Ticker

7/recent/ticker-posts

MTAMBO WA KUCHUJA SUMU YA MAJI TAKA, RAFIKI WA MAZINGIRA TEMEKE

Mtambo maalum wa kuchuja sumu ya maji taka.
NA. JIMMY KIANGO

Harufu kali ya taka zilizooza, magonjwa ya ngozi, vikohozi visivyokwisha, maisha ya  kupishana na funza, minyoo na inzi wakubwa wa  kijani yamebaki historia kwenye eneo la Kanisani -Barabara ya Mwinyi Buza  Kwalulenge, Temeke, mkoani Dar es Salaam.

Wakazi wa maeneo hayo sasa wanaweza kukaa nje na kula chakula bila bughudha ya inzi wa kijani na funza waliokuwa wakizaliana kila siku kutoka kwenye dampo lisilo rasmi lililopo eneo hilo.

 

Ngozi za miguu na mikono ya watoto na wazazi wao wengi zilikuwa zimepauka, kuchanika na kukakaamaa kama vipande vya mihogo iliyoanikwa juani.

 

Ngozi zilikosa nuru hata kama zingepakwa kopo zima la mafuta ya mgando. Hakuna kilichofaa kuzinawirisha ngozi za wakazi wengi wa eneo la  bondeni kwa Lulenge.

 

Ardhi ya eneo kubwa yanakotiririka maji machafu yenye sumu ilikuwa imebeba mateso makubwa ya kutorutubisha chochote.

 

Hakuna kilichostawi, nyasi na majani ya asili yalikauka kama yamemwagiwa tindikali, mimea ya kupandwa ndio kabisa, haikuwa ikitoa shukurani kwa madebe ya maji yaliyokuwa yakimiminwa ili iiote na kumea.

 

Kimsingi hali ilikuwa ni mbaya, halikuwa jambo la  ajabu kwa mbegu za mchicha zilizomwagwa tutani, zikimbishia mkulima kuchipua. Hakuna kilichomea wala kunawiri.

HATIMAE MKOMBOZI AMEPATIKANA

Kila lenye mwanzo halikosi mwisho, hivyo ndivyo anavyosema mwanamama Aneth Stanslaus mkazi wa eneo hilo.

 

Baada ya mateso ya muda mrefu, hatimae Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF-Tanzania) kwa kushirikiana na taasisi ya AbinBev ya Afrika Kusini ambayo inamiliki Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) iwamekuja na Mradi wa Usalama wa Maji Dar es Salaam (DWS).

 

Taasisi hizi kwa kushirikiana na serikali ndio  mashujaa wa mazingira na afya za wakazi wa Buza kwa Lulenge.

 

Mradi huo unahusisha maeneo ya uwanda wa chini wa mto Ruvu(Lower Ruvu), Mto Kizinga na Mto Msimbazi,umefufua matumaini ya maisha kwa wakazi wa eneo hilo na kizuri zaidi  umeonesha namna ya kujenga upya uhusiano kati ya uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii kwa kubadili mifumo wa ikolojia iliyoharibika kuwa suluhisho linalookoa maisha. 

 

Faraja hiyo imeletwa na ujenzi wa mtambo maalum wa kuchuja sumu inayotoka kwenye maji taka yanayotiririka kutoka kwenye chemchem zinazoanzia kwenye dampo hilo.

 

Mtambo huo umebeba mbinu za asili zinazoweza kukabiliana na changamoto za dharura za mijini, huku zikiboresha afya ya umma na kurejesha matumaini kwa jamii zilizo hatarini.

MABADILIKO NDANI YA TEMEKE

Katika Wilaya ya Temeke, hususan Kata ya Buza, mradi huo umeleta mabadiliko ya kweli kupitia ukarabati wa vyanzo vya maji na ujenzi wa mtambo maalum unaosaidia kuchakata maji yenye sumu kuwa maji salama.

 

Pembezoni ya Mto Kizinga, wastani wa mita  300 kutoka kwenye mto huo kuna mtambo unaoonekana kama bwawa la kufuga samaki.

 

Maji yaliyomo ndani ya bwawa hilo lililozungushiwa wavu ni hatari kuliko sumu ya panya, ndani yake hakuna kiumbe hai kinachothubutu kuishi, mashida ya miti ya mianzi iliyochomekwa ili kuiotesha, yamegoma kuota na badala yake yamekauka kama vipande vya mifupa ya ngombe iliyokaushwa.

 

Mratibu wa maji kutoka WWF, Mhandisi Christian Chonya anasema vipande hivyo vya miti ya mianzi wamevipandikizwa ili kuona kama vinaweza kuota na kuwa sehemu ya kunyonya sumu hiyo kwa njia ya asili.

