Mwenyekiti wa Kundi la majadiliano la Afrika Kuhusu Mabadiliko Tabianchi (AGN)Dkt. Richard Muyungi.
NA JIMMY KIANGO
Jumla ya Watanzania sita (6) wameteuliwa kuwemo kwenye kamati mbalimbali za Kimataifa zinazohusika moja kwa moja na maamuzi ya masuala ya kukabiliana na athari za Mabadiliko Tabianchi.
Hatua hiyo ni matunda ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kwenye eneo la kukabiliana na athari za Mabadiliko Tabianchi huku ikiwa nchi Mwenyekiti wa Kundi la majadiliano la Afrika Kuhusu Mabadiliko Tabianchi (AGN) kwenye Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) uliofanyika Belém, Brazil, kuanzia 10 hadi 21 Novemba 2025.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kundi la majadiliano la Afrika Kuhusu Mabadiliko Tabianchi (AGN) ambae pia ni Mshauri wa Rais wa Jamahiri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye masuala ya Mazingira, Dkt. Richard Muyungi.
Kwenye eneo la Uhifadhi wa Bahari, Dkt. Muyungi alisema tayari kuna mikakati inaendelea ili kuilinda bahari ambayo ni muhimu katika kunyonya gesi joto na miongoni mwa watu waliopewa jukumu hilo ambao ni wasaidizi wake wawili mmoja ni Mtanzania na mwengine ni Mghana.
Ingawa Dkt. Muyungi hakutaja majina ya Watanzania hao, lakini alisema miongoni mwao wapo walioteuliwa kuwa Wenyeviti wa Kamati hizo, ikiwemo Kamati ya Kujenga Uwezo (Capacity Building Commetee).
“Hii ni hatua kubwa sana kwetu kama nchi, si jambo rahisi nchi kufanikiwa kuingiza watalaamu sita kwenye kamati mbalimbali za dunia zinazosimamia masuala ya Mabadiliko Tabianchi, ila sisi tumeweza na kuna mambo mengi mazuri tumefanikiwa kuyapata ila naamini yatawekwa wazi kwenye mkutano wa wataalamu na wadau wa Mazingira walioshiriki Mkutano wa COP 30,”amesema.
Akizungumzia mkutano huo wa Wataalamu na wadau wa Mazingira kutoka serikalini na sekta binafsi wanaotarajiwa kukutana leo Desemba 17,2025, jijini Dar es Salaam kujadili na kuweka mikakati ya namna sahihi ya kutekeleza uamuzi uliofikiwa kwenye Mkutano wa COP30.
Katika mkutano wa COP30, Tanzania ilibeba agenda zaidi ya 12 muhimu, miongoni mwake zikiwa ni umuhimu wa ulinzi wa Bahari kwa mustakabali wa nchi na upatikanaji wa njia sahihi za kuiwezesha jamii kuweza kukabiliana na mabadiliko Tabianchi.
Pamoja na kuwa na agenda lukuki, katika mkutano huo Tanzania pia ilikuwa ndio sauti ya pamoja ya vipaumbele vya Afrika kutokana na kuwa na nafasi ya Uenyekiti wa AGN huku agenda kuu ikiwa ni matumizi ya Nishati safi ya kupikia lengo likiwa ni kupambana na kupunguza kiasi cha uchafuzi wa anga.
Katika ufafanuzi wake kwenye suala la ulinzi wa Bahari dhidi ya utupaji wa taka ngumu za Plastiki na ni namna gani jamii ya pwani itanufaika na kile kilichoamuliwa COP30, Dkt. Richard Muyungi, alisema ingawa suala la ulinzi wa bahari halikuwa moja ya agenda kuu kwenye mkutano huo, lakini lilijadiliwa kutokana na umuhimu wa Bahari katika kunyonya gesi joto na kuna mambo mbalimbali yameamuliwa kwa maslahi ya bahari na wakazi wa pwani.
“Yapo mambo muhimu yamejadiliwa juu ya uhifadhi wa bahari kwa mustakabali wa dunia na tumekubaliana kutafuta namna sahihi ya kushughulikia ulinzi wa bahari na majawabu yake yanapaswa kupatikana kwenye Mkutano wa COP32, utakaofanyika Ethiopia.”amesema.
Kutokana na umuhimu wa mkutano huo wa leo, Rais, Dkt. Samia , ambae ndie kinara wa agenda ya Nishati Safi ya Kupikia Tanzania na Afrika kwa ujumla anatarajiwa kuuongoza.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa wa kimkakati unaolenga kuzifungamanisha ahadi za kimataifa na vipaumbele vya nchi katika kuchochea maendeleo endelevu na kukabiliana na athari za Mabadiliko Tabianchi.
Kwa uapande wake Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Human Dignity and Environmental Care Foundation (HuDEFO), Sara Pima, ametoa wito kwa mkutano huo kuzipa nafasi zaidi sauti sauti za jamii zilizo mstari wa mbele katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.
“Ni lazima tukubali kuwa jamii haziwezi kuwa watazamaji wa maamuzi yanayohusu maisha yao. Kikao hiki kiwe mwanzo wa kuhusisha kwa dhati wanawake, vijana na makundi yaliyo pembezoni ili hatua za baada ya COP30 ziwe na haki, usawa na matokeo ya kudumu.”amesema Pima
Amesisitiza kuwa wanawake, vijana na jamii za vijijini bado hazipati nafasi ya kutosha katika upangaji na utekelezaji wa miradi ya tabianchi, hali inayodhoofisha ufanisi wa maamuzi yanayofikiwa katika mikutano ya kimataifa.
Aidha Mkutano huo utakuwa ni sehemu muhimu kwa wataalamu wa Tanzania kutafsiri uamuzi wa COP kutoka kuwa wa kimataifa na kuwa wa kitaifa lengo likiwa ni kurahisha utekelezaji utakaowahusisha wananchi moja kwa moja.
Dkt.Muyungi, aliweka wazi kuwa mkutano huo ni muhimu kwa nchi kwani ndio utakaotoa taarifa za kina za kile kilichofanywa na ujumbe wa Tanzania nchini Brazil.
“Kitu cha muhimu kwetu baada ya kumalizika kwa COP30, si kuendelea kuishi kwa ahadi, badala yake utekelezaji ndio unapaswa kupewa nafasi. Muhimu kwetu ni kuwa na mifumo ya kitaifa itakayopima matokeo, kuonyesha nani anawajibika kwenye nini na kuhakikisha fedha za tabianchi zinafika kwenye jamii zenye uhitaji.
“Muhimu ni kuimarisha mifumo ya uwajibikaji na kuzitafsiri kwa vitendo ahadi zilizotolewa ambazo zilijumuisha mataifa yote na kuzibadili ili ziwe mipango na mikakati yenye tija kwa nchi.”
Amesema Tanzania inapaswa kuimarisha mifumo ya uwajibikaj.”
Mkutano huo unatarajiwa kutoa mwelekeo wa pamoja kuhusu vipaumbele vya utekelezaji wa maamuzi ya COP30, mgawanyo wa majukumu kwa taasisi husika na mfumo wa kufuatilia matokeo, huku kiu ya wakazi wa pembezoni mwa fukwe na Bahari ikiwa ni kataka kuona ahadi za kimataifa zikigeuka kuwa mabadiliko yanayoonekana katika maisha yao ya kila siku.
0 Comments