| Miti ya Mikoko |
NA. JIMMY KIANGO
Katika mkutano wa pembeni kuhusu Miradi ya Huduma za hali ya Hewa na Matumizi yake (CLIMSA) kwenye COP30, Novemba 11, mwaka huu, Tanzania iliwasilisha mifano ya urejeshaji wa mikoko katika Delta ya Rufiji na matumizi ya Jarida la Hali ya Hewa Kilimo kwa wakulima vijijini, kama suluhisho la kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia mradi wa urejeshaji wa mikoko Delta ya Rufiji, Tanzania iliionyesha jumuiya ya kimataifa, juhudi zake za kurejesha misitu ya mikoko iliyoharibiwa na mabadiliko ya tabianchi na ukataji miti.
Mradi huu unatekelezwa na shirika la Blue Carbon Tanzania kwa kushirikiana na jamii za eneo hilo, ambapo Meneja Program wa shirika hilo Frida Bryson, alikieleza kikao hicho kuwa, urejeshaji huo unasaidia kupunguza athari za tabianchi, kuimarisha maisha ya jamii, na kufungua fursa za mapato kupitia biashara ya kaboni.
Si delta ya Rufiji pekee iliyoathiriwa na ukataji mikoko, maeneo mengi ya ukanda wa Pwani hapa nchini yenye miti ya mikoko yameathiriwa na vitendo hivyo.
Baadhi ya maeneo hayo ni Pwani ya Dar es Salaam, Bagamoyo, Lindi, Mtwara pamoja na Tanga yameathiriwa na ukataji wa miti ya mikoko kwa ajili ya shughuli za kijamii kama kupata kuni, kuchoma mkaa na malighafi za ujenzi.
Hata hivyo, juhudi za urejeshaji wa miti ya mikoko katika maeneo yaliyoathiriwa kama vile Kigamboni, jijini Dar es Salaam, yameanza kufufua matumaini mapya kwa wakazi wa maeneo hayo, na sasa simulizi yake ni ya kuvutia mithili ya sauti ya ndege mnana wa porini, na ukitaka kuthibitisha hilo, basi fika Kigamboni majira ya usiku.
| Zoezi la urejeshaji wa mikoko likiendelea, wa kwanza kushoto ni Mwandishi wa makala haya, akishiriki kupanda mikoko. |
Majira ya usiku, pwani ya Kigamboni huwa na utulivu wa aina yake, utulivu unaovutwa na pumzi ndefu za misitu ya mikoko iliyotandaa na kusimama imara kama walinzi wa Rais wa nchi, ambayo imekuwa fahari ya Tanzania kwenye mkutano wa COP30 unaoendelea nchini Brazili.
Mawimbi ya bahari yanachapa mwendo wake polepole kwenye matope, kila mti wa mkoko huonekana kana kwamba una masikio yanayosikiliza mazungumzo ya maji, macho yanayotazama takataka kutoka nchi kavu na mikono inayoshika maisha ya bahari yasiyoonwa na wengi. Mikoko ni maisha ya bahari, baionuai na ikolojia ya pwani.
Ukweli ni kwamba hadithi ya mikoko si hadithi ya miti pekee kama miti mingine nje ya bahari. Mikoko ni hadithi ya chujio la bahari, ni maisha na uchumi.
Kwa miaka mingi, mikoko imekuwa shujaa asiyeonekana ikichuja taka ngumu, uchafu na tope linalotiririka kutoka nchi kavu ikiwa na lengo la kuiacha bahari safi na salama, samaki waendelee kuishi na maisha ya wavuvi yawe na matumaini.
Mizizi yake mirefu iliyokwenda chini na mingine kuchomoza juu ya ardhi na kushikana kama vidole vya mikono ya bibi mzee anayelinda kaya, imekuwa ndiyo sababu ya bahari kuendelea kuwepo, ingawa inakabiliwa na matishio kadhaa yakiwemo ya taka ngumu.
Bila shaka dunia awali haikutambua umuhimu wa mikoko baharini na ilipoanza kuelewa, imekuta tayari mikoko mingi Tanzania na duniani kwa ujumla imeanza kupotea.
MIKOKO FAHARI YA TANZANIA COP30
Kutokana na kuwepo kwa tishio la mikoko kuwa hatarini kutoweka, Tanzania ilianzisha harakati za urejeshaji wa mimea hiyo na kwa mwaka huu moja ya malengo yake ni kuyageuza mafanikio ya urejeshaji wa misitu ya mikoko kuwa mfano wa, kimataifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Tunafanya hivi kwa ajili ya watoto wetu,” anasema Jumanne Hussein, mvuvi mwenye umri wa miaka 48 ambae amekuwa akishirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kufanya urejeshaji wa miti hiyo,” alisema.
