Ticker

7/recent/ticker-posts

ASILIMIA 95 YA TAKA NGUMU ZINAZOCHAFUA BAHARI DAR ZINAZALISHWA NCHINI

Chupa za Plastiki zikiwa zimezagaa ufukweni mwa Bahari.

 
NA JIMMY KIANGO

Wakati dunia ikiendelea kutafakari kile kilichoamuliwa kwenye Mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko Tabianchi  (COP30) kule Belem, Brazili, ukweli mchungu kuhusu mazingira yetu unajificha kwenye fukwe za Dar es Salaam. 

Chini ya mwanga wa jua kali linalochochewa na mabadiliko ya tabianchi, bahari ya Hindi sasa inageuka kuwa jalala la kupokea taka ngumu hasa za Plastiki ambazo kwa kiwango kikubwa zinazalishwa na viwanda vya ndani.


Utafiti uliofanywa na watafiti Florence Jovenary Peter, Mhadhiri Msaidizi Taasisi ya Sayansi ya Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Marc Kochzius, mtafiti wa masuala ya bahari kutoka Chuo Kikuu cha Vrije kilichopo Brussels, nchini Ubelgiji, uliofanywa mwaka 2024 umefichua kile ambacho wengi walikuwa hawakifahamu.

 

Kwa kutumia mbinu za kisayansi (Accumulation na Standing Stock Surveys), watafiti hao walipenya katika fukwe za Selander iliyopo wilaya ya Ilala na Mbezi katika wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam na kutoa matokeo yanayoshtua.


Walibaini kuwa, zaidi ya asilimia 60 ya sumu inayoitafuna bahari ni plastiki ambazo wengi wanaamini zinazalishwa nje ya nchi, ukweli ni kwamba wauaji wakubwa wa viumbe wa baharini na mazingira ya bahari ni viwanda vya ndani hasa vinavyotengeneza vinywaji mbalimbali hasa vile vinavyoongeza msisimko wa mwili (energy drink).


Utafiti huo umethibitisha kuwa asilimia 95 ya taka zenye chapa zinazoingia baharini ni bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. 

Hii inamaanisha  kuwa viwanda vya ndani na mifumo ya  utupaji taka kuanzia majumbani ndiyo adui mkubwa wa bahari.

Mhadhiri Msaidizi Taasisi ya Sayansi ya Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Florence Jovenary Peter 
TAKA ZA PLASTIKI SUMU YA BAHARI
Kuna uhusiano wa karibu kati ya ongezeko la joto ukanda wa pwani, hususan Dar es Salaam na uharibifu wa mazingira ya bahari unaochangiwa na utupaji holela wa taka ngumu za plastiki ambazo haziozi.


Utafiti umebainisha kuwa ongezeko la joto na msongamano wa watu Dar es Salaam ni vichocheo vya matumizi makubwa ya vinywaji baridi ambavyo vingi vimefungashwa katika chupa za plastiki. 


Hii inamaanisha kuwa bila mfumo madhubuti wa urejelezaji (recycling), chupa hizo zitaendelea kutupwa holela kuanzia mtaani, mtoni na kuishia baharini na kusababisha madhara kwa mazingira ya bahari na viumbe vyake ikiwemo kuathiri matumbawe ambayo ni mazalia ya Samaki.


KIWANGO CHA PLASTIKI KINACHOZALISHWA NCHINI

Takwimu kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zinaonesha kuwa takribani kiasi cha tani milioni 7 za taka ngumu huzalishwa hapa nchini kwa mwaka, ambapo wastani wa asilimia 45 hadi 50 ya taka hizo ndio hukusanywa na kutupwa kwenye madampo rasmi, huku asilimia 50 hadi 55 hubaki kwenye mazingira na kuzagaa kwenye mito, mifereji na mitaro ya maji ya mvua.”


Hata hivyo utafiti unaonesha kuna jitihada zimefanyika za kupunguza kasi ya uchafuzi wa mazingira ya bahari unaotokana na taka za plastiki hasa baada ya mwaka 2019 serikali kupiga marufuku ya matumizi ya bidhaa za plastiki.


Marufuku hiyo imesaidia kupunguza kasi ya uchafuzi wa mazingira ya bahari kati ya mwaka 2020 na 2021, lakini utafiti unaweka wazi kuwa wakati wa msimu wa mvua kubwa unageuka kuwa "muda wa maangamizi," ambapo taka nyingi zaidi husombwa na maji na kuelekea baharini.

Mtafiti wa masuala ya bahari kutoka Chuo Kikuu cha Vrije kilichopo Brussels, nchini Ubelgiji,Marc Kochzius.

