Ticker

7/recent/ticker-posts

UCHAFUZI WA VYANZO VYA MAJI MTO KIZINGA, TBL, WWF WANUSURU AFYA ZA WANANCHI BUZA

Timu ya Wataalmu kutoka WWF, Bodi ya Maji Bonde la WamiRuvu na Waandishi wa Habari wakikagua mradi wa Usalama wa Maji Dar es Salaam.

NA. JIMMY KIANGO
Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF-Tanzania) kwa kushirikiana na taasisi ya AbinBev ya Afrika Kusini ambayo inamiliki Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), imeweza kunusuru afya za wakazi wa eneo la Barabara ya mwinyi Buza kwa Lulenga, Temeke, Dar es Salaam.

Watoto na wakazi wa eneo hilo ambao wengi wao wanajihusisha na kilimo cha mbogamboga pembezoni mwa mto Kizinga, walikuwa wakisumbuliwa na vikohozi, magonjwa ya tumbo, kuchanika kwa ngozi sanjari na maradhi ya funguzi za miguu na mikono.


Madhara hayo yalisababishwa kwa kiasi kikubwa na maji ya sumu yanayotiririka kutoka kwenye chemchem zilizopo kwenye dampo lisilo rasmi la Kanisani, ambalo sasa limefungwa kutokana na jitihada za WWF na TBL.


Kimsingi hali hii imesababishwa kwa kiasi kikubwa na utupaji taka ngumu usiozingatia kifungu cha 114-119 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira kwa kisingizio cha kuinusuru ardhi yao iliyokuwa ikimomonyoka na kuvunja makazi yao.

 

Hatua hii ililisukuma shirika la WWF kwa kushirikiana na TBL, Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, Halmashauri ya Temeke na wananchi kutafuta namna ya kukabiliana na changamoto hiyo na ndipo hapo ikaonekana ipo haja ya kujenga mtambo maalum utakaosaidia kuchuja sumu hiyo iliyokuwa ikiwaathiri wakazi wa maeneo hayo.

 

UJIO WA MRADI WA USALAMA WA MAJI DAR 

Akiuzungumzia ujio wa mradi wa Usalama wa Maji Dar es Salaam (Dar es Salaam Water Security) Msimamizi wa mradi huo kutoka WWF, Mhandisi John Kassambili, amesema  mradi huo unahusu Usalama wa Maji kwa Dar es Salaam na miji ya pembezoni.

 

Mhandisi Kassambili amesema mradi huo wa miaka mitatu ulizinduliwa Januari 2022 na aliyekuwa Niabu Waziri wa Maji, Meryprisca Mahundi ukihusisha maeneo ya uwanda wa chini wa mto Ruvu(Lower Ruvu), Mto Kizinga na Mto Msimbazi.

 

MALENGO YA MRADI

Mhandisi Kassambili amesema mradi umekuwa na malengo mbalimbali ikiwemo kutathmini hali ya vyanzo vya maji, hali iliyopo na nini kifanyike.

 

Malengo mengine ni utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kutunza na kuhifadhi rasilimali za maji kwa kutumia njia za asili (Nature based Solution) kwa kuzingatia sera ya maji kama mwongozo na Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya maka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, ambayo imeelekeza kwamba usimamizi wa rasilimali za maji unapaswa kuwa shirikishi.

 

“Kwa hiyo katika miradi yetu ambayo mradi umetekeleza katika maeneo ambayo nimeyataja umekuwa ukishirikisha jamii kikamilifu  kwa maana kwamba katika kila hatua jamii imehusishwa na imeshikiriki kikamilifu.

 

Bango la tahadhari ambayo haitekelezwi kwani shughuli za kilimo zinaendelea chini ya bango hilo.

“Hapa tulipo ni eneo la barabara ya Mwinyi katika Kata ya Kiburugwa eneo la Buza, Manispaa ya Temeke kama unavyoona ni eneo la dampo lisilo rasmi.

