NA MWANDISHI WETU- AFRINEWSSWAHILI-TANGA
Bahari inayounganisha pwani ya Tanga na visiwa vya Pemba imekuwa zaidi ya eneo la maji yanayokutana na upeo wa macho.Imekuwa chanzo cha maisha, matumaini na ustawi kwa maelfu ya wananchi wanaotegemea uvuvi, kilimo cha mwani na shughuli nyingine zinazounda msingi wa Uchumi wa Bluu katika ukanda huo.
Kila alfajiri, wavuvi huingia baharini wakitafuta riziki, huku wakulima wa mwani wakitumia maarifa ya kizazi hadi kizazi kuvuna fursa zilizojificha ndani ya maji ya Bahari ya Hindi.
Lakini nyuma ya neema hiyo, kulikuwa na changamoto zilizokuwa zikitishia mustakabali wa rasilimali hizo na maisha ya wananchi wanaozitegemea.
Uharibifu wa mazingira ya bahari, uvuvi haramu, ukataji wa mikoko na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za baharini vilikuwa vikiongezeka kwa kasi.
Athari zake zilianza kuonekana katika kupungua kwa baadhi ya viumbe wa baharini, kuharibika kwa mazalia ya samaki na kuzorota kwa mifumo muhimu ya ikolojia inayolinda ukanda wa pwani.
Kadiri changamoto hizo zilivyozidi kuongezeka, ndivyo ilivyodhihirika wazi kuwa hakuna taasisi, jamii au eneo ambalo lingeweza kukabiliana nazo peke yake.
Ilikuwa ni wakati wa kuunganisha nguvu, maarifa na uzoefu kwa lengo moja la kulinda bahari na kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika nayo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Ndipo lilipozaliwa Jukwaa la Tanga-Pemba SeaCAP, ambalo leo linaonekana kuwa daraja muhimu linalounganisha Tanzania Bara na Zanzibar katika juhudi za kuhifadhi rasilimali za bahari sambamba na kukuza maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.
MAARIFA YANAYOVUKA BAHARI
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa LMMA Pemba, Shehani Amani, kuanzishwa kwa jukwaa hilo kumefungua ukurasa mpya kwa wavuvi, wakulima wa mwani na wajasiriamali wa pande zote mbili.
Anasema kabla ya kuanzishwa kwa SeaCAP, Tanga na Pemba zilikuwa zikitekeleza shughuli zao kwa kujitegemea bila kuwa na mfumo madhubuti wa kubadilishana uzoefu au kujifunza kutoka kwa wenzao.
“Awali kila upande ulikuwa unafanya kazi kivyake. Wakulima wa mwani wa Pemba walikuwa na uzoefu wao, huku Tanga ikiwa na uzoefu katika maeneo mengine ya uhifadhi.
Lakini baada ya kuanzishwa kwa Tanga-Pemba SeaCAP, tumepata nafasi ya kubadilishana maarifa na kujifunza kutoka kwa kila mmoja,” anasema.
Kupitia ushirikiano huo, wananchi wa Pemba wamejifunza mbinu za upandaji wa mikoko na uhifadhi wa nyasi bahari kutoka Tanga.
Wakati huohuo, wananchi wa Tanga wamepata maarifa kuhusu kilimo cha mwani, ufugaji wa majongoo bahari na ufugaji wa chaza kutoka kwa wenzao wa Pemba.
Matokeo yake yamekuwa makubwa. Mbinu hizo zimeongeza uwezo wa wananchi kutumia rasilimali zilizopo kwa njia endelevu huku zikiongeza thamani ya shughuli zao za kiuchumi.
“Leo tunaona wananchi wengi wakijihusisha na shughuli za kiuchumi ambazo hapo awali hazikuwa maarufu katika maeneo yao. Hii ni faida kubwa kwa sababu inapanua vyanzo vya mapato kwa jamii,” anasema Shehani.
VIKUNDI VYA UJASILIAMARI VYABADILI MAISHA
Athari chanya za SeaCAP hazijaishia kwenye uhifadhi pekee. Jukwaa hilo pia limekuwa kichocheo cha kuibuka kwa vikundi mbalimbali vya ujasiriamali vinavyowapa wananchi fursa ya kujiongezea kipato kupitia shughuli zinazohusiana na rasilimali za bahari.
Kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, ikiwemo Shirika la IUCN, vikundi hivyo vimekuwa vikiwasaidia wananchi kuanzisha miradi ya kiuchumi inayowawezesha kujitegemea na kuboresha maisha yao.
“Watu wanapata kipato, wanasomesha watoto wao, wanajenga nyumba na kuboresha maisha yao kwa ujumla. Haya ni matokeo ya moja kwa moja ya uwekezaji katika uhifadhi na Uchumi wa Bluu,” anasema Shehani.
Kwa upande wake, Sophia Waziri kutoka Wilaya ya Pangani mkoani Tanga anasema manufaa ya ushirikiano huo yanaonekana wazi katika maisha ya wananchi wa ukanda wa pwani.
Anasema kwa muda mrefu wananchi wa Tanga hawakuwa na uzoefu mkubwa katika kilimo cha mwani.
Hata hivyo, kupitia mafunzo na ushirikiano na wenzao wa Pemba, sasa wameanza kutambua fursa zilizopo katika sekta hiyo.
“Kilimo cha mwani ni moja ya shughuli zinazoongeza kipato kwa haraka. Kupitia ushirikiano huu, watu wa Tanga wameanza kuona umuhimu wake na wamepata maarifa ya namna ya kulifanya kwa tija,” anasema.
Kwa mujibu wake, ushirikiano huo umeimarisha pia mshikamano kati ya jamii za Tanga na Pemba katika kulinda rasilimali za bahari ambazo zinawanufaisha wote.
UHIFADHI NA UCHUMI NDANI YA KAPU MOJA
Mwenyekiti Mwenza wa Jukwaa la Tanga-Pemba SeaCAP, Denis Mpotwa, anasema jukwaa hilo lilianzishwa mwaka 2022 baada ya kutambuliwa kuwa ukanda wa Tanga na Pemba una utajiri mkubwa wa rasilimali za bahari zinazohitaji usimamizi wa pamoja.
Katika ukanda huo kunapatikana matumbawe, mikoko, nyasi bahari, viumbe adimu wa baharini na vivutio mbalimbali vya utalii vinavyoweza kuchangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya uchumi wa taifa.
“Lengo letu ni kuhakikisha wadau wote wanakutana na kujadili kwa pamoja namna ya kuhifadhi rasilimali hizi huku tukihakikisha jamii zinanufaika nazo kiuchumi,” anasema.
Kwa mujibu wa Mpotwa, mafanikio ya jukwaa hilo yanatokana na kuunganisha matokeo ya tafiti za kisayansi na maarifa ya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kwa muda mrefu.
Anasisitiza kuwa hakuna Uchumi wa Bluu unaoweza kustawi bila kuwepo kwa uhifadhi wa rasilimali za bahari.
“Tunapozungumzia Uchumi wa Bluu lazima tuzungumzie uhifadhi. Bahari ikiharibiwa, samaki wakitoweka na mikoko ikikatwa hovyo, hakuna uchumi utakaobaki ndiyo maana tunahakikisha shughuli za kiuchumi zinaendana na uhifadhi,” anasema.
MAFANIKIO YANAYOVUKA MIPAKA
Mafanikio ya Tanga-Pemba SeaCAP yameanza kuvutia maeneo mengine nchini. Kwa mujibu wa Mpotwa, uzoefu uliopatikana kupitia jukwaa hilo tayari umechangia kuanzishwa kwa jukwaa kama hilo katika Mkoa wa Mtwara, huku mipango ikiendelea katika maeneo mengine ya ukanda wa pwani.
Aidha, wadau wa jukwaa wamepata fursa ya kutembelea nchi mbalimbali na kujifunza mifumo ya kimataifa ya usimamizi wa rasilimali za bahari na ufadhili wa shughuli za uhifadhi.
“Tumeshuhudia nchi ambazo jamii zake zinanufaika moja kwa moja na uhifadhi kupitia mapato ya utalii na mifumo ya kifedha inayosaidia kuhifadhi mazingira.
Tunataka kujifunza na kutumia mifano hiyo hapa nchini,” anasema.
SERIKALI YATAMBUA UMUHIMU WA USHIRIKIANO
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uvuvi, Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi, Christian Mnzowa, anasema kuanzishwa kwa jukwaa hilo kulitokana na kuongezeka kwa changamoto za mazingira ya bahari katika ukanda wa Tanga na Pemba.
Anataja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uharibifu wa matumbawe, ukataji wa mikoko, uvuvi wa baruti na matumizi ya zana haramu zinazoharibu mazalia ya samaki pamoja na nyasi bahari.
“Awali kila taasisi ilikuwa ikifanya kazi peke yake. Lakini baadaye tukagundua kuwa changamoto hizi haziwezi kutatuliwa na taasisi moja. Ilibidi kuunganisha nguvu za Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na wadau wengine wa maendeleo,” anasema.
Anabainisha kuwa ushirikiano huo umezikutanisha wizara, taasisi za uhifadhi, halmashauri, mashirika ya kiraia na jamii za wavuvi katika juhudi za kuhakikisha rasilimali za bahari zinatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa sasa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Bluu Zanzibar zinaendelea kuimarisha jukwaa hilo kwa matumaini kwamba litakuwa chombo muhimu katika kusimamia rasilimali za bahari na kukuza Uchumi wa Bluu nchini.
BAHARI YA MATUMAINI
Kwa wananchi wa Tanga na Pemba, Tanga-Pemba SeaCAP si jukwaa la kawaida. Ni daraja la maarifa, ushirikiano na matumaini mapya.
Ni mfano unaoonyesha kwamba uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi vinaweza kwenda sambamba ikiwa jamii, serikali na wadau wataunganisha nguvu zao.
Katika mawimbi yanayounganisha Tanga na Pemba, sasa si samaki na boti pekee zinazovuka. Yanavuka pia maarifa, uzoefu na maono ya pamoja ya kujenga maisha bora kupitia matumizi endelevu ya bahari ambayo kwa miongo mingi imeendelea kuwa uti wa mgongo wa maisha ya wananchi wa ukanda huo.
0 Comments