Ticker

7/recent/ticker-posts

TAMWA YAANZISHA MRADI WA UFUGAJI NYUKI KUINUA WANAWAKE KIUCHUMI

 

Dkt. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji-TAMWA

NA SIDI MGUMIA, DAR ES SALAAM

Chama cha Wanawake Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) kimezindua mradi wa ufugaji nyuki katika Kijiji cha Msufini, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, ukiwa na malengo mawili makuu: kuinua kipato cha wananchi hasa wanawake na vijana na kulinda mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

 Mradi huu unatekelezwa katika shamba lenye ukubwa wa hekari 94, ambalo limepimwa na kufanyiwa utafiti na Wizara ya Kilimo ili kubaini mazao yanayoweza kustawi. Umefadhiliwa na Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) na unatekelezwa kwa ushirikiano na wakazi wa Msufini.

Florance Majani, Afisa Uchechemuzi na Masuala ya Sera-TAMWA (kulia) akifafanua jambo wakati wa mafunzo. Katikati ni Christina Samwe, Afisa Nyuki wa Halmashuri ya Kibaha na kushoto ni Fatma Underson, Afisa Nyuki Mkowa wa Pwani  

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa wanachama wa chama hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben, alisema mradi huu utawapa wanawake na vijana fursa ya kujipatia kipato endelevu kupitia shughuli rafiki kwa mazingira. 

“Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa TAMWA (2021–2025) unaolenga uwezeshaji wanawake na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Hatua ya awali inajumuisha uwekaji wa mizinga 200 ya nyuki,” alisema Dk. Rose.

Kwa upande wake, Afisa Uchechemuzi na Masuala ya Sera wa TAMWA, Florence Majani, alieleza kuwa ufugaji nyuki ni chanzo cha kipato kinachohitaji gharama ndogo, hakiharibu mazingira, na hutoa mazao yenye thamani kubwa kama asali na nta, yenye soko la ndani na nje ya nchi.

Christina Samwe ambaye ni Afisa Nyuki kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha

Afisa Nyuki wa Wilaya ya Kibaha, Christina Samwe, alibainisha kuwa mazao ya nyuki yakiwemo asali, masega, gundi ya nyuki, maziwa ya nyuki na chavua hutumika kama chakula, dawa na bidhaa za biashara. Aliongeza kuwa kilo moja ya asali huuzwa kwa wastani wa shilingi 10,000 nchini na pia husafirishwa kwenda India, Oman na Uturuki. Hata hivyo, alitoa tahadhari kwamba uvunaji usiozingatia ubora unaweza kushusha thamani ya bidhaa. 

Washiriki wa mafunzo

Naye Afisa Nyuki wa Mkoa wa Pwani, Fatma Underson, alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na wataalamu ili kuhakikisha ubora wa uzalishaji. Alitoa mfano wa Wilaya ya Rufiji, ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa asali bora kutokana na mazingira yake asilia yasiyo na kemikali. 

Christina Samwe, Afisa Nyuki akiongea na washiriki wa mafunzo

Mradi huu unatarajiwa kuanza rasmi Agosti 2025 baada ya kukamilika kwa mafunzo na usambazaji wa mizinga na vifaa. Lengo kuu ni kuwafanya wanawake wa Msufini kuwa mfano wa kuigwa katika matumizi bora ya rasilimali asilia kwa maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira kwa vizazi vijavyo.


Post a Comment

0 Comments