Ticker

7/recent/ticker-posts

TANZANIA YAWEKA KIPAUMBELE KUDHIBITI MMOMONYOKO WA UDONGO NA VIMBUNGA

Miundombinu ya barabara, makazi, na biashara zilizozama kutokana na mafuriko yaliyoikumba manispaa ya Kigoma Ujiji mwaka 2023/2025.

NA. ADELA MADYANE-KIGOMA

Tanzania imeandaa miradi mitatu ya kimkakati itakayowania fursa ya kupata fedha za kukabiliana na hasara na uharibifu kupitia Mfuko wa Hasara na Uharibifu (FRLD).

Hatua hiyo ni matokeo ya maazimio yaliopitishwa katika Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), uliomalizika Novemba 21,2025 jijini Belem, nchini Brazili.


Mkutano huo ulitoa fursa kwa nchi zinazoendelea ambazo zimeathirika na mabadiliko ya tabia nchi kuanza kutuma maombi ya ufadhili ili kufidia hasara hizo.


Mfuko wa FRLD uliozinduliwa mwaka 2022 katika mkutano wa COP27 nchini Misri, umezindua rasmi wito wake wa kwanza wa maombi ya ufadhili ambapo nchi zitakuwa na miezi sita ya kuwasilisha mapendekezo ya miradi kuanzia katikati ya Desemba 2025 hadi Juni 2026 huku ufadhili ukitarajiwa kuanza kutolewa Julai 2026.


Kiasi cha kwanza kilichotengwa kwa mwaka 2026-2027 ni dola milioni 250 kwa ajili ya nchi zote zenye sifa huku nchi nyingi za Afrika zina sifa ya kuomba fedha hizo.


MIRADI MITATU MUHIMU

Akizungumza na AFRINEWS SWAHILI Afisa Mkuu wa Mazingira na Mratibu wa Taifa wa Uhimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi Dkt. James Nyarobi, ameitaja miradi ambayo wanaamini itapata ufadhili kuwa ni wa kukabiliana na maporomoko ya ardhi na udongo hasa katika maeneo ya Hanang, Mbeya na Kagera pamoja na maeneo mengine yaliyokumbwa na kadhia hiyo.


Eneo la piili ni kwenye kukabiliana na mafuriko ya mara kwa mara na maeneo ya visiwa yanayoathiriwa na vimbunga kufuatia mabadiliko ya tabia nchi.Amesema  kuwa vipo vimbunga vinavyotokea hapa nchini na kuacha madhara makuwa kwa wananchi akitoa mfano wa kimbunga Hidaya kilichosababisha athari katika maeneo ya visiwa na pwani ambapo uharibifu ulitokea.


Eneo la tatu kukabiliana na mmomonyoko wa fukwe ambao unachangiwa na kuongezeka kwa kina cha maji cha bahari na mmomonyoko wa udongo unaosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha katika maeneo ya nchi kavu na kusababisha mmomonyoko katika mazingira ya pwani.


“Tunatambua hasara inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi ipo kwenye maeneo mengi nchini ikiwa ni pamoja na mkoa wa Kigoma na maeneo mengine, dirisha linapofunguliwa linakuwa na fedha kiasi, hatuwezi kuweka changamoto za nchi nzima kwa kiwango kidogo cha fedha kilichotengwa, ni muhimu kuwa na vipaumbele kuwa tutaanza na kipi na kipi kitafuata, na maeneo mengine yatatafutiwa kwa kadiri rasilimali fedha itakavyopatikana na kadiri fursa zitakavyojitokeza.”

Eneo la msitu lililogeuka eneo la mashamba ya watu baada ya kukatwa miti katika eneo la Kanembwa wilayani Kibondo.
TANZANIA ILISHAJIANDAA

Dkt. Nyarobi amesema hata kabla ya kushiriki katika mkutano wa COP30, Tanzania ilikuwa imeshajiandaa kwa kubainisha miradi ya kimkakati kwa ajili ya kuomba ufadhili kutoka kwa wafadhili wengine. 


“Tunajua kwenye mikutano ya COP ndio sehemu pekee ya kukutana na wadau wote, kwa hiyo tuliandaa maandiko mapema kabisa, tulipokwenda kwenye mkutano wa COP30 tuliwapatie wadau ambao wanaweza kutusaidia fedha au kuwekeza katika nchi yetu, lakini pia tuliandaa maandiko na kuyachambua yanayofaa kutafutiwa fedha za hasara na uharibifu na yale yanayoweza kuelekezwa katika mifuko mengine”, amesema Nyarobi


Ameeleza kuwa Mfuko umeweka utaratibu wa kushindaniwa kwa namna ya kupelekea maandiiko ya miradi itakayoshawishi upatikanaji wa fedha kwa nchi husika akifafanua kuwa maandiko hayo yanapaswa kuwa na ushahidi wa kutosha unaoonesha hasara na uharibifu ambapo thamani ya kila mradi ni kati ya dola milioni tano hadi dola milioni 20.


MAOMBI YA FEDHA YAMETAWANYWA 

Dkt. Nyarobi anabainisha kuwa maombi ya fedha za kukabiliana na mabadiliko Tabia nchi, hayajaishia kwenye mfuko wa FRLD pekee, bali pia wamepeleka kwenye mfuko wa “Green Climatic Fund” (GCF), “Global Environment Facility” (GEF), “Adaptation Fund” pamoja na mifuko mingine ambayo huweza kufidia hasara na uharifu.


