Ticker

7/recent/ticker-posts

MALAWI, MSUMBUJI NA TANZANIA WASHIRIKIANA KULINDA IKOLOJIA YA BONDE LA MTO RUVUMA


NA JIMMY KIANGO

Nchi za Malawi, Msumbiji na Tanzania zimeamua kushirikiana kulinda mifumo ya ikolojia na kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Katika kufanikisha zoezi hilo kiasi cha takribani dola za Marekani milioni 7.12 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi bilioni 18.3 kinatarajia kutumika katika kulinda mifumo ya ikolojia katika katika nchi hizo tatu zilizopitiwa na bonde la Mto Ruvuma.


Mradi huo unaojulikana kama GEF Ruvuma, umelenga Kuimarisha usimamizi shirikishi wa mpakani wa mfumo wa chanzo hadi bahari wa Bonde la Mto Ruvuma na maeneo yake ya pwani ili kuhakikisha afya ya mifumo ya ikolojia na usalama wa maisha ya wananchi. 


Akiuzungumzia mradi huo ambao pia utasaidia maisha endelevu na jumuishi ya wananchi, Afisa Mradi huo kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Maliasili Tanzania (IUCN-Tanzania),Bi. Ng’walu Kidayi amesema mradi huo ni wa kikanda ambao unatekelezwa katika nchi zinazopitiwa na bonde hilo ambazo ni Malawi, Msumbiji, na Tanzania.


Bi. Kidayi amesema kuwa mradi huo una thamani ya takribani dola za Marekani milioni 7.12 na unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 60 kutoka mwaka huu wa 2026 hadi Desemba 2030.

Aliwataja wafadhili wa mradi huo kuwa ni Global Environment Facility (GEF) na unaongozwa na IUCN kama wakala wa utekelezaji wa GEF, kwa kushirikiana na Global Water Partnership Southern Africa (GWPSA) na Wetlands International Eastern Africa (WIEA) ambazo ni taasisi zinazotekeleza mradi huo.


“Lengo la mradi ni kulinda uadilifu wa mifumo ya ikolojia huku ukiimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kusaidia maisha endelevu na jumuishi ya wananchi katika nchi zote tatu zinazopitiwa na bonde la Ruvuma.


“Taasisi za kikanda na za kitaifa katika nchi hizo tatu zina nafasi muhimu katika utekelezaji wa mradi, huku mifumo ya uratibu wa pamoja wa mpakani ikitumika kama kitovu cha usimamizi na ushirikiano wa bonde,”amesema.

SHUGHULI ZA MRADI WA GEF

Mradi wa GEF utatekeleza shughuli mbalimbali ili kuimarisha upangaji na usimamizi shirikishi wa ardhi, maji safi, mifumo ya pwani na bahari kwa kutumia mfumo wa chanzo hadi bahari (source-to-sea approach).


Shughuli hizi zimepangwa katika vipengele vitano vikuu vya mradi ambavyo ni Kuimarisha mifumo ya taasisi kwa ajili ya usimamizi wa bonde na maeneo ya pwani katika mipaka ya nchi na Kuwezesha usimamizi wa bonde na maeneo ya pwani kupitia maamuzi yanayotegemea ushahidi wa kisayansi.


Shughuli nyengine ni Kusaidia upangaji wa kimkakati wa uwekezaji na uhamasishaji wa rasilimali kwa ajili ya usimamizi jumuishi wa bonde na pwani,Kukuza usimamizi endelevu wa ardhi na maji kwa njia ya ushirikishwaji wa jamii na wadau na Usimamizi wa mradi, uzalishaji wa maarifa, mawasiliano na usambazaji wa taarifa.


Kwa pamoja, vipengele hivyo vinalenga kuimarisha ushirikiano wa nchi katika usimamizi wa maji ya mipakani, kulinda mifumo muhimu ya ikolojia kutoka milimani hadi baharini na kuleta manufaa ya kijamii, kimazingira na kiuchumi kwa jamii za Bonde la Ruvuma.

UTEKELEZAJI WA AWALI

Katika kuhakikisha mradi huo unaleta tija kusudiwa kwa jamii iliyopakana na bonde hilo, watendaji wa mradi huo walianza utekelezaji wa awali kwa kuandaa warsha ya uzinduzi yenye lengo la kuweka msingi rasmi wa kuanza utekelezaji wa mradi.


Lengo kuu likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu malengo ya mradi, kuhakikisha nchi wanachama na wadau wanajihusisha kikamilifu na kuumiliki mradi na kwamba warsha hiyo iliyofamnyika kwa siku mbili Machi 4-5,2026 jijini Dar es Salaam imetumika kutambulisha mradi na kueleza matokeo yanayotarajiwa.


Shughuli zilizotekelezwa kwenye warsha hiyo ni pamoja na kufafanua majukumu ya wadau wakuu, kuweka uwiano wa kazi kati ya timu za mradi na washirika pamoja na kutoa jukwaa la kuthibitisha dhamira ya ushirikiano, kuhamasisha majadiliano na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa mradi huo.

 

Pamoja na mambo mengine warsha hiyo imetumika kuwatambulisha wadau wakuu kuhusu lengo la mradi, malengo mahususi, matokeo, vipengele na bidhaa za mradi.


Aidha imetumika kufafanua na kuoanisha majukumu ya wadau katika utekelezaji wa mradi, mifumo ya kufanya maamuzi, mifumo ya utoaji taarifa, mawasiliano na utatuzi wa migogoro.


Pia imeongeza uelewa wa wadau kuhusu mifumo ya uwajibikaji ya GEF na IUCN ikiwemo usimamizi wa fedha, ufuatiliaji, tathmini na ujifunzaji, usimamizi wa mazingira na jamii na usimamizi wa hatari.


Warsha hiyo imetoa uelewa na kupokea maoni kuhusu Mpango wa Ushirikishwaji wa Wadau, Utekelezaji wa Masuala ya Jinsia, Ufuatiliaji na Mfumo wa Ufuatiliaji wa Ufadhili Shirikishi.


MATOKEO CHANYA

Warsha ya uzinduzi imesaidia kuongezeka kwa uelewa wa wadau na umiliki wa mradi, usimamizi wa fedha, ufuatiliaji na tathmini ya GEF na IUCN na kuujua mpango kazi wa miaka kadhaa na bajeti ulioboreshwa.

 

Post a Comment

0 Comments