MATAKWA YA SHERIA
Kifungu cha 114 (1-3) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, iliyofanyiwa maboresho mwaka 2025 kinabainisha wazi kuwa:  (1) Ili kuhakikisha kwamba taka ngumu zinapunguzwa kufikia kiwango cha chini katika maeneo yaliyo chini ya mamlaka yake, Serikali za Mitaa zitaagiza:- 

1. (a)  kwa aina tofauti za taka, takataka, mabaki au uchafu, zichambuliwe na kutenganishwa kwenye chanzo chake; 

2. (b)  kuweka viwango vya kuongoza aina, saizi, umbo, rangi na vipimo vingine kwa ajili ya jaa za taka zinavyotumika; na 


3. (c)  kuweka utaratibu kwa kushirikisha viwanda na sekta binafsi na Asasi Zisizo za Kiserikali katika kupanga, kukuza weledi miongoni mwa wazalishaji, wachuuzi, wasafirishaji, watengenezaji viwandani na watu wengine kwa nia ya kupata jaa zinazofaa kwa taka na utenganishaji wa taka kwenye chanzo. 

(2) Mamlaka ya serikali za mitaa kwenye maeneo yake zitafanya mambo yafuatayo:- 

1. (a)  zitahakikisha Tathmini ya Athari kwa Mazingira inayofaa inafanyika kwa ajili ya shughuli zote kuu mpya zinazolenga kwenye usimamizi unaostahili wa taka ngumu; 

2. (b)  zitasimamia taka ngumu zinazozalishwa kwa mujibu wa mipango endelevu iliyotolewa na serikali za mitaa husika; na 

3. (c)  zitahakikisha uchambuzi wa taka unaostahili unafanyika pale kwenye chanzo na unazingatia viwango au vipimo vilivyoagizwa na serikali husika ya mitaa. 

(3) Kwa madhumuni ya kutoa uamuzi kuhusu ubora wa mbinu yoyote mahsusi ya ukusanyaji, ushughulikiaji wa upunguzaji wa madhara au utupaji wa taka ngumu, mamlaka ya serikali za mitaa itatafiti kwenye maeneo yake kwa lengo la kupata uelewa wa kiwango cha uzalishaji wa taka ngumu na muundo wake. 

 

Aidha Kifungu cha 115(1) cha Sheria hiyo kinazitaka mamlaka za serikali za mitaa kufanya utafiti wa mara kwa mara wa aina ya taka zinazozalishwa katika maeneo yao. 


Agizo hili la kisheria linalenga kujua aina ya taka zinazozalishwa mara kwa mara na kuweka mikakati ya kudhibiti au kuziondoa kwa njia isiyokuwa na madhara kwa mazingira na binadamu. Hata hivyo, utekelezaji wa kifungu hiki umekuwa na kigugumizi. 


SERIKALI YATOA TAMKO
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Bi. Sarah Kibonde, anabainisha Tanzania inaelekea kukamilisha Mpango wa Udhibiti wa Uchafuzi wa Bahari (Marine Litter Action Plan-MLAP) ambao utakuwa mwarobaini wa uchafuzi wa mazingira ya bahari.


“Kazi ya kukamilisha MLPA inafanywa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, lengo likiwa ni kuhakikisha bahari inakuwa salama,” amesema.  

Bi. Sarah, amesema mpango huo unatarajiwa kukamilika mwaka huu na dhamira kuu ni kuhakikisha mazingira ya bahari yanakuwa salama.

“Ofisi ya Makamu wa Rais inakamilisha Mpango wa Udhibiti wa Uchafuzi wa Bahari (Marine Litter Action Plan),”amesema Bi. Sarah.


Mpango huu unakuja wakati ambao viumbe wa majini duniani wanapambana na tani 270,000 za plastiki, huku asilimia 80 ya uchafu huo ukitokea nchi kavu.


Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya Mazingira ya bahari, Dkt. Robert Katekiro ameuelezea mpango huo kama juhudi za makusudi za kulinda mazingira ya bahari ambayo ni tegemeo la kiuchumi kwa jamii za pwani ambazo zinategemea bahari kuendesha maisha yao.


UHAI WA BAHARI UNAHITAJI USHIRIKIANO
Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Rushingisha George,anasema bahari haiwezi kujiokoa yenyewe na kwamba Utafiti wa Jovenary na Kochzius umetoa rai ya ushirikiano wa kimkakati. 


Hii si vita ya Ofisi ya Makamu wa Rais pekee; ni vita inayohitaji wazalishaji wa plastiki, wanaharakati, na nchi jirani tunazoshirikiana nazo katika bahari ya Hindi kuwajibika kwa pamoja.


Kama Mpango wa MLAP hautatekelezwa kwa ukamilifu, nadharia na takwimu zilizokusanywa zitakuwa ni upotezaji wa rasilimali. Bahari safi si anasa, ni uhai.


 

Post a Comment

0 Comments