![]() |
| Meneja
Mipango wa TAMWA, Silvia Daulinge |
NA SIDI MGUMIA, DAR
ES SALAAM
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwa
kushirikiana na taasisi ya Well Spring, kimeendesha mafunzo maalum kwa
waandishi wa habari kuhusu namna bora ya kuripoti masuala ya haki ya afya ya
uzazi kwenye vyombo vya habari. Lengo kuu ni kuongeza uelewa wa jamii, kupaza
sauti za wanawake na wasichana, na kuhakikisha masuala haya yanapewa nafasi ya
kutosha kwenye mijadala ya kitaifa.
Mafunzo hayo, yaliyofanyika katika ofisi za TAMWA, Sinza, Dar es Salaam, yalihudhuriwa na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Umuhimu wa Mradi
Meneja Mipango wa TAMWA, Silvia Daulinge, alisema mradi huu unalenga kuhuisha huduma za habari kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na ustawi wa afya ya uzazi.
“Tunataka kuongeza mijadala ya kina kwenye vyombo vya habari
kuhusu haki ya afya ya uzazi, ili jamii ipate taarifa sahihi na kwa wingi.
Masuala haya yamepewa kipaumbele kidogo, hivyo tunataka kuamsha uandishi wa
habari zenye uchambuzi na zinazochochea mabadiliko,” alisema.
Daulinge aliongeza kuwa mradi huo pia unachangia utekelezaji
wa Lengo la Maendeleo Endelevu Namba 3, linalohusu afya na ustawi wa watu,
hususan wanawake na wasichana wadogo.
![]() |
| Dkt. Syriacus Buguzi, Kiongozi Mwandamizi wa Utafiti kutoka Utafiti Forum akifafanua jambo kwa washiriki wa mafunzo |
Wito kwa Waandishi wa Habari
Dkt. Syriacus Buguzi, Kiongozi Mwandamizi wa Utafiti kutoka Utafiti Forum, alisisitiza umuhimu wa waandishi kuzingatia maadili na kuepuka upotoshaji wa taarifa, iwe kwa makusudi au bila kukusudia.
“Tusiandike habari zinazoweza kupotosha jamii. Badala yake,
tuandike kwa mpangilio mzuri, tukitumia vyanzo sahihi ili kuongeza uelewa wa
wananchi kuhusu elimu ya afya ya uzazi,” alisema.
![]() |
| Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben |
Sheria na Kanuni Muhimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, alieleza
kuwa waandishi wanapaswa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo wanaporipoti
masuala ya afya ya uzazi.
“Kwa kuandika habari zikielezea sheria na miongozo husika,
tunaweza kusaidia jamii kujua haki zao na pia kupunguza changamoto kama mimba
za utotoni, ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia,” alisema.
Alisisitiza kuwa uandishi wa habari ukitumia msingi wa
kisheria unaweza kusaidia hata kuibua sheria mpya au marekebisho ya sera ili
kuendana na matakwa ya kitaifa na kimataifa.
![]() |
| Neema Kasaburilo, Afisa Jinsia na Habari-TAMWA |
Changamoto
Zinazoathiri Haki ya Afya ya Uzazi
Kwa mujibu wa Neema Kasaburilo, Afisa Jinsia na Habari
kutoka TAMWA, utafiti wa awali wa mradi ulibaini changamoto kadhaa, ikiwemo:
Upotoshaji wa taarifa kupitia mitandao ya kijamii kwa vijana
kutokana na kukosa mwongozo kutoka kwa wazazi.
Upungufu wa huduma vijijini na umbali wa vituo vya huduma,
hali inayoongeza hatari ya ukatili kwa watoto.
Uwakilishi mdogo wa vijana kwenye mchakato wa maamuzi ya
sera za afya ya uzazi.
Mimba za utotoni kutokana na kuanza mahusiano ya mapenzi
wakiwa na umri mdogo.
Ukatili wa kijinsia unaofanywa na watu wa karibu wa familia
na kushindwa kuripoti kutokana na hofu au ukosefu wa uaminifu na wazazi.
Uendelezaji wa ukeketaji, ikiwemo katika baadhi ya maeneo ya
mijini kama Kipunguni, Dar es Salaam, jambo linalokosa ufuatiliaji na uripoti
wa kutosha.
![]() |
| Mafunzo yakiendelea |
Hitimisho
Kupitia mafunzo haya, TAMWA na Well Spring wanatarajia
kuandaa kizazi cha waandishi wa habari watakaoripoti masuala ya haki ya afya ya
uzazi kwa weledi, uadilifu na uchambuzi wa kina. Lengo ni kuhakikisha kwamba
sauti za wanawake na wasichana zinasikika na changamoto zinazowakabili
zinapatiwa ufumbuzi kupitia uhamasishaji wa kitaifa.





0 Comments