Ticker

7/recent/ticker-posts

MAFANIKIO NA CHANGAMOTO ZA COP30

*Tanzania imefanikiwa kuwa sauti ya wasio na sauti

NA JIMMY KIANGO

COP30 ilihitimishwa Novemba 22,2025 baada ya zaidi ya wiki mbili za mazungumzo na majadiliano kuhusu hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku Tanzania ambayo ilikuwa ndie Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) ikifanikiwa kuwa sauti muhimu ya Afrika.

Ukweli wa hilo umethibitishwa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Peter Msoffe, ambae amesema Tanzania imeendelea kuimarisha hadhi yake kimataifa, hususan kupitia nafasi ya AGN, jambo lililowezesha ajenda muhimu za bara la Afrika kujadiliwa na kukubaliwa.


Wakati hali ya mazingira ya Bahari yakiwa katika hatari kutokana na kukithiri kwa utupaji wa taka ngumu hasa chupa za Plastiki, mwaka huu mkutano ulilenga kuharakisha utekelezaji wa Makubaliano ya Paris katika kipindi nyeti ambacho malengo ya kimataifa ya tabianchi yako chini ya shinikizo kubwa.


Katika Mkutano huo zaidi ya ujumbe wa nchi 190 ulikutana katika mji wa Belém, uliopo katika eneo la Msitu wa Amazon, wakati ambapo hatua za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zilikuwa hatarini na zaidi ya washiriki 56,000, walihudhuria.


Kimsingi  COP30 ilikuwa ni sawa na mkutano ambao dunia ilipaswa kugeuka kutoka kwenye ahadi kwenda kwenye utekelezaji, ikijijenga juu ya zaidi ya miongo mitatu ya mazungumzo ili kutoa fedha halisi, kulinda mazingira kwa kiwango kikubwa na kurekebisha mwelekeo wa dunia kuelekea lengo la nyuzi joto 1.5°C. 


Lengo halikuwa tu kuendeleza urithi wa mikutano iliyopita, bali kuthibitisha kuwa ushirikiano wa kimataifa (multilateralism) bado unaweza kuleta hatua zenye maana katika dunia inayozidi kuongezeka joto. 


Katika siku za mwisho za mkutano, Katibu Mtendaji wa UNFCCC, Simon Stiell, alisisitiza kuwa: “Maendeleo haya ya vitendo si ya anasa. Ni ya msingi kabisa. Katika enzi hii mpya, mengi yatategemea kuusogeza mchakato wetu karibu zaidi na uchumi halisi, ili kuharakisha utekelezaji na kusambaza faida zake kubwa kwa mabilioni ya watu.”

COP30 ilifanyika katika wakati muhimu kwa ushirikiano wa kimataifa, ikiwa na lengo la kuonesha kuwa utawala wa pamoja wa tabianchi bado unaweza kufanya kazi licha ya mvutano mkubwa wa kijiografia. 


Katika kipindi chote cha mkutano, nchi zilifanya kazi ya kusukuma mbele matokeo ya pamoja ambayo hakuna nchi ingeweza kuyafanikisha peke yake, kuanzia kukubaliana misingi ya ramani ya Fedha za Tabianchi ya Baku hadi Belém, kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zenye misitu, serikali wafadhili na Mashirika ya Umoja wa Mataifa kupitia Mfuko wa Tropical Forests Forever Facility (TFFFF), hadi kuratibu juhudi za kimataifa dhidi ya gesi hatarishi zinazochangia ongezeko la joto kwa haraka kama methane. 


Mafanikio haya ya pamoja yalionesha umuhimu endelevu wa UNFCCC kama jukwaa la majadiliano, likithibitisha kuwa ushirikiano wa kimataifa bado ni muhimu katika kukabiliana na janga linalovuka mipaka yote.


Hata hivyo, matokeo hayakuwa ya miujiza. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema katika hotuba yake ya kufunga mkutano kuwa “COP30 imeleta maendeleo,” lakini akaongeza kuwa “siwezi kujifanya kuwa COP30 imetoa kila kitu kinachohitajika,” akirejea ukosefu wa maendeleo katika kuachana na matumizi ya nishati ya mafuta (fossil fuels) na kushindwa kufikia makubaliano ya pamoja kuhusu kukomesha ukataji miti. 


Kutokana na “kukosekana kwa mwafaka,” Rais wa Brazil,Luiz Inácio Lula da Silva (Lula) alizindua ramani mbili za utekelezaji kwa masuala hayo kama mpango wake binafsi.


MATOKEO MAKUU
Kwa mara ya kwanza dunia ilikubaliana kuwa na kifurushi kikuu cha maamuzi kinachojulikana kama ‘global mutirão’ ambacho kiliunganisha ahadi katika maeneo ya kupunguza hewa chafu, kukabiliana na athari za tabianchi, fedha za tabianchi na ulinzi wa mazingira. 


Ingawa kilikuwa muhimu kisiasa kwa kudumisha uhalali wa mchakato wa Makubaliano ya Paris, kwa kiasi kikubwa kilirudia ahadi zilizokuwepo tayari badala ya kuanzisha wajibu mpya wenye nguvu zaidi.


