Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo, amesisitiza umuhimu wa asasi za kiraia katika kukabiliana na kuenea kwa jangwa na uharibifu wa ardhi, akieleza kuwa ushiriki wao ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Taifa na kimataifa ya uhifadhi wa mazingira.
Chikomo alitoa kauli hiyo kwenye Warsha ya Kitaifa ya Maandalizi ya Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa (UNCCD COP17), iliyofanyika Juni 30, 2026, jijini Dodoma.
Katika wasilisho lake lililobeba dhima ya Asasi za kiraia katika kukabiliana na jangwa Tanzania,"The Role of Civil Society Organizations (CSOs) in Combating Desertification in Tanzania" alisisiza zaidi ushirikiano wa pamoja.
Warsha hiyo iliandaliwa chini ya Mradi wa Kilimo Endelevu Arusha (KEA) unaotekelezwa na MVIWAARUSHA, CARI na RECODA kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).
Lengo lake lilikuwa kuwaandaa wadau wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika mkutano wa UNCCD COP17 utakaofanyika Ulaanbaatar, Mongolia, kuanzia Agosti 17 hadi 28, 2026.
Akiwasilisha mada yake, Chikomo alieleza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na JET katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira kupitia uandishi wa habari na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya mazingira.
Pia alifafanua nafasi ya JET katika kuwakilisha wadau wa Tanzania kwenye mkutano wa UNCCD COP17 na katika juhudi nyingine za kimataifa za kukabiliana na uharibifu wa ardhi.
Alisema asasi za kiraia zina nafasi kubwa katika kukabiliana na changamoto za mazingira kupitia utoaji wa elimu kwa umma, kusaidia utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira, kujenga uwezo wa jamii, pamoja na kutetea sera na sheria zinazolinda mifumo ikolojia iliyo hatarini na kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za asili.
Aidha, alieleza kuwa asasi hizo zinaendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Kuenea kwa Jangwa (National Action Programme - NAP) unaotekelezwa kwa kuzingatia Mkataba wa UNCCD, kwa lengo la kufikia Land Degradation Neutrality (LDN) ifikapo mwaka 2030.
Warsha hiyo ilitoa fursa kwa washiriki kubadilishana taarifa kuhusu Mkataba wa UNCCD na matokeo ya mkutano wa Désertif’actions 2026, kujengeana uwezo kuhusu mchakato wa mazungumzo ya UNCCD, kuimarisha ushirikiano katika usimamizi endelevu wa ardhi, kilimo hai, urejeshaji wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuandaa mapendekezo ya Tanzania yatakayowasilishwa katika mkutano wa COP17.
Warsha hiyo ilifunguliwa rasmi na mwakilishi wa UNCCD National Focal Point kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais – Kitengo cha Mazingira (VPO-DoE), Abdallah Lungo, ambaye alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, asasi za kiraia na wadau wengine katika kulinda mazingira na kuhakikisha matumizi endelevu ya ardhi nchini.
0 Comments