NA JIMMY KIANGO
.
Kwa miongo mingi, uvuvi wa Tanzania umebaki kuwa wa jadi licha ya mchango wake mkubwa katika ajira, usalama wa chakula na pato la taifa.
Takribani asilimia 95 ya uzalishaji wa samaki nchini unatokana na wavuvi wadogo, wanaotumia mitumbwi ya mbao, nyavu za kawaida na teknolojia duni.
Ndani ya mazingira haya, huibuka uharibifu na uchafuzi wa mazingira ya bahari kutokana na baadhi ya wavuvi kutumia dhana haramu za uvuvi ambazo zinaiteketeza bahari.
Kwa kulitambua hilo na katika kuhakikisha bahari inakuwa salama na wavuvi wanakuza vipato vyao na Uchumi wa Buluu unakuwa na tija ya kweli kwa jamii ya Pwani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imepanga kutoa mikopo nafuu isiyo na riba kwa wavuvi.
Uamuzi huo ni mwendelezo wa Serikali ya Tanzania ya kutaka kuitumia bahari kuwa moja ya vyanzo vikuu vya kukuza uchumi kwa wavuvi kupitia Uchumi wa Buluu.
Aidha hatua hiyo inatajwa kama dhamira ya Tanzania ya kutaka kutekeleza maazimio yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC COP30), uliofanyika Belém, Brazil mwaka 2025 ya kulinda mazingira ya bahari.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena, Mikopo hiyo itakayotolewa mwaka huu haitakuwa ya fedha bali ni mikopo ya boti za Fiber za uvuvi.
Hiyo itakuwa ni awamu ya tatu huku lengo likiwa ni kuendelea kuwawezesha wavuvi kufanya uvuvi wa kibiashara, utakaowasaidia kukua kiuchumi.
Boti zitakazotolewa ni za urefu wa kuanzia mita 5-14 na injini zake zikiwa na nguvu ya farasi (HP) kwa mpangilio wa injini ya 9.9HP kwa boti yenye urefu wa mita tano, boti ya mita nane na 10 itakuwa na injini ya 15HP na Mita 12 na 14 zitakuwa na injini yenye uwezo wa 60HP.
Mbali na uwezo mkubwa wa injini, lakini pia zitakuwa na uwezo wa kubeba kati ya wavuvi sita hadi 20 na uwezo wa kubeba tani mbili za samaki.
Ili kuhakikisha wavuvi wanavua kisasa, boti hizo zitakuwa na kifaa maalum cha kuongoza safari (GPS) vifaa vya uokozi, kifaa cha kuzima moto, boti mbili saidizi kwa boti za mita 12 na 14 pamoja na nyavu na vifaa vyake.
Ili kufanikisha upatikanaji wa urahisi wa mikopo hiyo, Wizara imeelekeza wanaotaka kujua zaidi namna ya kuomba na vigezo vya kina kufika kwa Wakurugenzi wa Halmashauri husika kupitia Afisa Uvuvi au ofisi za Kanda za Sekta ya Uvuvi www.mifugouvuvi.go.tz.
Aidha Wizara imetoa wito kwa wananchi waliotayari kukopa kuwasilisha maombi yao Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika na kwamba maombi hayo yanapaswa kuwasilishwa kabla ya Januari 16,2026 kupitia anuani ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Bi. Agness amesema hatua hiyo inatokana na dhamira ya serikali ya kutaka kulinda mazingira ya Bahari kwa kuwaondoa wavuvi kwenye kuvua kwa kutumia dhana duni na wengine kutumia mabomu na baruti hali inayochangia kuiangamiza bahari.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena
WAVUVI WAFURAHIA
Chande Ally ambae ni mvuvi na mfanyabiashara wa samaki katika soko la kimataifa la Feri, anasema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda mazingira ya bahari na kuwaongezea kipato pia.
“Uvuvi wa kutumia boti ndogo za asili hautupi fursa ya kukuza vipato vyetu, ujio wa mikopo hiyo ya maboti ya uvuvi ya kisasa utasaidia kuongeza kipato na kuilinda bahari,”amesema Chande.
Nae Mussa Mtoka ambae pia ni mvuvi pamoja na kupongeza, lakini ameitaka serikali kutoweka mashariti magumu katika kufanikisha utoaji wa mikopo hiyo ya boti za uvuvi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wavuvi Pwani ya Kunduchi, Zedi Mwinyi Zedi ameipongeza serikali kwa uamuzi huo na kusema wazi kuwa utasaidia kuboresha maisha ya wavuvi watakaofanikiwa kukopesheka.
BOTI ZA KISASA ZITALINDA BAHARI
Afisa Utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Baraka Sekadende amesema kuwa uamuzi wa serikali kuwakopesha wavuvi wadogo boti za kisasa zenye injini, vifaa vya usalama na teknolojia za utafutaji wa samaki ni hatua ya kimkakati inayolenga kubadilisha uso wa sekta ya uvuvi na kuilinda bahari.
Hatua hii inajengwa juu ya misingi ya Sera ya Taifa ya Uvuvi (2015), Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya 2003, pamoja na mkakati mpana wa kukuza uchumi wa buluu na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na maji ya ndani.
Sehemu ya Boti za kisasa za uvuvi zinazotolewa kwa wavuvi wadogo kwa mkopo.
FAIDA KWA MVUVI MMOJA MMOJA
Dkt. Sekadende anasema hatua hiyo itawaondoa wavuvi kwenye uvuvi wa kujikimu na kwenda kwenye uvuvi wa kibiashara, kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki na kipato,kufika maeneo ya uvuvi wa kina kirefu yenye samaki wengi zaidi na kuvua kwa muda mrefu na kwa ufanisi mkubwa.
Aidha uvuvi wa kutumia boti utapunguza gharama za uendeshaji kwa safari ndefu, kwa mvuvi mdogo, hii ni hatua ya kihistoria kutoka uvuvi wa “leo nile, kesho nione” kwenda uvuvi wa mapato yanayotabirika, yanayoweza kugharamia elimu, afya na uwekezaji mwingine wa kifamilia.
Usalama wa maisha baharini utakuwa ni wa uhakika kwani ajali za kuzama, kupotea baharini na vifo vya wavuvi ambazo zimekuwa ni changamoto sugu, hasa kwa wanaotumia mitumbwi dhaifu, utakuwa ni wa uhakika.
Kukopeshwa kwa boti za kisasa zilizo na injini imara,
vifaa vya mawasiliano,jaketi za kujiokoa, kutapunguza kwa kiasi kikubwa hatari za vifo na ajali. Hii ni faida ya kijamii isiyoonekana moja kwa moja kwenye takwimu za pato, lakini yenye uzito mkubwa kwa jamii za pwani na kwenye maziwa.
Mpango huu utahamasisha uvuvi halali na uzingatiaji wa sheria kwani mvuvi anayepata boti kwa mkopo wa serikali huingizwa rasmi kwenye mfumo wa usajili, leseni na ufuatiliaji (Monitoring, Control and Surveillance – MCS).
Hatua hii humtoa kwenye mazingira ya uvuvi haramu na kumfanya kuwa mshirika wa serikali katika uhifadhi wa rasilimali za uvuvi na bahari kwa ujumla.
FAIDA KWA TAIFA
Hatua hii itaimarisha Uchumi wa Buluu na mapato ya umma kuongezeka, kupanua msingi wa Uchumi wa Buluu kwani
kwa muda mrefu, Tanzania imekuwa na rasilimali kubwa ya bahari lakini imekuwa na mchango mdogo kiuchumi.
Mkopo huo utawezesha wavuvi kuongeza uzalishaji wa samaki,
kupunguza utegemezi wa samaki kutoka nje,
kufungua fursa za usindikaji, uhifadhi na usafirishaji na inabadilisha uvuvi kuwa sekta ya kimkakati, si shughuli ya pembeni.
Mapato ya Serikali yataongezeka kwani wavuvi walioko kwenye mfumo rasmi hulipa ada za leseni,huchangia kodi kupitia minyororo ya thamani na hutoa data sahihi za uzalishaji.
Hii huisaidia serikali kupanga sera bora zaidi, kuepuka uvuvi kupita kiasi, na kudhibiti upotevu wa mapato unaosababishwa na uvuvi haramu.
Aidha hupunguza shinikizo kwa rasilimali za karibu na fukwe, ambako wavuvi wengi huendeleza uvuvi wa jadi unaoegemea maeneo ya karibu na mwambao, hali inayosababisha uvuvi kupita kiasi na uharibifu wa mazalia ya samaki.
Boti za kisasa zinapowawezesha wavuvi kwenda mbali zaidi, shinikizo kwenye ikolojia ya mwambao hupungua, jambo linaloendana na misingi ya uvuvi endelevu.
Uamuzi wa serikali kuwakopesha wavuvi wadogo boti za kisasa ni hatua sahihi ya kimkakati inayolingana na sera za taifa, sheria za uvuvi na dira ya uchumi wa buluu.
Ni uwekezaji unaoweza kumbadilisha mvuvi mmoja mmoja kiuchumi na kijamii na kuliwezesha taifa kuvuna ipasavyo rasilimali zake za maji.
0 Comments