RAMANI YA FEDHA KUTOKA BAKU HADI BELEM

COP30 iliendeleza Ramani ya Fedha za Tabianchi ya Baku hadi Belém, inayolenga kukusanya dola trilioni 1.3 kwa mwaka ifikapo 2035 kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kupitia vyanzo vya umma, binafsi na misaada nafuu. 


Hata hivyo, taasisi ya ODI na wachambuzi wengine walionya kuwa baadhi ya makadirio katika ramani hiyo yanaweza kuwa na matumaini makubwa kupita kiasi, na kwamba utekelezaji wake utategemea zaidi dhamira ya kisiasa kuliko hoja za kiufundi pekee. 


Zaidi ya hayo, ramani hiyo haikujadiliwa na nchi zote 198 kama ilivyo katika maamuzi ya kawaida ya COP, bali iliandaliwa na Marais wa COP, hivyo uzito wake wa kisiasa bado hauko wazi.


Maandishi yaliyopitishwa COP30 yanatoa wito wa kukusanywa kwa fedha hizo kama zilivyoainishwa katika Ramani ya Fedha, sambamba na lengo la kuongeza mara tatu fedha za kukabiliana na athari za tabianchi (adaptation) na kuanza utekelezaji wa Mfuko wa Hasara na Uharibifu uliokubaliwa COP28.


Hata hivyo, utekelezaji wake utategemea dhamira ya kisiasa ya muda mrefu kutoka kwa uchumi mkubwa wa dunia jambo ambalo halikuonekana wazi Belém.


DHAMIRA MPYA YA BELEM

Matokeo muhimu yalikuwa uzinduzi wa “Dhamira ya Belém”, mpango mpya wa kimataifa unaolenga kuharakisha hatua za pamoja za kupunguza uzalishaji wa gesi chafu duniani. 


Mpango huu unasisitiza ushirikiano kati ya nchi, sekta binafsi na jamii za ndani katika utekelezaji wa suluhu bunifu za tabianchi. 


Unalenga kuongeza matumizi ya nishati jadidifu, kuimarisha uimara wa tabianchi katika maeneo hatarishi, na kukuza ubunifu wa teknolojia endelevu.


Sifa mojawapo muhimu ya dhamira hii ni ahadi ya kuimarisha msaada wa kifedha na kiteknolojia kwa nchi zinazoendelea ili ziweze kutimiza malengo yao ya tabianchi. 

Ingawa umepongeza kwa mtazamo wake jumuishi unaounganisha hatua za tabianchi na maendeleo ya kiuchumi, mafanikio yake yatategemea uwezo wa kudumisha kasi, kupata fedha za kutosha na kuweka mifumo madhubuti ya uwajibikaji. 


Hata hivyo, mkabala wake wa wadau wengi unaonekana kama hatua sahihi katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.


LENGO LA DUNIA LA KUKABILIANA NA ATHARI (GGA)
COP30 iliweka kipaumbele cha kuanzisha viashiria vya kupima utekelezaji wa lengo la dunia la kukabiliana na athari (Global Goal Adaptation-GGA). 

Hata hivyo, licha ya miaka miwili ya kazi ya kitaalamu, mkutano haukuweza kutoa matokeo thabiti. 


Orodha ya viashiria 60 vilivyopitishwa ikiwemo fedha, uhamishaji teknolojia, ujenzi wa uwezo na sera zinazozingatia usawa wa kijinsia ilidhoofishwa na mabadiliko ya dakika za mwisho yaliyopunguza uaminifu na utekelezekaji wake. 


Matokeo yake, nchi zimeachwa bila mwongozo wa kutosha wa kuimarisha mifumo ya kitaifa ya ufuatiliaji kabla ya tathmini ya pili ya kimataifa.


Uamuzi kuhusu Mipango ya Kitaifa ya Kukabiliana na Athari (NAPs) ulipitishwa pia, ukitambua maendeleo ya nchi zinazoendelea lakini pia kuonesha changamoto katika upatikanaji wa rasilimali na taarifa za tabianchi.


 Ingawa ulisisitiza umuhimu wa maarifa ya jamii za asili na sera jumuishi za kijinsia, haukutoa mwongozo wa kutosha kuhusu kuongeza msaada kwa utekelezaji wa NAPs au kuhakikisha uratibu na mifumo mingine kama Mkakati wa Kitaifa wa Bioanuwai. 


Mapengo haya yanaweza kuchelewesha juhudi za kukabiliana na athari, hasa kwa nchi zilizo hatarini zaidi.

USHIRIKI WA ASASI ZA KIRAIA COP30
Asasi za kiraia zilikuwa na mchango mkubwa na unaoonekana wazi COP30, zikionesha nguvu na changamoto za diplomasia shirikishi ya tabianchi. 


Viongozi wa jamii za asili, vijana na wanaharakati walijitokeza kwa wingi Belém, huku maandamano yakifanyika katika kipindi chote cha wiki mbili. 


