magumu ya kisheria yanayozuia vikundi kutoka nje ya eneo la mradi kushiriki.
Tigwela ameshauri kuunganishwa kwa mikopo ya asilimia 10 ya vikundi na fursa za zabuni, ili mitaji isiwe kikwazo na marejesho yawe rahisi kupitia makato ya moja kwa moja.
PPRA: ELIMU INATOLEWA, MWITIKIO NI MDOGO
Meneja wa Kanda ya Pwani wa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Vicky Mollel, anasema mamlaka hiyo imekuwa ikitoa mafunzo kwa kushirikiana na Halmashauri, NGOs na vyama vya wafanyakazi.
Alisema baadhi ya mafunzo hayo yalifanyika Desemba 19, 2025 – Manispaa ya Kinondoni, Januari 10, 2026 – mikoa ya Mbeya, Tabora, Mwanza na Dar es Salaam na Januari 26, 2026 – Wilaya ya Chalinze.
Hata hivyo, changamoto zilizotajwa kupitia mafunzo hayo ni mwitikio mdogo wa walengwa, mahudhurio hafifu, ufuatiliaji dhaifu baada ya mafunzo, dhana potofu kuwa kufanya kazi na serikali ni mchakato mgumu.
MKURUGRNZI PPRA: TEKELEZENI SHERIA
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, amesisitiza kuwa kutotekeleza sharti la asilimia 30 ni kosa la jinai.
Akizungumza Desemba 15, 2025 mkoani Tanga, alikariri masharti ya kifungu cha 128(2)(d) kuwa yeyote atakayekiuka matakwa ya sheria, akitiwa hatiani, atawajibika kwa faini au kifungo kama ilivyoainishwa.
TANZANIA INAWEZA KUJIFUNZA KUTOKA NJE
Tanzania inaweza kujifunza kutoka nchi ambazo zimefanikiwa katika eneo hili. Nchi hizo ni kama vile Afrika Kusini – kupitia sera ya PPPFA na mpango wa B-BBEE, imeongeza ushiriki wa makundi yaliyotengwa kihistoria.
Kenya – kupitia mpango wa AGPO, kisheria asilimia 30 ya zabuni hutengwa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kwa kutumia mfumo wa kidijitali.
Brazil – sheria zake zinatoa upendeleo kwa biashara ndogo na za kati (SMEs), huku mfumo wa zabuni mtandaoni ukirahisisha upatikanaji wa taarifa.
MAPENDEKEZO
Ili kuhakikisha utekelezaji kamili wa sharti la asilimia 30, hatua zifuatazo zinapendekezwa na baadhi ya viongozi;
Elimu endelevu - mafunzo ya vitendo kuhusu usajili wa vikundi, biashara zinazohitajika na serikali na matumizi ya mfumo wa NeST.
Urahisishaji wa masharti - mapitio ya kanuni zinazozuia vikundi kushiriki nje ya maeneo yao ya makazi.
Ufuatiliaji na uwajibikaji - kuweka mfumo wa kupima utekelezaji wa asilimia 30 kwa kila taasisi.
Ushirikiano wa taasisi - kuunganisha ofisi za Manunuzi, Maendeleo ya Jamii na utoaji wa mikopo ya asilimia 10.
Uhamasishaji wa jamii - kutumia vyombo vya habari na watendaji wa kata kufikisha elimu kwa walengwa.
Sheria ipo, adhabu zipo, na fursa zipo. Changamoto iliyopo ni utekelezaji na uelewa.
Iwapo taasisi za umma hazitatekeleza kikamilifu sharti la asilimia 30, si tu kwamba zitakuwa zimekosa wajibu wa kijamii, bali pia zitakuwa zinajiweka katika hatari ya kuwajibika kisheria.
Ununuzi wa umma si utaratibu wa kifedha pekee, ni chombo cha maendeleo jumuishi. Makundi maalum yanapaswa kupewa nafasi si kwa huruma, bali kwa haki yao ya kisheria.
0 Comments