Ticker

7/recent/ticker-posts

DIPLOMASIA YA SAMIA YATUA URUSI, KUFUNGUA FURSA MPYA KWA WATANZANIA

NA. FATMA JALALA

Ziara ya kimkakati inayochora upya nafasi ya Tanzania katika diplomasia ya uchumi wa dunia

Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Shirikisho la Urusi, imeibua mjadala mpana kuhusu mwelekeo mpya wa diplomasia ya uchumi na nafasi ya Tanzania katika mfumo unaobadilika wa mahusiano ya kimataifa. Safari hii ya kitaifa, iliyofanyika kwa mwaliko wa Rais Vladimir Putin, inatazamwa kama hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya mataifa haya mawili yenye historia ndefu ya mahusiano ya kirafiki.


Katika kauli yake kabla ya kuondoka nchini, Rais Samia alibainisha kuwa ziara hiyo si ya kawaida, bali ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, ambayo inatoa nafasi kubwa kwa sekta binafsi na ushirikiano wa kimataifa unaolenga maendeleo ya wananchi. 


Alisisitiza kuwa mazungumzo na viongozi wa Urusi yamelenga kufungua milango ya ushirikiano katika sekta za msingi zinazogusa maisha ya Watanzania.

Pia alieleza dhamira ya Tanzania kushiriki majukwaa ya biashara na uwekezaji ili kutangaza fursa zilizopo nchini, sambamba na kupanua masoko ya bidhaa za Kitanzania ndani ya Urusi na maeneo mengine ya ushawishi wa kiuchumi.

Ushirikiano wa kiuchumi unaoanza kupata kasi

Katika siku ya kwanza ya mazungumzo rasmi Moscow, Rais Samia na mwenyeji wake Rais Vladimir Putin walijadili mustakabali wa uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili. Pande zote zilipongeza ongezeko la biashara lililofikia asilimia 72 kati ya mwaka 2020 na 2025, ishara ya uhusiano unaokua kwa kasi licha ya changamoto za kimataifa.


Hata hivyo, viongozi hao walikubaliana kuwa bado kuna nafasi kubwa zaidi ya kupanua ushirikiano huo ili kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi. Mkazo uliwekwa katika sekta za sayansi na teknolojia, elimu, nishati, madini, kilimo, miundombinu na utalii—sekta ambazo zinaweza kuharakisha mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.


Sauti ya Samia na dira ya ushirikiano
Akizungumza akiwa Moscow, Rais Samia alieleza kuwa ziara hiyo ina umuhimu wa kihistoria kwa Tanzania, akibainisha kuwa imepita zaidi ya nusu karne tangu ziara ya mwisho ya kiserikali kufanyika nchini Urusi tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.


Alieleza shukrani kwa mwaliko huo na kuikumbusha dunia mchango wa Urusi katika harakati za ukombozi wa Tanzania, akisisitiza kuwa uhusiano huo una mizizi ya kihistoria inayopaswa kuendelezwa kwa maslahi ya maendeleo ya sasa na ya baadaye.


Mtazamo wa Urusi kuhusu Tanzania
Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin alieleza kuridhishwa na kasi ya maendeleo ya Tanzania na kusema Urusi imekuwa ikifuatilia kwa karibu mageuzi yanayoendelea nchini. Alisisitiza kuwa mazungumzo yake na Rais Samia yamekuwa yenye tija kubwa, na kuahidi kuimarisha zaidi ushirikiano katika sekta za maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.


Nafasi ya Tanzania katika dunia inayobadilika

Ziara hii inaweka picha pana ya Tanzania katika mazingira ya kimataifa. Kwa upande wa taifa, inaashiria nchi yenye utulivu wa kisiasa, sera huru za mambo ya nje na uwezo wa kushirikiana na mataifa makubwa bila kuegemea upande mmoja. Kwa Afrika, inatuma ujumbe kuwa bara hilo linazidi kuwa mshirika hai katika maamuzi ya maendeleo ya dunia, si mpokeaji tu wa maelekezo ya nje.


Katika ngazi ya kimataifa, ziara hii inaakisi mabadiliko ya mfumo wa dunia kuelekea ushirikiano wa mataifa mengi yenye ushawishi (multipolar world), ambapo nchi kama Tanzania zinapata nafasi ya kujenga mahusiano ya kimkakati na washirika mbalimbali kwa maslahi ya maendeleo yao.


Fursa zinazoweza kuibuka kwa Watanzania
Iwapo makubaliano yanayojadiliwa yatatekelezwa kikamilifu, Tanzania inaweza kunufaika kwa namna mbalimbali. Hii ni pamoja na ongezeko la uwekezaji na ajira, upanuzi wa biashara kati ya Tanzania na Urusi, fursa zaidi za elimu na mafunzo kwa vijana, uhamishaji wa teknolojia ya kisasa, ongezeko la utalii na mapato ya fedha za kigeni, pamoja na kuimarika kwa nafasi ya Tanzania katika diplomasia ya kimataifa.


Pia, ushirikiano huo unaweza kufungua vyanzo vipya vya maendeleo kupitia miradi ya pamoja ya kiuchumi na kisayansi, ambayo inaweza kuharakisha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi nchini.


Kwa mtazamo wa kitaalamu, ziara ya Rais Samia nchini Urusi ni zaidi ya tukio la kidiplomasia. Ni jaribio la kimkakati la kuipanua nafasi ya Tanzania katika uchumi wa dunia na kuunganisha diplomasia na maendeleo ya wananchi.

Hata hivyo, katika kila hatua muhimu ya diplomasia ya taifa, ni kawaida kuwepo kwa mitazamo tofauti kuhusu mwelekeo na manufaa ya ziara za viongozi wa kitaifa. Wanaotilia shaka umuhimu wa ziara ya Rais Samia nchini Urusi wana haki ya kutoa maoni yao, kwani mjadala wa sera ni sehemu ya ujenzi wa demokrasia. Hata hivyo, tathmini ya ziara za aina hii inapaswa kuzingatia maslahi mapana ya taifa na mabadiliko ya mazingira ya kimataifa kuliko hisia za kisiasa za muda mfupi. 


Katika dunia ya sasa, maendeleo yanachochewa na uwezo wa nchi kujenga ushirikiano na washirika mbalimbali, kuvutia uwekezaji, kupata teknolojia na kufungua masoko mapya. Kwa msingi huo, thamani ya ziara hii haitapimwa kwa mahali ilikofanyika wala kwa majina ya viongozi waliokutana, bali kwa matokeo yatakayozalishwa kwa uchumi wa taifa na ustawi wa Watanzania katika miaka ijayo.

Aidha, kipimo halisi cha mafanikio yake hakitakuwa kwenye hotuba au picha za mikutano ya viongozi, bali katika matokeo halisi yatakayoonekana katika maisha ya Watanzania ikiwemo ajira mpya, biashara zilizoimarika, teknolojia mpya na ongezeko la ustawi wa jamii.

Ndipo historia itakapotoa jibu la mwisho; je, ziara hii ilikuwa safari ya kawaida ya kidiplomasia au mwanzo wa sura mpya ya maendeleo ya Tanzania katika karne ya ishirini na moja.





Post a Comment

0 Comments