Mijadala rasmi ya jamii za asili na matukio yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa yaliangazia uongozi wao katika usimamizi wa ardhi na utawala wa tabianchi, huku maelfu wengine wakitoa sauti zao nje ya eneo la maamuzi (Blue Zone). 


Hata hivyo, mkutano uliibua pia migogoro ya kawaida ikiwemo malalamiko ya kubanwa kwa maeneo ya maandamano, migongano na vyombo vya ulinzi na hisia kuwa nguvu halisi ya maamuzi bado haijawafikia kikamilifu asasi za kiraia. 


Hivyo, COP30 ilionesha umuhimu wa asasi za kiraia katika kudai uwajibikaji, lakini pia changamoto za kuhakikisha sauti zao zinaakisiwa ipasavyo katika uamuzi wowote utakaofanywa na Umoja wa Mataifa.

CHANGAMOTO 
Kuandaa COP30 Belém kulibeba alama kubwa ya kimaudhui lakini pia changamoto nzito, zikionesha ugumu wa kuandaa mkutano wa kimataifa katikati ya Msitu wa Amazon. 


Ingawa Brazil ililenga kuonesha uongozi wake wa kimazingira, migogoro ya muda mrefu ya ndani ilijitokeza wazi, hususan pale makundi ya jamii za asili yalipofunga njia za kuingia katika ukumbi wa mkutano wakidai ulinzi zaidi wa ardhi zao na hatua za haraka dhidi ya ukataji miti. 


Maandamano hayo yaliweka wazi pengo kati ya simulizi za kitaifa za tabianchi na uhalisia wa jamii zilizo mstari wa mbele, yakizua maswali kuhusu maslahi yanayowakilishwa kweli ndani ya kumbi za majadiliano.


Wakati huo huo, changamoto za kiusalama na miundombinu zilionesha mgongano kati ya malengo ya tabianchi na uhalisia wa kuandaa mkutano mkubwa. 


Ujenzi wa miundombinu mipya ikiwemo barabara yenye utata ya kilomita 13 ya Avenida Liberdade iliyokatiza msitu unaolindwa, maboresho makubwa ya uwanja wa ndege na jiji, pamoja na upanuzi wa maeneo ya malazi ulikosolewa kwa kusababisha uharibifu wa mazingira na kuweka kipaumbele mahitaji ya mkutano kuliko masuala ya tabianchi ya jamii za eneo hilo. 


Aidha, uzalishaji wa hewa ukaa kutokana na usafiri wa maelfu ya wajumbe kwa ndege, na matumizi ya boti za dizeli kwa malazi, uliibua mvutano zaidi. 

Changamoto hizi zilionesha upinzani katika kuandaa mkutano wa tabianchi katika eneo nyeti la kiikolojia.


Zaidi ya hayo, kutokuwepo au kuwepo kwa kiwango cha chini sana kwa viongozi wakuu kutoka Marekani na China, nchi mbili zinazochangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, kuliweka hatarini uhalali na ufanisi wa COP30. 


Ukosefu wa uwakilishi wa ngazi ya juu kutoka Marekani uliacha ombwe katika ahadi za fedha za tabianchi na juhudi za pamoja za kushughulikia hasara na uharibifu. 


China, ingawa ilishiriki, ilichukua msimamo wa tahadhari, huku mshauri wake mkuu wa tabianchi akisema kuwa Beijing “haitaki kuongoza peke yake” bila uwepo thabiti wa Marekani. 


Hali hii ilidhoofisha mizani ya jadi ya nguvu za tabianchi duniani, ikaongeza sintofahamu kuhusu mgawanyo wa mzigo, na kupunguza mshikamano wa ahadi za muda mrefu.

 

COP30 IMEFANIKIWA

COP30 ilifanikiwa kudumisha muundo mkuu wa Makubaliano ya Paris na kusukuma mbele baadhi ya mipango muhimu kisiasa. 


Ilionesha kuwa hata katika mazingira ya kujiondoa kwa baadhi ya mataifa makubwa, mchakato wa kimataifa bado unaweza kufikia maamuzi ya pamoja. 


Hata hivyo, mkutano haukutoa maamuzi ya mageuzi makubwa yanayohitajika kuiweka dunia katika mwelekeo unaolingana na lengo la nyuzi joto 1.5°C. 


Katika maeneo mengi ikiwemo kuachana na nishati ya mafuta, ukataji miti, kukabiliana na athari na fedha za tabianchi ahadi za Belém zilikuwa zaidi ya kurudia malengo ya awali badala ya kuyazidi.


Ili kuharakisha maendeleo ya kimataifa, shinikizo kubwa zaidi kutoka kwa asasi za kiraia, serikali za kitaifa, sekta binafsi na taasisi za kimataifa litakuwa muhimu. 


COP30 ilidumisha hali iliyopo, lakini juhudi zijazo lazima zipite hatua hiyo kwa uamuzi zaidi ikiwa dunia inataka kukabiliana ipasavyo na mgogoro unaozidi wa tabianchi.

 


Post a Comment

0 Comments