 

“Baada ya kukutana na wadau na kuainisha changamoto ambazo zinahusika na utupaji wa taka kwenye mto Kizinga, tulishirikiana wakazi, Kanisa lililopo eneo hili, halmashauri husika na mamlaka ya Bonde la Maji la Wami Ruvu na kuona ipo haja ya kuchukua hatua.

 

“Tuligundua kuna tatizo la mmomonyoko wa udongo uliosababisha baadhi ya nyumba kuanguka na kuacha mashimo makubwa.

 

“Hatua ya kwanza iliyochukuliwa na wananchi kwa kushirikiana na serikali za mitaa walikubaliana kumwaga taka kwenye mashimo hayo. 

 

“Walichukua hatua hiyo kama njia mbadala ya kunusuru mmomonyoko wa ardhi uliojitokeza mahali hapa, lakini tulikuja kugundua kuwa walichukua hatua hiyo kama hatua  ya haraka ila hawakujua madhara ambayo yangekuja kutokea baadae endapo dampo hili lingeendelea kutumika.

Sehemu ya mtambo wa kuchuja sumu iliyomo kwenye maji yanayotiririka kutoka kwenye dampo lisilo rasmi.
“Kwa hiyo tulifanya tathmini ya awali na kuja na mapendekezo kadhaa, ambayo ni kuelimisha wananchi kwa kufanya vikao na mikutano ya hadhara kwa kushirikiana na serikali za mitaa ya maeneo ya hapa na pili ilikuwa ni kuweza kuangalia nini kifanyike ili kunusuru hali ya maeneo haya.”

 

HALI ILIVYOKUWA AWALI

Mhandishi Kassambili anasema eneo hilo lilikuwa haliwezi kukalika kwa sababu taka zilizokuwa zinatupwa kutoka maeneo mbalimbali zilikuwa zinatoa harufu mbaya na wadudu wakiwemo nzi na funza, uchafuzi wa hali ya hewa, kimsingi hali hiyo ilikuwa inasababisha matatizo ya kiafya kwa wananchi.

 

Anasema kwa kushirikiana na serikali za maeneo husika walianza kuchukua hatua baada ya kuona madhara yanayotokana na dampo kwa sababu maji yanayojichuja kutoka kwenye dampo hilo yalikuwa yanaingia kwenye mto Kizinga na mengi yakiwa na sumu.

 

Ikumbukwe kuwa maji ya mto Kizinga yanategemewa kwa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo na shughuli nyengine za kibinadamu.

 

“Mradi uliona haja ya kujenga chujio dogo ili kuangalia kama kuna uwezekano wa kupunguza au kuondoa moja kwa moja sumu inayotoka kwenye maji hayo yanayoanzia kwenye dampo hilo.”

 

Mtambo wa kuchuja sumu iliyomo kwenye maji yanayotiririka kutoka kwenye dampo la mtaa wa Kanisani

HALI ILIVYO SASA

Mhandishi Kassambili ameweka wazi kuwa baada ya ujio wa mradi huo, serikali iliweza kuelewa kuwa dampo hilo lisilo rasmi lilikuwa likisababisha madhara na kuamua kusitisha shughuli zote za umwagaji wa taka kwenye eneo hilo. 

 

“Kwa sasa hakuna harufu kali kama awali na pia hakuna inzi wala funza, wananchi walikuwa wanaishi na wadudu hao hatari kwa afya zao na ilifikia hatua ili wananchi waweze kula ni lazima waingie kwenye vyandarau bila kujali ni mchana au usiku.”

 

Mafanikio mengine ni ni kukamilika kwa mtambo wa kupunguza sumu ya maji hayo na kilichobaki sasa ni kuangalia ufanisi na kiwango ambacho mtambo huo unaweza  ukatibu maji hayo ili kupunguza au kuondoa kabisa sumu inayopatikana kwenye maji hayo yanayoingia kwenye mto Kizinga.