“Ipo miradi mbalimbali ambayo serikali imefanikiwa kupata fedha kutoka vyanzo mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi ambao umeanza kutekelezwa mkoa wa Kigoma hivi karibuni ambao umepata fedha kutoka mfuko wa GCF, na huo mradi unatekelezwa katika wilaya tatu za Kasulu, Kibondo na Kakonko na ipo miradi zaidi ya 15 kwa upande wa bara na 10 kwa upande wa Zanzibar, inayotekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini kupitia vyombo vya ndani”, anafafanua zaidi.


JITIHADA ZINAHITAJIKA

Katika kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo, jitihada na mikakati madhubuti inahitajika kwani kiwango cha kwanza cha fedha kilichotengwa kwa nchi zote zenye sifa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ya hasara na uharibifu ya zaidi ya Dola bilioni 400 kwa mwaka na hivyo viongozi wanapaswa kupanga vipaumbele kwa umakini ili kuanza na kile kinachohitajika zaidi.


Ili kunufaika na fursa hii, Mwenyekiti wa Kikundi cha Majadiliano cha Afrika (AGN),Dkt. Richard Muyungi, , amesisitiza kuwa katika kuchukua hatua za kimkakati kunapaswa kuwa na “Focal Person” wa kitaifa ili kuratibu maombi ya ufadhili na kuhakikisha miradi inawasilishwa kwa wakati,kuandaa mpango wa kitaifa wa miradi ya dharura utakaobainisha maeneo ya kipaumbele na mikakati ya utekelezaji.


Vilevile amehimiza kuepuka urasimu ili kuhakikisha fedha zinawafikia wananchi walioko mstari wa mbele katika kukabiliana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko  tabianchi sambamba na viongozi kuhakikisha wanawajibika kuhakikisha kuna uwazi na ushirikishwaji wa jamii katika utoaji wa fedha.


Katika mkutano wa kilele, Mwenyekiti Mwenza wa FRLD, Jean-Christophe Donnellier, alisema wito huu wa awali wa ufadhili utasaidia kujifunza na kuunda mfumo wa muda mrefu wa mfuko huo. 

Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2020 kuhusu Hasara na Uharibifu unaosababishwa na  Mabadiliko Tabianchi 


Tanzania inapoteza takribani dola milioni 200 kila mwaka kutokana na athari kama ukame, mafuriko, na mmomonyoko wa ardhi huku sekta ya kilimo ikipata pigo zaidi, ikifuatiwa na makazi ya watu na miundombinu ya barabara.


Evans Njewa, Mwenyekiti wa Kundi la nchi zenye Maendeleo Duni (LDCs), alipongeza uzinduzi huo akisema ni lazima mfuko utoe msaada wa haraka, rahisi na unaofikika kwa jamii zilizo katika mstari wa mbele wa athari za hali ya hewa.

Njewa anataja umuhimu wa fedha za L&D kuwa zitashughulikia athari ambazo zimepita uwezo wa nchi zinazoendelea kujikinga (Adaptation) nazo ambapo kwa Tanzania fedha hizi hujumuisha uharibifu wa miundombinu, kupotea kwa urithi wa kitamaduni na kuhamishwa kwa jamii au watu kutoka makazi yao.


WANANCHI WATAKA VIONGOZI KUWAJIBIKA

Kufuatia ufafanuzi huo baadhi ya wananchi wa mkoa wa Kigoma wamewataka viongozi kuwajibika ili kuhakikisha fedha zinaptaikana na elimu inaendelea kutolewa ili kuzuia uharibifu zaidi.


Geofrey Kalimanzira, kutoka Makere, anasema uharibifu uliopo hasa katika eneo la misitu ni mkubwa jambo ambalo limesababisha kuwe na mvua zisizo eleweka pamoja na kusababisha ukame katika vyanzo vingi vya maji jambo ambalo linaleta madhara  kwa wananchi.


“Wilaya ya Kasulu ilikuwa sehemu pekee yenye misitu minene na vyanzo vingi vya maji kwa mkoa wa Kigoma, lakini hivi tunavyozungumza misitu imeisha, msitu wa Makare Kusini umeisha, msitu wa Malagarasi umeisha, umevamiwa na wananchi wanaohama hapa na pale kutafuta malisho ya mifugo yao, mingine imekatwa na wakimbizi wakitafuta kuni za kupikia, wengine wakitafuta mashamba yenye rutuba, serikali ifanye jambo kunusuru maisha yetu”, anasema Kalimanzira


Tafiti za serikali na mashirika zinazohusika na uhifadhi wa mazingira zinaonesha kuwa kila mwaka hekta 470,000 za misitu hukatwa na kusababisha uharibifu wa mazingira na kupungua kwa rasilimali za kiikolojia.


Fikirini Zuberi yeye anataja kuwa pamoja na nchi kuandaa miradi bora, anaiomba iendelee kupita katika kila maeneo yaliyoathirika kwa kushirikiana na wananchi ili kuweza kujua uharibifu zaidi unaotokea hasa maeneo ya vijijini ambapo wengi wa wananchi hawajui kama kinachotokea ni mabadiliko ya tabianchi badala yake wakimini katika ushirikina na kwamba huenda Mungu anaachilia ghadhabu kutokana na dhambi.

 

 



Post a Comment

0 Comments