NA. JIMMY KIANGO
Katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliana na athari za mabadiliko tabia nchi yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu, wataalamu wa masuala ya Ikolojia ya Bahari wameungana nchini Brazili na kutoa azimio lililohimiza umuhimu wa viongozi waa nchi zote duniani kuutambua umuhimu wa bahari kwa ustawi wa dunia na watu wake.
Jukwaa la wadau wa Bahari duniani kwenye mkutano wa COP30 unaoendelea nchini Brazili ‘Ocean Pravilion’ ndio limemetoa azimio hilo ambalo limeungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambae pia ni mtaalamu wa Mazingira ya Bahari Dkt.Jestina Katandukila.
Katika mazungumzo yake na Afrinewsswahili, Dkt. Katandukila anasema azimio la wataalamu hao limelenga maeneo muhimu na Tanzania kama sehemu ya waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi hasa katika mazingira ya bahari tunapaswa kulitekeleza.
“Kwa mtazamo wangu, ni azimio sahihi kwa wakati sahihi, nikiongelea mkutano kwa ujumla, naona unakwenda vizuri na natumaini ukifika mwisho tutapata suluhisho mbadala zinazohusisha ukuaji wa sayansi na teknolojia kwenye kutatua changamoto nyingi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hasa kwenye nchi zinazoendelea hususani kwenye nyanja za uchafuzi wa bahari na fukwe ambao unahusisha utupaji taka ngumu kiholela au ukosefu wa njia mbadala wa uteketezaji wa taka hizo.
“Japo suluhisho kwa changamoto zitaainishwa na kujadiliwa kwenye mkutano wa COP30 2025 lakini ufanisi wa utekelezaji utategemea sera za kila nchi na vipaumbele vyake ikizingatia uboreshwaji miundombinu wezeshi na kuongeza viwango vya uwezo wa kutumia teknolojia sahihi na kuleta matokeo chanya kwenye kupunguza uchafuzi wa fukwe na bahari.
“Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye kupunguza changamoto za kuhamasisha na utekelezaji wa sera za kukuza uchumi wa buluu. Mafanikio hayo yametokana na ushirikishwaji wa wadau wote wa mazingira kuanzia ngazi za vijiji, makundi mbalimbali wakiwemo wanawake na vijana, sekta za serikali na binafsi.
“Japokuwa Tanzania kuna changamoto ndogo ndogo za kikanda, ikiwemo utupaji wa taka ngumu hasa za plastiki; hili linaweza kuendelea kupungua kwa kadri uelewa wa athari zake utakavyoainishwa kwa jamii ya eneo husika au wazalishaji wa taka hizo. Uwezeshaji wa matumizi ya technologia sahihi kwenye kukuza uchumi wa buluu uongezwe ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia kwa mafanikio chanya.”amesema.
Wadau wa mazingira ya bahari, wanaamini kuwa Bahari na Misitu ni nguzo pacha kwa mustakabali endelevu na kwamba yapo mambo saba muhimu ambayo yanapaswa kutekelezwa kwa uharaka ili kuiokoa dunia.
Athari zinazoikumba Tanzania kwenye mazingira ya bahari kutokana na kukithiri kwa taka ngumu nje na ndani ya bahari zinalifungamanisha moja kwa moja na azimio hilo, ambalo kimsingi limelenga kuikoa bahari kwa ngazi ya kitaifa na kimataifa.
| Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambae pia ni mtaalamu wa Mazingira ya Bahari Dkt.Jestina Katandukila(picha kwa hisani ya mtandao). |
AZIMIO
Tunashiriki anga moja, ardhi moja, na bahari moja. Mifumo hii ya asili iliyounganishwa ndiyo inayounga mkono watu wote na uhai wa duniani, ikivuka mipaka, utajiri, tamaduni na itikadi.
Ustahimilivu wetu unategemea afya ya misitu na bahari, nguzo pacha za uthabiti wa sayari na washirika muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupotea kwa bayoanuai.