 

Kimsingi utekelezaji wa mradi huo umetokana na  kasi ya ukuaji wa miji na usimamizi duni wa taka ulikuwa umeisukuma jamii katika mgogoro wa muda mrefu wa kiafya na kimazingira.

 

CHEMCHEM ZILIZOKUWA BARAKA, ZILIGEUKA KUWA LAANA

Mhandisi Chonya anasema kwa miaka mingi, wakazi walitegemea chemchemi za asili kando ya Mto Kizinga kwa mahitaji yao ya kila siku ya maji. 

 

Hata hivyo, utupaji holela wa taka uliibadili taratibu chemchemi hizo zilizokuwa baraka zikawa laana, utirirshaji wa maji safi ukatoweka na kuwa chanzo cha maji machafu na hatarishi kwa afya za binadamu.

 

Utupaji wa taka ulizilazimisha familia zilizo karibu na eneo hilo kujikuta wakiishi na maji  machafu, Watoto walikuwa katika hatari kubwa zaidi, walicheza karibu na maji machafu, walihatarisha afya zao.

 

SULUHISHO ENDELEVU

Katika kukabiliana na hali hiyo iliyoendelea kuwa mbaya, mradi huo umeonekana kuwa ni suluhisho bunifu na endelevu.

 

Kupitia michakato shirikishi, mfumo huu husafisha maji machafu kwa njia ya asili, kuboresha ubora wa maji na kurejesha uwiano wa ikolojia bila kutumia miundombinu ghali inayohitaji nishati nyingi.

 

Mradi ulitekelezwa chini ya Mpango wa Maji Safi wa WWF Tanzania, ukiongozwa na Mratibu wa Maji, Mhandisi Chonya, ambaye ushauri wake wa kitaalamu ulihakikisha suluhisho linazingatia mahitaji ya mazingira na jamii.

 

“Mradi wa Usalama wa Maji Dar es Salaam ni kuhusu kuhakikisha uhai kwa watu na mazingira. Temeke, hususan eneo la Buza kando ya Mto Kizinga, tulikuta chanzo cha maji ambacho hakikuwa kinafanya kazi kabisa. Chemchemi ya asili iliyokuwa ikiihudumia jamii ilikuwa imegeuka kuwa eneo chafu na hatarishi kutokana na uharibifu wa juu ya mto, utupaji taka na shughuli holela za binadamu,” alisema.

 

WATOTO WALIATHIRIKA ZAIDI

Alieleza kuwa watoto ndio walikuwa waathirika wakubwa kwani walikuwa wakicheza kwenye maji yaliyochafuliwa, familia zilizo karibu na mitiririko ya maji hayo zilikuwa kwenye hatari kubwa za kiafya. 

 

“Hali hii ilihitaji suluhisho la haraka. Ndiyo maana, kwa kushirikiana na wadau wetu, tuliamua kutumia suluhisho linalotegemea asili kwa kujenga Ardhi Oevu Bandia.

“Ardhi oevu hii inafanya kazi kama kichujio cha asili cha maji. Inaboresha ubora wa maji, inaongeza upatikanaji wa maji na kurejesha mifumo ikolojia huku ikilinda jamii. 

 

“Muhimu zaidi, inapunguza hatari za kiafya na kuunda mazingira salama kwa wakazi, hususan wanawake na watoto,” aliongeza.

 

Alisisitiza kuwa, “Lengo letu si kuboresha tu usalama wa maji Dar es Salaam bali pia kuonesha kwamba uhifadhi wa mazingira unaweza kuokoa maisha moja kwa moja. Tunapolinda vyanzo vya maji, tunalinda jamii. Mradi huu unathibitisha kuwa suluhisho endelevu zinawezekana pale wadau wanaposhirikiana kwa ajili ya watu na mazingira.”

 

WITO KWA JAMII

Mhandisi Chonya amewaomba wananchi kuelimishana wao kwa wao juu ya kutotupa takataka pembezoni mwa vyanzo vya maji na kwamba kuharibu vyanzo hivyo kuna athari kubwa kwao kiafya na kiuchumi na sio kama wanaikomoa serikali.

 

“Wanapaswa kujua wanapochafua vyanzo vya maji wanajiongezea mzigo wao wenyewe kwa sababu serikali italazimika kuyatibu maji hayo kwa gharama na gharama hiyo inafidiwa na wananchi wenyewe kupitia ankara za maji.

 

“Aidha ni vema taasisi, mashirika na wadau wengine kushirikiana na serikali kujitokeza katika kushiriki kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kujitangaza kibishara  na kusaidia kushiriki kwenye uhifadhi kwa kushirikiana na WWF ni shirika linalofanya kazi kwa uadilifu kwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinakuwa endelevu na thamani ya pesa inafanya kile kilichokusudiwa kama ilivyofanya ABinBev kupitia TBL kwa kuufadhili mradi huu.”   

 

Post a Comment

0 Comments