| Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima |
NA.JIMMY KIANGO
Wakati idadi ya vijana Tanzania ikikadiriwa kuwa milioni 21.3 kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022, ni vijana 630 pekee ndio wamepata fursa ya kushiriki katika kupata asilimia 30 ya manunuzi ya umma.
Hatua hii inadhihirisha wazi kuwa idadi kubwa ya vijana nchini, hawana uelewa wowote juu ya kuchangamkia fursa hiyo ya kiuchumi, ingawa kifungu cha 64(1) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2023 kinazitaka taasisi zote za umma kutekeleza mifumo ya manunuzi yenye ujumuishaji kwa kuweka utaratibu maalum wa kutenga sehemu ya zabuni za umma kwa makundi maalum, yakiwemo wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu, kwa lengo la kukuza usawa wa kijamii na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Lakini pia, kifungu cha 64(2) cha sheria hiyo kinaipa nguvu Mamlaka za Udhibiti wa Manunuzi ya Serikali (PPRA), kutoa kanuni na miongozo ya kuhakikisha utekelezaji wa sharti hilo unafanyika kwa ufanisi na uwazi.
Kwa kuzingatia matakwa hayo ya kisheria, PPRA imeweka miongozo inayotaka kila taasisi ya umma kutenga angalau asilimia 30 ya thamani ya manunuzi ya umma kwa makundi maalum ambayo ni 10% kwa vijana, 10% kwa wanawake, 5% kwa wazee na 5% kwa walemavu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kutumia manunuzi ya umma kama chombo cha kupunguza umasikini, kuongeza ajira na kukuza biashara za wananchi wa ndani.
Hata hivyo hali ni tofauti nchini, na hasa wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo vijana wengi waliozungumza na mtandao huu hawana uelewa wowote juu ya suala la manunuzi ya umma na fursa zilizopo kwenye eneo hilo.
Seif Mkumbo mkazi wa Nyakasangwe, Kinondoni, Dar es Salaam anaejihusisha na shuguli za usafirishaji abiria kwa njia ya pikipiki maarufu kama bodaboda, amebainisha kuwa hajui chochote kuhusu jambo hilo.
“Niwe mkweli, sina nijuacho kwenye suala la manunuzi ya umma, na hii inamaanisha kuwa hata fursa zilizopo kwenye manunuzi hayo sizijui,”amesema Mkumbo.
Khaleed Said kijana mwenye umri wa miaka 32, msomi wa shahada ya kwanza ya mawasiliano ya umma ameiambia Afrinewsswahili kuwa anajua suala la manunuzi ya umma, lakini hakuwa akijua chochote juu ya kutengwa kwa asilimia 30 zinazogusa makundi maalum wakiwemo vijana.
“Hii ni habari kubwa sana, sikuwa najua chochote juu ya fursa hii, mimi niliamini masuala ya manunuzi ya umma yanawahusu watu wenye mitaji mikubwa pekee, na sikuwahi kufikiri kama vijana tuna fursa kubwa kama hii.”
watu wenye ulemavu 25, na wazee 42, ikiwapa fursa ya kushiriki asilimia 30 ya manunuzi ya umma.
Kwa upande wake Jenester Simon, kijana mfanyabiashara wa vinywaji baridi, nae ni miongoni mwa vijana waliokiri kutokuwa na taarifa yeyote juu ya fursa zilizopo kwenye manunuzi ya umma.
Anna Kamugisha anasema kuwa anajua juu ya manunuzi ya umma, lakini hakuwa na uelewa kama na yeye ni mnufaika wa fursa hiyo.
VIGEZO VYA KUPATA FURSA YA 30%
Ili kupata fursa hiyo ni lazima kila kikundi kihusishe asilimia 70 ya wahusika na asilimia 30 inaweza kujumuisha watu tofauti.
Kikundi ni lazima kiwe kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria na uongozi wake unapaswa kuhusisha wahusika wa ndani na si wageni.
Afisa Sheria wa PPRA, Maria Mng’ong’o amefafanua kuwa ili kikundi cha vijana kikidhi vigezo vya kunufaika na fursa hiyo ni lazima asilimia 70 ya wahusika iwahusishe vijana wenye umri wa kati ya miaka 18-35 na asilimia 30 inaweza kujumuisha vijana wenye umri wa zaidi ya miaka 35.
“Hii ni fursa na upendeleo maalum kwa vijana, kwa sababu pia unatolewa kwa ngazi ya mikoa na wanufaika ni vijana waliounda vikundi rasmi kwenye mikoa husika na upendeleo wa asilimia 100 utawalenga vijana au makundi maalum ya mkoa husika,” amesema.
