NA JIMMY KIANGO
Katika hali inayozua wasiwasi wa kimazingira jijini Dar es Salaam, wataalamu na wananchi katika Wilaya ya Kinondoni wameziomba mamlaka, ikiwemo Halmashauri ya Manispaa na Baraza la Taifa la Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira (NEMC), kuchukua hatua za dharura kudhibiti uchimbaji mchanga holela katika mito na mabonde.
Ushauri huo unakuja wakati shughuli hizo zikishamiri kwa kasi, huku zikiacha makovu makubwa ya kimazingira ikiwemo kubomoka kwa kingo za mito, tishio la kuongezeka kwa kasi ya mafuriko, na uharibifu wa makazi ya watu.
UUCHIMBAJI ENDELEVU
Profesa Pius Yanga, Mkurugenzi wa Kituo cha Masomo ya Mabadiliko ya Tabianchi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CCCS-UDSM), anabainisha kuwa suluhu si kuzuia kabisa, bali ni kuweka taratibu madhubuti.
Kulingana na Profesa Yanga, uchimbaji ukiratibiwa kitaalamu, unaweza kuwa sehemu ya suluhu ya kusafisha mito na kuongeza kina chake.
“Uchimbaji usiofuata utaratibu unaharibu muundo asilia wa mito na kuifanya iwe na kona nyingi zisizo za asili. Hii inasababisha mito kuhama mkondo na kuelekea kwenye makazi ya watu wakati wa mvua nyingi hivyo kusababisha mafuriko,” anafafanua Profesa Yanga.
Aidha, alionya kuwa kuacha vijana wajiongoze kiholela kunahatarisha maeneo oevu na vichaka vya asili, jambo ambalo linaathiri bayoanuai na kupunguza uwezo wa asili wa ardhi kunyonya au kupunguza kasi ya maji ya mvua.
VIJANA WAOMBA MWONGOZO
Upande wa pili wa sarafu, wachimbaji mchanga wanadai kuwa shughuli yao ni chanzo cha kipato na pia ni kazi inayosaidia kusafisha mto.
Jeremia Kitomali, mchimba mchanga anayeendesha shughuli hiyo katika mto Nyakasangwe wilayani Kinondoni anasema kwa sasa wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara kutokana na kukosa vibali rasmi.
“Tunapata kipato na tunafanya usafi wa mto, lakini tunakamatwa. Tunaiomba serikali itutambue na kutupa mwongozo na vibali ili tufanye kazi hii kwa amani,” amesisitiza Kitomali.
Hoja hiyo inaungwa mkono na John Chinguku, Mshauri wa mradi wa OYE, unaoshusika na utunzaji mazingira ambae anasisitiza kuwa kutenga maeneo rasmi kutasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira huku uikiimarisha usalama wa maisha ya wananchi.

NEMC NA WITO WA KUSHIRIKIANA
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuweka wazi kuwa NEMC iko tayari kuwaratibu vijana katika vikundi ili wafanye shughuli hiyo kwa uendelevu.
Dkt. Semesi ametoa wito kwa halmashauri za wilaya, wasimamizi wa mabonde, na Kamisheni ya Madini kushirikiana katika kuwasaidia vijana ikiwa ni pamoja na kutengeneza mwongozo wa uchimbaji mchanga katika maeneo yao.
Hata hivyo, pendekezo kama hili liliwahi kutolewa mwaka 2020 na mtangulizi wake, Dkt. Samuel Gwamaka, lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.
“Ni muhimu kulinda miundombinu ya serikali inayotumia fedha nyingi za walipa kodi. Uchimbaji ukiratibiwa, gharama za kukarabati miundombinu inayoharibiwa na mafuriko itapungua kwa kiasi kikubwa,” alihitimisha Dkt. Semesi.
HALI HALISI
Ni dhahiri kuwa mgongano uliopo kati ya mahitaji ya kiuchumi ya vijana na kulinda mazingira unahitaji busara ya kiutawala badala ya nguvu za kisheria pekee.
Serikali kupitia NEMC na Manispaa haina budi kuacha kuchelewa; ni wakati wa kugeuza uchimbaji mchanga kutoka kuwa adui wa mazingira badala yake kuwa mshirika wa uhifadhi, kwa kuweka miongozo thabiti na kuunda vikundi rasmi vya wachimbaji, hatua itakayosaidia kuokoa kingo za mito na kulinda maisha na mali za wakazi wa Kinondoni dhidi ya ghadhabu ya mabadiliko ya tabianchi.
0 Comments