Anaongeza kuwa, “Mikoko ikipotea, samaki wanapotea, na bahari inakula ardhi yetu. Tumeliona hilo na ndio maana tunashiriki kwenye jitihada za kuirejesha.”
Kwa miaka mingi, mikoko imekuwa kinga muhimu dhidi ya mawimbi makubwa na mmomonyoko wa fukwe. Hata hivyo, uharibifu wa mazingira unaosababishwa na utupaji wa taka ngumu hasa za plastiki na mabadiliko ya tabianchi vimeacha eneo kubwa la fukwe kuwa hatarini.
Katika mkutano wa COP30 unaoendelea nchini Brazil, Tanzania imewasilisha miradi ya mikoko kama sehemu ya michango yake ya kitaifa (NDCs) chini ya Mkataba wa Paris, sambamba na kutafuta ufadhili zaidi kupitia mifumo ya kimataifa ya fedha za tabianchi.
Wanasayansi wanabainisha kuwa, mikoko inaweza kuhifadhi hadi mara 10 zaidi ya kaboni kwa hekari kuliko misitu ya mvua ya tropiki, hivyo kuwa nyenzo muhimu dhidi ya ongezeko la joto duniani.
Hata hivyo, Tanzania tayari imepoteza zaidi ya hekari 100,000 za mikoko na hii ni kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutokana na uvunaji holela, kilimo cha chumvi na ujenzi usiozingatia sheria.
MCHE MMOJA KWA WAKATIMwaka 2021/22 katika mwambao wa fukwe, jitihada za kufanya urejeshaji mikoko zilianza, zaidi ya miche 500,000 ya mikoko imepandwa ndani ya miaka mitatu kupitia kampeni ya kitaifa ya “Mikoko Milioni Kumi,” inayolenga kurejesha hekari 10,000 kufikia 2030.
Wanawake wamekuwa nguvu kubwa katika urejeshaji huo.
“Awali tulidhani hii ni kazi ya wanaume,” anasema Fatuma Rajabu, kiongozi wa kikundi cha wanawake. “Lakini tulijifunza kuwa kulinda pwani ni kulinda familia.”
FURSA YA UCHUMI WA BULUU NA MASOKO YA KABONI
Miradi ya mikoko inafungua pia fursa za kiuchumi kupitia masoko ya “kaboni ya bluu. “Kwa kila hekari ya mikoko, mamia ya tani za kaboni hufyonzwa,” anasema Frida Bryson Meneja Program wa Shirika la Blue Carbon Tanzania, linajojhihusisha na upandaji wa mikoko katika Delta ya Rufiji.
Taasisi hiyo inatumia teknolojia mbalimbali kama droni, sensa na akili bandia (AI) kufuatilia ukuaji wa mikoko na uhifadhi wa kaboni jambo ambalo linahitajika uwekezaji wa kimataifa ili kuifanya misitu ya mikoko kuwa endeklevu.
NEMC YATAHADHARISHA
Kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari, mawimbi makubwa na maji chumvi kupenya mashambani kunadhihirisha umuhimu wa mikoko kama kinga.
NEMC linaonya kuwa kuendelea kupungua kwa mikoko kunaweza kuwaongezea maelfu ya watu hatari ya kuhamishwa.
Serikali tayari imeimarisha ulinzi kupitia Sheria ya Misitu, kutenga maeneo ya mikoko kuwa hifadhi na kuhamasisha urejeshaji unaoongozwa na jamii.
Washirika wa kimataifa kama Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wanaendelea kutoa msaada. Katika program za urejeshaji wa miti ya mikoko.
Bryson anaamini jitihada zinazofanywa na Tanzania katika urejeshaji wa miti ya mikoko, zinaweza kuwa rejea ya bara zima la Afrika.
“Endapo tutathibitisha kuwa kaboni ya bluu inanufaisha jamii si mashirika pekee, tutafungua ukurasa mpya wa fedha za uhifadhi Afrika.” alisema.
Kwa kuibua hadithi ya mikoko kama nguzo ya maisha, uchumi na kinga dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, Tanzania si tu imejenga matumaini mapya kwa jamii zake za pwani, bali pia imeweka alama ya uongozi wa Afrika katika ulinzi wa mazingira kupitia COP30.
0 Comments