Ticker

7/recent/ticker-posts

VIJANA WENGI KINONDONI HAWAIJUI FURSA ILIYOPO KWENYE UNUNUZI WA UMMA


 

NA. JIMMY KIANGO

Katika muktadha wa ukuzaji uchumi na ajira nchini Tanzania, serikali imeweka mikakati kadhaa ya kuhakikisha makundi yaliyokandamizwa kiuchumi, ikiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, wanapata fursa ya kushiriki zaidi katika shughuli za uchumi wa Taifa. 

 

Moja ya mikakati hiyo ni eneo la Ununuzi wa umma ambao kwa mujibu wa Sheria kumewekwa sharti la asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi ya umma kutengwa kwa makundi maalum. 

 

Lengo kuu ni kuwapa wanachama wa makundi haya fursa ya kupata zabuni, kukuza biashara ndogo ndogo na hivyo kupunguza ukosefu wa ajira.

 

Hata hivyo, licha ya sera hiyo kuwepo kwa muda sasa, vijana wengi wa Kinondoni hawana uelewa wa kutosha juu ya fursa hii, jambo linalosababisha kutowasilisha maombi ya zabuni, kushindwa kufikia vigezo vinavyohitajika na hatimaye kushindwa kunufaika na fursa hizo.

 

ASILIMIA 30 UHAI WA UCHUMI KWA MAKUNDI MAALUM

Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 inatumika kama mkondo mkuu wa taratibu za ununuzi wa bidhaa, huduma na ujenzi kwa taasisi za serikali. 

 

Kwa mujibu wa sheria iliyopo na kanuni zake, sheria hii inasisitiza kwamba taasisi za umma zitengeneze fursa maalum kwa makundi yaliyoainishwa. 

 

Kifungu cha 64 (1-2c) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma kinahitaji kwamba, taasisi zote za ununuzi wa umma zitenge angalau asilimia 30 ya thamani ya ununuzi wao kwa mwaka kwa makundi maalum, ikiwa ni pamoja na vijana, watu wenye ulemavu, wanawake na wazee. 

 

Aidha, Kanuni ya 30C ya Kanuni za Ununuzi wa Umma inafafanua jinsi sehemu hiyo ya asilimia 30 inavyotakiwa kutekelezwa na taasisi za umma. 

 

Makundi maalum lazima yaandikishwe na kuthibitishwa kama makundi maalum kwenye Mfumo wa Kitaifa wa Manunuzi (NeST) kabla ya kupata fursa hizi. 

 

MWONGOZO WA PPRA 

Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeandaa mwongozo wa namna ya kushiriki kwa makundi maalum katika ununuzi wa umma ili kusaidia taasisi za umma na wanachama wa makundi hayo, kuelewa taratibu na vigezo vya utekelezaji wa asilimia 30. 

 

Kwa mujibu wa kanuni na mwongozo wa utekelezaji, Vijana wanapaswa kupata asilimia 10 ya zabuni zilizotengwa, Watu wenye ulemavu wanapaswa kupata asilimia 10, Wanawake wanapaswa kupata asilimia 5 na Wazee wanapaswa kupata asilimia 5.

Kwa muhtasari, taasisi za umma zinatakiwa kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi wa umma kwa mwaka kwa makundi maalum, na sehemu hii lazima iwe wazi na kutolewa kwa makundi husika kupitia zabuni zilizotangazwa kwa uwazi. 

 

CHANGAMOTO YA UELEWA

Pamoja na sheria, Kanuni na Miongozo kuwa wazi, ukweli ni kwamba kuna changamoto ya uelewa miongoni mwa vijana wa wilaya ya Kinondoni.

 

Vijana wengi wa Kinondoni wanakosa taarifa sahihi na uelewa wa fursa hii: 

Amina Bakari (25), mjasiriamali wa huduma za mtandao anasema: Sikujua kabisa kuwa serikali ilitenga asilimia 10 ya zabuni kwa ajili ya vijana kama mimi. Nilidhani ni ajira ya kawaida tu, tungetegemea, si fursa hii ya manunuzi ya umma.”

