Ticker

7/recent/ticker-posts

TANZANIA YATUMIA MBINU SHIRIKISHI KULINDA BAHARI, MATUMBAWE

 


Matumbawe ni makazi na sehemu muhimu ya mazalia ya samaki Baharini.



NA JIMMY KIANGO

“Bahari hii imetulisha tangu enzi za babu zetu,” anasema Salum Juma, mvuvi wa anaefanya shughuli zake kwenye mwale wa Kivukoni, jijini Dar es Salaa. “Tulipokuwa tunatupa taka holela na tunavua ovyo, tulidhani bahari haina mwisho. Lakini ilipoanza kutuacha, ndipo tulielewa kosa letu.”

Kwa miaka mingi, utupaji wa taka ngumu usiozingatia kifungu cha 117 (a,b) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, ukataji wa mikoko,  uvuvi haramu, matumizi ya baruti, nyavu haribifu na athari za mabadiliko ya tabianchi zilianza kuharibu mifumo ya ikolojia ya bahari. 


Matumbawe ambayo ni mazalia ya samaki na kinga dhidi ya mmomonyoko wa fukwe yalianza kufa kimya kimya, jambo la kushukuru athari zake zimeonekana na sasa badala ya kutumia nguvu za dola pekee, Tanzania imechagua njia tofauti ambayo ni kuishirikisha jamii hasa ya pwani katika kuilinda bahari na ikolojia yake.


JAMII KWANZA, BAHARI INAFUATA

Kupitia mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Bahari, serikali kwa kushirikiana na halmashauri, wanasayansi, Taasisi zisizo za kiserikali na wananchi, ilianza kuwapa jamii mamlaka ya kulinda rasilimali zao.


Katika vijiji vya pwani ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam Lindi na Mtwara, kamati za mazingira za vijiji zilianzishwa. Wavuvi wakageuka kuwa walinzi wa bahari.

“Sasa sisi wenyewe tunapiga doria,” anaeleza Asha Rashid, mwanakamati wa mazingira kijiji cha Kigombe.

“Ukiona mtu anaharibu matumbawe, hatusubiri polisi ama Askari wa uhifadhi, tunaanza sisi kukemea.”

MATUMBAWE YANAPUMUA TENA

Katika baadhi ya maeneo yanayolindwa na mamlaka  za Serikali na zile za jamii, Marine Protected Areas (MPAs) na Community Conservation Areas, dalili za matumaini zinaonekana. 


Samaki wameanza kurejea, matumbawe yanaota upya, na kipato cha wananchi kinaimarika kupitia uvuvi endelevu na utalii wa ikolojia.

Juma Mbarouk, kijana aliyekuwa mvuvi wa baruti sasa ni mwongozaji wa watalii wa miamba ya matumbawe.
“Ninapata kipato kizuri bila kuharibu bahari. Wageni wanakuja kuona matumbawe yaliyo hai, siyo yaliyokufa,” anasema kwa tabasamu.

SAYANSI, MILA NA USHIRIKIANO

Kilichoifanya Tanzania ifanikiwe ni kuchanganya maarifa ya kisayansi na uzoefu asili wa jamii. 

Wazee wa pwani walishirikishwa kueleza misimu ya samaki, maeneo matakatifu ya bahari na historia ya matumizi ya rasilimali.


“Bahari ina sheria zake,” anasisitiza Mzee Salum.
“Ukizivunja, itakuadhibu. Serikali iliposikiliza sauti zetu, mambo yakaanza kubadilika.”

Miti ya Mikoko ambayo ni chujio la Bahari na makazi ya viumbe bahari mbalimbali.

SOMO KWA VIZAZI VIJAVYO

Hadithi ya ulinzi wa bahari Tanzania si hadithi ya sera pekee ni hadithi ya watu. Ni ushahidi kuwa uhifadhi hauwezi kufanikiwa bila kuwashirikisha wale wanaoishi na bahari kila siku.

Kwa jamii ya pwani, ujumbe ni mmoja:
bahari si ya serikali peke yake, ni ya wote na ulinzi wake unaanza na sisi.

SERIKALI YAJIVUNIA

Katika mahojiano yake na mwandishi wa makala haya mapema mwezi huu, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema kuwa jamii hususan jamii za wenyeji wa pwani wamekuwa wakishirikishwa kikamilifu katika shughuli za ulinzi na uhifadhi wa matumbawe na wao ndio wamekuwa walinzi wakuu na mafanikio yameonekana.

 

Mhandisi Luhemeja alifafanua kuwa mbinu ya kuishirikisha jamii imefanikisha wananchi kupata manufaa ya haki na yanayoonekana kupitia fursa za kipato zinazostahimili mbadiliko ya tabianchi.


TANZANIA KIMATAIFA

Kutokana na mafanikio hayo ya kushirikisha jamii, Tanzania iliweza kuwa darasa kwa nchi nyengine kwenye Mkutano wa Saba wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA 7) uliofanyika jijini Nairobi, Kenya mwanzoni mwa mwezi huu.

 

Pembeni ya mkutano huo, Desemba 10,2025, Mhandisi Luhemeja alishiriki mjadala kuhusu ‘Kutumia sayansi pamoja na maarifa ya asili kwa ajili ya kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha uhifadhi wa mazingira’.

 

Katika mchango wake, Mhandisi Luhemeja aliwasilisha uzoefu wa Tanzania katika kufanikisha uhifadhi wa miamba ya matumbawe kupitia mbinu shirikishi.

 

Alieleza kuwa jamii hususan jamii za wenyeji wa pwani wamekuwa wakishirikishwa kikamilifu katika shughuli za ulinzi na uhifadhi wa matumbawe.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja 
Alisema mbinu ya kuishirikisha jamii imefanikisha wananchi kupata manufaa ya haki na yanayoonekana kupitia fursa za kipato zinazostahimili mbadiliko ya tabianchi.

 

Washiriki wa mjadala huo walikuwa ni pamoja na mawaziri wa mazingira, viongozi wa jamii za asili, watafiti, wataalamu wa mazingira na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na hifahi ya mazingira kutoka Afrika, Amerika ya Kusini na maeneo mengine ya dunia.

 

Lengo lilikuwa ni kubadilishana uzoefu, kushauriana na kuweka mikakati ya pamoja ya kujenga ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi katika ikolojia ya bahari na miamba ya matumbawe.

 

Mkutano huo uliwashirikisha wakuu wa nchi na serikali, mawaziri wanaoshughulikia Mazingira, wataalam na wadau wa Mazingira na maendeleo endelevu kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia.

 

Mada kuu katika mkutano huo ilikuwa ni "Kukuza Suluhu endelevu kwa ajili ya sayari yenye ustahimilivu".

 

Aidha, Mkutano huu uliofanyika siku chache mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi-COP30 uliofanyika Belem nchini Brazili mwezi Novemba, ulijadili na kupitisha maazimio na maamuzi mbalimbali yanayohusu mabadiliko ya tabianchi, hifadhi ya bioanuai na udhibiti wa uchafuzi wa Mazingira duniani. Mkutano huo uliokuwa wa siku tano ulihitimishwa Desemba 12, 2025



 

Post a Comment

0 Comments