Juu ya vijana wengi kutokuwa na elimu ya fursa hiyo, Mng’omng’o amesema juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa ili kuwafikia vijana wengi zaidi na makundi mengine maalum yaliyotajwa na sheria.
WAZIRI GWAJIMA ATOA NENO
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuwa ndani ya siku 100 tangu kuapishwa kwa Awamu ya Pili ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na mafanikio katika kuwawezesha vijana na makundi maalum nchi nzima.
Amesema Serikali imetekeleza urasimishaji wa vikundi 1,216 katika ununuzi wa umma (NeST), ambapo vikundi 1,123 vimepata zabuni, ikiwemo wanawake 426, vijana 630, watu wenye ulemavu 25, na wazee 42, na lengo la kufanya hivyo ni kuwapa fursa ya kushiriki asilimia 30 ya manunuzi ya umma.
“Mafanikio haya ni misingi ya uchumi jumuishi, shindani na endelevu, na serikali itaendelea kushirikiana na wizara, taasisi, sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma.”amesema Dkt. Gwajima
MAFANIKIO YA JUMLA
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 25, 2026 jijini Dodoma, Waziri Dkt.Gwajima amesema jumla ya Wafanya biashara ndogo ndogo (WBN) 119,595 wamepata usajili rasmi kupitia Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Wafanyabiashara Ndogondogo (WBN–MIS), ikiwemo wanawake 73,341 na wanaume 46,254. Miongoni mwao, Machinga 103,102, Mama na Baba Lishe 12,384, na waendesha bodaboda na bajaji 4,109.
Amesema urasimishaji na uwezeshaji wa wafanyabiashara ndogondogo na wajasiriamali katika sekta isiyo rasmi ni miongoni mwa mafanikio makubwa yanayopimika na yenye kugusa moja kwa moja maisha ya wananchi katika utambuzi.
Wizara imetoa Shilingi 10.5 bilioni kwa ajili ya mikopo yenye riba ya asilimia 7 kwa wafanyabiashara ndogondogo, ambapo tayari Shilingi 1.35 bilioni zimekwishatolewa kwa wafanyabiashara 588 kupitia Benki ya NMB.
Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Shilingi 337.97 milioni zimetolewa kwa wanawake wajasiriamali 45 kwa riba ya 4%.
“Kupitia TRA, waendesha bodaboda na bajaji 209,632 wamepata leseni za udereva, na kupitia mfumo wa Wezesha Portal, jumla ya vikundi 6,041 vimepatiwa usajili na kufanikishwa kupata mikopo, ikiwemo vikundi vya wanawake 3,207, vijana 2,318 na watu wenye ulemavu 516, vikijumuisha wajasiriamali 30,205.”amesema Dkt.Gwajima
Hata hivyo Dkt.Gwajima amesema kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ushirikiano na SIDO, wajasiriamali 16,325 wamepata urasimishaji, 11,000 wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali, na zaidi ya watu 3,900 wamenufaika na namba za mlipa kodi (TIN) na leseni za biashara.
Pia, mikopo 265 yenye thamani ya Shilingi 1.08 bilioni imetoa ajira 652, ambapo ajira za vijana ni 489.
Amesema kuwa Sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na madini zimepata usajili na uwezeshaji wa wajasiriamali na wafanyabiashara ndogondogo, ikiwemo wakulima 532,023, wavuvi 2,100, wafugaji viumbe maji 2,478, na wachimbaji wadogo wa madini 2,239.
Jumla ya Shilingi 33.45 bilioni zimepatiwa vikundi mbalimbali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mfumo wa Halmashauri.
“Serikali imeongeza huduma karibu na wananchi kupitia midahalo ya makundi rika 9,545, mfumo wa mawasiliano mtandaoni www.nis.jamii.go.tz, na kituo cha huduma kwa wateja ambacho kimepokea changamoto 425,075.
Sekretarieti ya Jukwaa la Kitaifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi imezinduliwa kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kiuchumi kutoka sekta zote.”amesema
Aidha Dkt.Gwajima amesema kuwa huduma za ustawi wa jamii pia zimeimarishwa, ikiwemo walengwa 171,529 kuhusiana na Wazee, watoto, wenye ulemavu na manusura wa ukatili, huku watoto 2,699 wameunganishwa na familia zao.
Aidha madawati 2,479 maalum ya kutatua changamoto za watu wazima katika vituo vya usafirishaji yametoa hudumia stahiki kwa wahusika.
0 Comments