 

“Kuna mabadiliko makubwa baada ya ujio wa mradi huo kwa sababu sasa nyasi ambazo zilikuwa zikiungua, zimeanza kuota na madhara yaliyokuwa yakiwapata wananchi hasa kwa kuungua ngozi na kupata fungusi yamepungua.

 

“Pia WWF inafanya tathmini za kitaalamu, ambapo wamechukua sampuli na kupeleka maabara ili kuweza kujua ufanisi wa mtambo huo.”

 


WITO KWA JAMII

Mhandisi Kassambili amewaomba wananchi kuelimishana wao kwa wao juu ya kutotupa takataka pembezoni mwa vyanzo vya maji na kwamba kuharibu vyanzo hivyo kuna athari kubwa kwao kiafya na kiuchumi na sio kama wanaikomoa serikali.

 

“Wanapaswa kujua wanapochafua vyanzo vya maji wanajiongezea mzigo wao wenyewe kwa sababu serikali italazimika kuyatibu maji hayo kwa gharama na gharama hiyo inafidiwa na wananchi wenyewe kupitia ankara za maji.

 

“Aidha ni vema taasisi, mashirika na wadau wengine kushirikiana na serikali kujitokeza katika kushiriki kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kujitangaza kibishara  na kusaidia kushiriki kwenye uhifadhi kwa kushirikiana na WWF ni shirika linalofanya kazi kwa uadilifu kwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinakuwa endelevu na thamani ya pesa inafanya kile kilichokusudiwa kama ilivyofanya ABinBev kupitia TBL kwa kuufadhili mradi huu.”   

 

Bi. Aneth Stanslaus akitoa ushuhuda wa faida za mradi huo mbele ya Wanahabari.

WANANCHI WATOA USHUHUDA

Bi. Aneth Stanslaus ambae ni mkazi wa Kilungule anasema yeye ni mmoja wa watu waliokuwa wakiathiriwa na maji hayo yenye sumu yanayotoka kwenye dampo la Kanisani.

 

Bi. Anaeth anasema awali haikuwa rahisi kwao kuwa na ngozi yenye nuru, kukosa vikohozi na kupata fangasi huku mazao yao yakiwa hayastawi hata wamwagie maji siku nzima.

 

“Haya maji ni hatari, yaani ngozi zetu na watoto wetu zilikuwa ni mbaya, afya zetu zilikuwa dhaifu kila siku, fungusi za miguu na mikono ndio zilikuwa haziishi, lakini baada ya ujio wa mradi huu, angalau sasa tuna nafuu kubwa, hakuna harufu mbaya, mimea imeanza kustawi na ngozi zetu zimeanza kupata nusu.”

 

Kauli ya Bi. Aneth imeungwa mkono na Marwa Joseph Mwita, ambae awali alikuwa anafikiria kuuza nyumba yake ili akatafute sehemu nyengine ambayo itakuwa na usalama kwake na kwa familia yake.

BODI  YA MAJI BONDE LA WAMI RUVU YAAHIDI KUUENDELEZA MRADI
Mtaalamu wa maji kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu, Aidan Kaaya aliwashukuru wadau hao kwa mradi huo ambao umekuwa na tija kubwa kwa jamii na kwamba wao wako tayari kuuendeleza hata pale muda wa ufadhili wa mradi utakapokwisha.

 

Kaaya amesema Bodi imeshiriki kikamilifu kwenye hatua zote za mradi huo na kwamba wao ndio walikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mto Kizinga unalindwa kwa sababu una umuhimu mkubwa kwa mkoa wa Dar es Salaam na nchi kwa ujumla.

 

Pamoja na mambo mengine Kaaya amewataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa mto huo kuacha kuchafua na kuharibi vyanzo vya maji kwa maslahi yao, kwani kitendo cha kuviharibu kitawagharimu kwa kiasi kikubwa.


 


 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments