NA JIMMY KIANGO
Shughuli za binadamu zimetajwa kuchangia pakubwa uchafuzi wa mazingira ya Bahari na Pwani, huku utupaji holela wa takataka hasa za plastiki utajwa kuwa ni hatari zaidi.
Takwimu za Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) zinaonyesha kuwa kila mwaka Tanzania inazalisha kiasi cha tani milioni saba za taka ngumu, huku uwezo wa kuzikusanya na kuzitupa kwa utaratibu stahiki ni kati ya asilimi 45 hadi 55,kati ya asimilia 45 hadi 55 hubaki kwenye mazingira na kuzagaa kwenye mifereji, mito na kuishia baharini.
Hii inamaanisha kuwa katika tani milioni saba za taka ngumu zinazozalishwa nchini, takribani kiasi cha tani milioni 3 hadi milioni 3.5 zinaishia baharini kila mwaka. Hatua hii inachangia kwa kiasi kikubwa kuathiri mazingira ya bahari,fukwe na mifumo ya ikolojia ya bahari kwa ujumla
.
Wataalamu wanaweka wazi kuwa uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya bahari una athari kwa Samaki na binadamu kwa kuchangia uzalishaji mkubwa wa joto la bahari na kuharibu matumbawe hali inayochangia kupunguza kiwango cha uzalishaji wa samaki na kushusha kipato cha wavuvi na wachuuzi wakubwa na wadogo wa samaki.
Taka hizo pia zinaathari kwa viumbe bahari vinavyoishi chini ya maji kutokana na baadhi ya taka hasa za plastiki kuwa na madhara ya moja kwa moja kwao.
Ili kuinusuru bahari juhudi za makusudi zinahitajika katika kukabiliana na hali hiyo na katika kulifanikisha hilo ujumbe wa Tanzania ulioshiriki kwenye Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), uliomalizika Novemba 21,2025 jijini Belem, nchini Brazili, uliiona haja ya kusaka fedha zaidi ili kupata nguvu ya kukabiliana na mabadiliko tabianchi.
Kiasi cha ahadi ya zaidi ya trilioni 1.154 kiliahidiwa kwa Tanzania kutoka kwa wadau mbalimbali waliofanya nao mazungumzo pembeni ya mkutano huo uliohusisha nchi zaidi ya 190 na washiriki zaidi ya 56,000. Hata hivyo ili Tanzania ifanikiwe kupata kiasi hicho cha fedha inapaswa kuhakikisha inafuatilia kwa karibu ahadi hizo.
Katika mkutano huo ujumbe wa Tanzania umefanikiwa kupata ahadi ya dola za Marekani milioni 447.12 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 1,103 na kiasi cha Euro 500,000 ambacho ni sawa na zaidi shilingi bilioni 1.461.
Pamoja na ahadi hiyo ya fedha ilizotafuta kwa jitihada zake, Tanzania pia ina nafasi ya kupata kati ya dola milioni tano hadi dola milioni 20 ikiwa ni mgao wa pamoja wa sehemu ya kiasi cha dola milioni 250, zilizoahidiwa kwenye mfuko wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zote.
Katika mazungumzo yake na Afrinews Swahili Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Rushingisha George, amesema kwenye Mkutano wa COP30, Tanzania imefanya jitihada na kufanikisha kupata fedha hizo, hata hivyo haziwezi kufika zenyewe bila kuzifuatilia kutoka kwa walioahidi.
“Hizo fedha ni ahadi, hazijatolewa papo kwa hapo na ili kuzipata lazima uzifuatilie, kimsingi si suala jepesi ila naamini kwa uwezo ambao Tanzania imeuonesha Brazil, uwezekano wa kuzipata upo,” amesema.
| Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Rushingisha George. |
Prof. Msofe, alisema Tanzania inatarajia kunufaika na dola za Marekani milioni 447.12, Euro 500,000 na dola za marekani milioni tano au 20 kutoka kwenye mfuko wa hasara na uharibifu kutokana na ushiriki wake katika mkutano wa COP30.
Mkutano wa wadau ulilenga kujadili fursa mbalimbali katika kusaidia jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kupitia miradi ya mazingira inayotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na wadau.
“Tanzania imeendelea kuimarisha hadhi yake kimataifa kupitia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) ambapo imewezesha na kukukubalika kwa agenda ya nishati safi ya kupikia na upatikanaji wa umeme wa bei nafuu kwa watu wote Afrika.
“Tumepiga hatua kwenye mkutano huo, tumewezesha ofisi ya Kanda ya Santiago Network on Loss and Demage kufunguliwa Dar es Salaam, aidha ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia imekubalika kKimataifa na hii ni agenda inayopewa nguvu na uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.”
| Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Profesa Peter Msofe. |
“Fedha hizo ni ahadi kutoka kwa wadau ambao Tanzania ilikutana na kufanya mazungumzo nao katika kuimarisha jitihada za kitaifa na kimataifa za kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi,” amesema.
Amesema wanufaika wa fedha hizo wanatarajiwa kuwa Watanzania pekee ikiwemo jamii ya Pwani kwa kuwa fedha hizo ziliahidiwa kutolewa baada ya Tanzania kufanya mazungumzo hayo kwa kuzingatia vipaumbele vyake wakati wajumbe wa Tanzania walipokutana na wawakilishi na watendaji kutoka taasisi au mashirika husika.
Bi. Kibonde amesema: Sababu kuu ya kutafuta fedha hizo ni kuimarisha jitihada za kukabiliana na Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi. Mkutano wa COP30 umekuwa nyenzo na jukwaa muhimu la kukutana na wadau mbali mbali wa kimataifa katika jitihada za kukabiliana na Mabadiliko Tabianchi.”
0 Comments