Tunapokutana Belém kwa ajili ya COP30, katika eneo lililoundwa na msitu wa mvua, mto na bahari, tunatoa wito kwa viongozi wote kutambua jukumu muhimu la bahari, sambamba na misitu, kama mdhibiti wa tabianchi duniani.
Mwaka huu, tukifuata kasi ya Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Bahari (UNOC3), Mpango wa Hatua za Bahari wa Nice, na ‘Blue NDC Challenge’, pamoja na mafanikio ya hivi karibuni ya Mkataba wa Bahari za Juu, tuna fursa ya kipekee ya kuingiza kikamilifu suluhisho za bahari katika malengo ya tabianchi, malengo ya bayoanuai na mikakati ya maendeleo endelevu.
Jukwaa la Bahari (Ocean Pavilion) linaleta sauti ya bahari katika mchakato wa UNFCCC ili sehemu hii muhimu ya mfumo wa Dunia ipate nafasi inayostahili katika mijadala ya tabianchi.
Bahari ni chanzo cha uthabiti wa sayari. Inazalisha zaidi ya asilimia 50 ya oksijeni ya dunia, inafyonza takribani theluthi moja ya hewa chafu (GHG); inasafirisha na kuhifadhi kiasi kikubwa cha kaboni; imechukua zaidi ya asilimia 90 ya joto la ziada linalozalishwa na hewa chafu na inasaidia kudhibiti mifumo ya hali ya hewa, kuendeleza mifumo ya ikolojia na kudhibiti joto la dunia sawasawa na misitu kwenye ardhi.
Ni moyo wa mzunguko wa maji duniani, msingi wa uchumi wa buluu na uti wa mgongo wa mifumo ya chakula inayotegemwa na mabilioni ya watu.
Hata hivyo, mifumo hii inatetereka kutokana na uzalishaji usiodhibitiwa wa hewa chafu, uvunaji rasilimali usio endelevu na uchafuzi wa mazingira.
Kuongezeka kwa joto la maji, wingi wa asidi, kupotea kwa bayoanuai na uharibifu wa ikolojia si vitisho vya kimazingira pekee, vinatikisa uchumi, jamii na usalama wa tabianchi kila sehemu.
Hata watu wasiokaribu na misitu au bahari wana uhusiano wa moja kwa moja na afya ya mifumo hii miwili muhimu. Kazi iliyo mbele yetu iko wazi: Ili kulinda sayari, lazima tulinde bahari na misitu ili kurejesha mazingira, lazima kuthamini na kurejesha mifumo ya ardhini na baharini, kuelewa, kufuatilia, na kulinda bahari hivyo basi ni jukumu la kimataifa lenye athari za kimataifa.
Tunatoa wito kwa majadiliano ya UNFCCC kuingiza hatua za bahari katika matokeo ya ‘Global Stocktake’ na katika mzunguko ujao wa michango iliyopangwa kitaifa (NDCs), kuhakikisha kuwa ahadi zinapimika, za wazi, na zinaweza kutekelezwa.
Ili kufanikisha hili, tunahitaji hatua zifuatazo:
1. Kutambua bahari kama mdhibiti mkuu wa tabianchi ndani ya mikakati ya kitaifa ya tabianchi na mifumo ya kimataifa.
2. Kuhakikisha suluhisho za tabianchi zinazotokana na bahari ni shirikishi, jumuishi na zenye haki, kwa kuzingatia mahitaji ya nchi maskini zaidi, nchi ndogo zinazoendelea za visiwa, na jamii za pwani zilizo mstari wa mbele.
3. Kuharakisha suluhisho za bahari na ukanda wa pwani zinazotokana na asili na kuhakikisha kuwa jitihada za uhifadhi zinaunganishwa na malengo ya kupunguza, kukabiliana na kuongeza ustahimilivu wa tabianchi.