 

Juma Mhina mkazi wa Tegeta, Kinondoni -Dar es Salaam,(28), ambaye ni mfanyabiashara mdogo wa Saruji anasema:

“Nilipojaribu kutafuta taarifa juu ya manunuzi ya umma, sikuelewa taratibu za kujiandikisha kwenye mfumo wa NeST. Hatukupewa mafunzo na hakuna mtu aliyeelekeza kikamilifu tunafanyaje.”

 

Neema Zebedayo(24), mfanyabiashara wa chakula maarufu kama Mama lishe anaeleza kuwa: Tumeambiwa juu ya asilimia 30, lakini hatujui sehemu gani ya malengo hayo yanatuhusisha sisi. Sote tunasikia tu kuhusu ajira, si namna ya kupata zabuni serikalini.”

 

John Ngulaye mfanyabiashara wa kusafirisha vifusi na mchanga kutoka machimbo ya Wazo (27), anasema pamoja na kuwa na elimu ya Stashahada ya biashara, hakuwahi kusikia chochote juu ya kuwepo kwa fedha zilizotengwa rasmi kwa ajili ya vijana kutoka kwenye manunuzi ya umma. 

 

Bakari Mohamed fundi ujenzi yeye anasema:

Nilisikia kuna sheria ya kutoa asilimia 30 kwa makundi maalum, lakini nataka kujua jinsi ya kuunda kikundi, jinsi ya kupata cheti na jinsi ya kuomba zabuni hizo, hatujapata mafunzo.”

 

Naye Zainab Magabala (23), muuza mazao ya kilimo hakusita kuweka wazi kuwa:

“Tunahitaji mafunzo ya vitendo kuhusu namna ya kushiriki katika zabuni hizi; siyo tu taarifa fupi kutoka kwenye vyombo vya habari, bali mafunzo ya jinsi ya kujiandikisha na kushindana kikamilifu.”

 

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyakasangwe, Bi.Zuhura Mabewa.


VIONGOZI NGAZI YA MTAA NA KATA

Kwa upande wa viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Mtaa na Kata wamekuwa na maoni mseto, ambapo wapo wanaoijua fursa hiyo, huku baadhi yao wakiwa hawajui chochote kuhusu asilimia 30 iliyopo kwenye Sheria ya Manunuzi ya Umma.

 

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyakasangwe, Kata ya Wazo wilayani Kinondoni, Zuhura Mabewa, aliiambia Afrinews kuwa suala hilo ni jipya kwake, hajui lolote na tangu aingie madarakani mwaka 2024, hajawahi kushirikishwa kwenye manunuzi ya miradi inayofanyika kwenye Mtaa wake.

 

“Niwe mkweli, sijui chochote juu ya sheria hii, nikushukuru wewe kwa kuja kuniambia, nadhani sasa itakuwa ni jukumu langu kuhakikisha vijana na hayo makundi maalum yaliyopo kwenye eneo langu wanafaidika na fursa hiyo,” amesema.

 

Kuhusu uwepo wa vikundi kwenye mtaa wake, Bi. Mabewa amesema, vikundi vipo, hata hivyo, vingi havijarasimishwa hadi kufikia hatua ya kutambuliwa na kuwezeshwa kushiriki kwenye miradi ya umma. Lakini ameahidi kuhakikisha anakutana na vijana, hasa wa bodaboda, ili kuwapa taarifa za fursa hiyo.

 

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Wazo, Mante Ntonja alisema anaijua hiyo fursa na kwamba ofisi yake kwa kushirikiana na ofisi ya Maendeleo ya Jamii Kata, wamekuwa wepesi kuyasaidia makundi maalum kupata mikopo ya asilimia 10 ili kukuza mitaji yao na hatimaye kufanikiwa kuingia kwenye fursa zilizopo kwenye manunuzi ya umma. 

 

Diwania Kata ya Wazo, Bi. Grace Mkumbwa.

Diwani wa Kata ya Wazo, Grace Mkumbwa amesema hana uelewa wa kutosha wa fursa hiyo iliyopo kwenye ununuzi wa umma, lakini tangu aingie madarakani mwaka 2025, amekuwa akihakikisha anashirikiana na vijana na makundi mengine ili kukuza vipato vyao.