4. Kukuza teknolojia mpya za kufuatilia vitisho vya kudumu na vya vipindi kama vile kuongezeka kwa usawa wa bahari, kuongezeka kwa asidi, kupotea kwa bayoanuai, uchafuzi wa plastiki, uchimbaji rasilimali, na uchafuzi katika mabonde yote ya bahari.
5. Kujenga mifumo madhubuti ya MRV (ufuatiliaji, utoaji taarifa na uthibitishaji) kwa suluhisho mpya za tabianchi zinazotokana na bahari ili kuhakikisha usalama, uimara wa kisayansi, na ulinganifu na malengo ya kitaifa na kimataifa.
6. Kuchochea mifumo bunifu ya fedha iliyo ya uwazi na uhasibu wa kuaminika, ikishirikisha sekta binafsi na wahisani, ili kukuza uhifadhi wa bahari, masoko ya kaboni ya buluu, na suluhisho za bahari.
7. Kujitolea kufadhili ramani, ufuatiliaji, na uchunguzi wa bahari kote kwenye bahari na katika maeneo yanayounganisha bahari na anga au nchi kavu, hasa mifumo inayosaidia kukabiliana na tabianchi na kuongeza ustahimilivu wa nchi maskini zaidi na nchi ndogo za visiwa kwa kutoa taarifa rahisi na zinazoweza kutumika.
Hatua hizi hazipaswi kutenganishwa wala kucheleweshwa, lazima ziunganishwe katika sera zote za tabianchi na uhifadhi, kuanzia tathmini za kimataifa (global stocktake) na ahadi za fedha hadi NDCs, mifumo ya kukabiliana na tabianchi, na mikakati ya mpito yenye haki na lazima wale wanaoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi wapewe kipaumbele.
Misitu na bahari kwa pamoja ndizo suluhisho za asili zenye uwezo mkubwa, za haki, na zilizothibitishwa. Tunapowekeza katika afya yake, tunawekeza katika mustakabali wetu wa pamoja.
Ni kwa kuweka bahari katika kiini cha mikakati ya tabianchi pekee ndipo tunaweza kujenga mustakabali thabiti, wenye usawa, na endelevu kwa wote. Acha mwaka 2025 ukumbukwe kama mwaka ambao dunia iliunganisha ardhi na bahari kulinda uhai wote duniani.
Azimio hilo limetiwa saini na Rais wa Taasisi ya Woods Hole Oceangraphic, Peter de Menocal, Mkurugenzi wa taasisi ya Scripps of Oceanograph ya Chuo Kikuu cha Calfornia San Diedo, Meenakshi Wadhwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya AGU, Jenice R. Lachance na Rais wa taasisi hiyo Brandon Jones.
Wengine ni Mkurugenzi, Sera za Kimataifa wa taasisi wa Carbon to Sea Initiative, Diane Hoskins, Mkurugenzi wa Utawala wa taasisi ya Wakfu wa Utafiti kutoka Sao Paulo (FAPESP) Fernando Menezes, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Fugro, Marl Heine, Mkurugenzi wa kituo cha utafiti cha ‘GEOMAR Helmholtz Centre for Ocean Research Kiel’, Dkt. Katja Matthes na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Ifremer, Francois Houllier.
Wengine ni Rais wa kituo cha Marine Hazards Mitigation Center
Prof. Amr Hamouda na makamu wake Suzan El-Gharabawy, taasisi ya Minderoo Foundation imewakilishwa na Mkurugenzi wa Mifumo ya Ikolojia Asilia, Holly Buschman, jukwaa la Ocean & Climate Platform limewakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Loreley Picourt, Kamishna wa masuala ya bahari kwa nchi za ukanda wa Pacific iliwakilishwa na Kamishna wake Dkt. Filimon Manoni.
Taasisi nyingine zilizotia saini azimio hilo ni Rais wa Ocean Policy Research Institute, Sasakawa Peace Foundation,
Mitsutaku Makino na Rais wa Taasis ya Utafiti wa Bahari na Hali ya Hewa ya Ureno (Portuguese Institute for Sea and Atmosphere) José Guerreiro.
0 Comments