 

“Sina uelewa wa kutosha na hilo suala la fursa iliyopo kwenye manunuzi ya umma, lakini najua kuna ile mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, nimekuwa nikihakikisha vijana na makundi mengine wanaichangamkia fursa hii. Hata hivyo, baada ya kupata taarifa hii, sasa nitakuwa na nyongeza ya fursa ambayo nitaitumia kuwapa vijana na makundi mengine.”

 

Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Vumilia Tigwela.

AFISA MANUNUZI KMC ATOA NENO

Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Vumilia Tigwela amekiri kukosekana kwa uelewa wa fursa iliyopo kwenye ununuzi wa umma.

 

“Kulingana na tathmini mbalimbali, sababu kuu za ukosefu wa uelewa miongoni mwa vijana ni kutopewa elimu na uelewa wa taratibu za manunuzi ya umma.

 

“Kutokuwepo kwa mafunzo maalum kwa vijana na makundi maalum, upungufu wa kampeni za kuelimisha kwa ngazi ya jamii na changamoto za kiufundi kwenye mfumo wa NeST,” amesema.

 

Bi. Vumilia amesema kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 KMC ilifanya manunuzi ya bilioni 50 kwenye miradi zaidi ya 300 na katika kiasi hicho cha fedha ni wastani wa shilingi bilioni mbili pekee ndio zimeyafikia makundi maalum.

 

Anasema pamoja na kukosekana kwa uelewa juu ya fursa hiyo, lakini pia vijana wengi hawana mitaji na hawajui namna ya kufanikisha kupata mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri.

 

“Binafsi yangu natamani vijana na makundi yote yanufaike na fursa hii iliyopo kwenye manunuzi, lakini shida iliyopo ni sheria kuweka taratibu ngumu kidogo zinazowezesha vijana kuungana hasa kwa maeneo ya mijini, lakini pia naona kuna haja ya kuwa na utendaji wa moja kwa moja kati ya Ofisi ya Ununuzi Wilaya na ofisi ya Maendeleo ya Jamii, ili kurahisha mchakato wa kuwawezesha vijana na makundi mengine.”

 

Ameongeza kuwa, ili suala hilo liwe endelevu kwa makundi yote hasa vijana, ni vema elimu ya fursa hiyo ikatolewa vyuoni kuanzia mwaka wa kwanza, hatua ambayo itawaondolea vijana fikra za kuajiriwa na kufikiria kujiajiri kwa kufanya kazi na serikali kupitia Ununuzi wa Umma.

 

Mwandishi wa makala haya, Jimmy Kiango (kulia) akifanya mahojiano na Bi. Vumilia (kushoto)

PPRA YAZIOMBA HALMASHAURI KUTOA ELIMU

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kupitia kwa Meneja wa Kanda ya Pwani, Bi. Vicky Mollel amekiri kuwepo kwa udhaifu wa utoaji wa elimu kwa jamii na kwamba wao wanafuatilia utolewaji wa elimu ya mfumo wa NeST kupitia Halmashauri zote.

 

“Sisi wenyewe PPRA tunatoa elimu kwenye Halmashauri mbalimbali, kwa kupitia Wakurugenzi na tunafuatilia kwa kuhudhuria semina hizo, ambazo Halmashauri zinawaalika wafanyabiashara na wajasiriamali wa eneo husika kuja kuhudhuria mafunzo hayo.


Bi. Vicky amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo kunahitajika elimu ya kutosha na uhamasishaji zaidi katika maeneo yote, na kwamba Halmashauri zote zinapaswa kutoa elimu kwa kuzingatia fursa ya asilimia 30 kwa makundi maalum hususani.

 

“Halmashauri zinapaswa kuibua vikundi na kuvisajili baada ya kutoa elimu. Wanapotoa elimu ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi, watoe pia elimu ya fursa mbalimbali ikiwemo ya mfumo wa NeST

 

“Vijana wanatakiwa waelimishwe zaidi kuwa, wanaposajili vikundi, waangalie ni biashara gani wanaweza wakafanya na serikali. Waangalie katika taasisi za serikali kuna uhitaji gani au ni vitu/huduma gani serikali inanunua kutoka kwa wananchi, ili nao waweze kujisajili kwa kusudi la kupata fursa za zabuni kupitia ununuzi wa umma. 

 

“Ikiwa kikundi cha vijana kimejisajili katika biashara ambayo serikali hainunui hususani kwa kupitia mfumo, lazima fursa hiyo itawapita.”amesema.

 

“Tunashirikiana na NGO’s, na Tanzania Chamber of Commerce katika utoaji wa elimu ya mfumo wa NeST na taratibu zake zikiwemo sheria. Mfano Desemba 19, 2025 tulitoa mafunzo hayo, ikiwemo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Hata ukiangalia katika mitandao yetu ya kijamii, ingia Instagram, Youtube utaona,

 

“Pia Januari 10, 2026 tulitoa elimu Katika mikoa minne ya Mbeya, Tabora, Mwanza na Dar es Salaam. 

 

CHANGAMOTO ZILIZOPO

Bi. Vicky amesema miongoni mwa changamoto zilizopo ni kukosekana kwa muitikio na mahudhurio hafifu: Muitikio wakati mwingine unakuwa mdogo, wanaotakiwa kupata elimu hiyo hawahudhurii.

 

Changamoto nyengine ni kukosekana kwa ufuatiliaji, ambapo wahusika hawafuatilii na hata baadhi ya wanaopata elimu hiyo pia, hawafuatilii fursa hizo wala kuyachukulia mafunzo hayo kuwa ni fursa kwao. Wengi wao wanaweka dhana potofu kuwa, kufanya kazi na serikali ni shida.

 

USHAURI WA VIJANA KWA SERIKALI

Idadi kubwa ya vijana waliozungumza na mtandao huu, wameiomba Serikali na mamlaka husika kuongeza elimu na uhamasishaji, ili fursa ya asilimia 30 ya makundi maalum iweze kutumiwa kikamilifu na vijana wa Kinondoni na maeneo mengine.

 

Kwamba Serikali kupitia PPRA, NEEC na mamlaka za mikoa na wilaya, ziweke mikakati ya kutoa mafunzo ya vitendo kwa vijana juu ya ununuzi wa umma.

 

Viongozi wa maendeleo ya jamii, walimu na wahudumu wa maeneo ya huduma kwa umma wanapaswa kuwa walimu wa jamii kuhusu namna ya kushiriki kwenye zabuni.

 

Watendaji waliopewa dhamana wawe tayari kusaidia uandikishaji wa vikundi na ushauri wa biashara,

kuwasaidia vijana kuunda vikundi vya kibiashara vinavyokidhi vigezo vya sheria kwa kupata hati za makundi maalum.

 

Kutoa ushauri wa biashara na mipango ya kitaalamu juu ya uandishi wa zabuni na utekelezaji wa miradi, ufuatiliaji na uwajibikaji wa Taasisi za Umma. Lakini pia kuimarisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria ya asilimia 30, ili kuhakikisha taasisi za umma zinatekeleza kikamilifu agizo la kisheria.

 

Na zaidi, kutoa ripoti za uwazi juu ya jinsi asilimia 30 inavyotumika na jinsi makundi yanayofaidika na fursa hiyo.

 

ASILIMIA 30 NI FURSA YA AJIRA

Bi. Vumilia anasema sheria ya ununuzi wa umma inayotaka taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalum ni fursa kubwa kwa vijana wa Kinondoni na Tanzania kwa ujumla kujiajiri. 

 

Hata hivyo, changamoto ya ukosefu wa uelewa na ufahamu wa taratibu inazuia vijana wengi kushiriki kikamilifu katika fursa hii. 

 

Kupitia elimu, mafunzo, msaada wa kiufundi na uwajibikaji bora, fursa hii inaweza kugeuka kuwa njia thabiti ya kuwajengea vijana ujuzi na kukuza biashara zao.

Post a Comment

0 Comments