Vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu fursa ya upendeleo wa kisheria uliyopo kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023.
Wakati kifungu cha 64(1-3) kinatoa haki kwa makundi maalum wakiwemo vijana kutengewa kiwango cha asilimia 30 ya ununuzi ya mwaka kwa ajili ya makundi maalum ya kijamii kwa kuzingatia taratibu zilizoanishwa katika kanuni, bado kuna utekelezaji dhaifu wa kuyashirikisha kikamilifu makundi hayo.
Hatua hiyo ya kukosa ushirikishwaji wa kutosha, inawatenga vijana wa Kinondoni na fursa zilizopo ndani ya wilaya yao kwenye eneo la miradi ya ununuzi wa umma.
Ikikumbukwe kuwa ununuzi wa umma ni moja ya nguzo muhimu za utekelezaji wa bajeti ya Serikali na chombo kikuu cha kuchochea uchumi wa ndani.
Kila mwaka, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hutumia mabilioni ya shilingi kununua bidhaa, huduma na kazi mbalimbali kupitia taasisi zake.
Kwa kutambua nafasi hiyo ya kimkakati, Serikali imeweka utaratibu mahsusi wa kuzishirikisha jamii za makundi maalum hasa vijana katika mnyororo wa ununuzi wa umma, kama njia ya kukuza uchumi shirikishi na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
MATAKWA YA SHERIA NA KANUNI
Sheria ya Ununuzi wa Umma (Public Procurement Act) pamoja na kanuni zake zinazoongozwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), zinatambua rasmi umuhimu wa makundi maalum katika maendeleo ya taifa.
Sheria na kanuni zake zinazitaka taasisi zote za umma kutenga angalau asilimia 30 ya thamani ya manunuzi kwa makundi maalum, ambayo yanajumuisha vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Lengo kuu la utaratibu huu si upendeleo, bali ni kuondoa vikwazo vya kihistoria vilivyoyazuia makundi haya kushiriki kikamilifu katika fursa za kiuchumi, ikiwemo ushindani wa zabuni za Serikali.
| Bakari Mohamed, fundi ujenzi , akiwa kazini. |
Idadi kubwa ya vijana waliozungumza na mtadao huu, wamekiri kutoshirikishwa kwa namna yeyote kwenye fursa hii iliyopo kwenye eneo la ununuzi wilaya ya Kinondoni.
Said Ahmed (26), mjasiriamali anasema: Hakuna ushirikishwaji kwenye suala hilo, kifupi hatushirikishwi.”
Maimuna Mjalasa mkazi wa Bunju, Kinondoni -Dar es Salaam,(30), ambaye ni mfanyabiashara mdogo wa mboga mboga anasema: Sijui lolote kwakweli, hakuna ushirikishwaji”
Christian Msamba (25), mfanyabiashara wa bodaboda ambaye anaendesha shughuli yake kwenye kituo cha bodaboda cha Wazo anasema kuwa: Suala la ununuzi wa umma ni jambo jipya kwangu. Sijawahi kushiriki wala kushirikishwa.
Charles Kiyuga, ambaye anajihusisha na ujenzi, anasema hajawahi kusikia chochote kuhusu fursa inayotolewa kwenye ununuzi wa umma wilaya ya Kinondoni.
“Sijui lolote kwakweli.”
Bakari Mohamed, fundi ujenzi yeye anasema:Nilisikia kuna sheria ya kutoa asilimia 30 kwa makundi maalum, lakini nataka kujua jinsi ya kuunda kikundi, jinsi ya kupata cheti na jinsi ya kuomba zabuni hizo, hatujapata mafunzo. Hebu tushirikishwe kwenye haya mambo ili tuondokane na kilio cha ajira.”
Kwa upande wa Zainab Magabala (23), muuza mazao ya kilimo hakusita kuweka wazi kuwa:
“Tunahitaji kushirikishwa na pia tunapaswa kupewa elimu ya vitendo kuhusu namna ya kushiriki katika zabuni hizi; siyo tu taarifa fupi kutoka kwenye vyombo vya habari, bali mafunzo ya jinsi ya kujiandikisha na kushindana kikamilifu.”
Ikumbukwe kuwa vijana ndani ya Mtaa wa Nyakasangwe uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wanapaswa kushirikishwa na kunufaika na mradi wa ujenzi wa barabara wa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita 7.32 wa DMDP II, unaosimamiwa na Wawala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA). Mradi huo unakadiriwa kugharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 2.
VIONGOZI WA MITAA WAKIRI UDHAIFU
Kwa upande wa viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Mtaa na Kata wamekiri kuwepo kwa udhaifu katika utekelezaji wa sheria hiyo, ambayo wengi wao hawaijui.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyakasangwe, Kata ya Wazo wilayani Kinondoni, Zuhura Mabewa, ameweka wazi kuwa haijui sheria hiyo na hajawahi hata kupata semina juu ya fursa iliyopo kwenye ununuzi wa umma.
“Kuna udhaifu kwenye utekelezaji wa hiyo sheria, kwanza niseme wazi kuwa sijui chochote juu ya sheria hii, nikushukuru wewe kwa kuja kuniambia, nadhani sasa itakuwa ni jukumu langu kuhakikisha vijana na hayo makundi maalum yaliyopo kwenye eneo langu wanafaidika na fursa hiyo.
“Ni kweli vijana hawashirikishwi, kama mimi kiongozi wa mtaa sina ninachojua, unadhani wao watapata wapi huo ushirikishwaji. Wana haki ya kushirikishwa.”
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Wazo, Mante Ntonja alisema anaijua hiyo fursa na kwamba ofisi yake kwa kushirikiana na ofisi ya Maendeleo ya Jamii Kata, wamekuwa wepesi kuyasaidia makundi maalum kupata mikopo ya asilimia 10 ili kukuza mitaji yao na hatimaye kufanikiwa kuingia kwenye fursa zilizopo kwenye manunuzi ya umma.
Diwani wa Kata ya Wazo, Grace Mkumbwa amesema hana uelewa wa kutosha wa fursa hiyo iliyopo kwenye manunuzi ya umma, lakini anakiri kuwa ipo haja kwa vijana kushirikishwa kikamilifu kwenye fursa hiyo na nyengine zilizopo wilaya ya Kinondoni.
“Sina uelewa wa kutosha na hilo suala la fursa iliyopo kwenye manunuzi ya umma, lakini najua kuna ile mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, nimekuwa nikihakikisha vijana na makundi mengine wanaichangamkia fursa hii. Hata hivyo, baada ya kupata taarifa hii, sasa nitakuwa na nyongeza ya fursa ambayo nitaitumia kuwapa vijana na makundi mengine.”
| Afisa Manunuzi Wilaya ya kinondoni, Bi. Vumilia Tigwela (kushoto) akiwa kwenye mahojiano na Mwandishi wa makala haya, Jimmy Kiango (kulia) |
AFISA UNUNUZI: NI JUKUMU LA WOTE
Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Vumilia Tigwela, amesema kuwa ni kweli hakuna ushirikishwaji wa kutosha kwa vijana juu ya jambo hilo.
Bi. Vumilia, anasema njia pekee ya kuifikisha elimu itakayosaidia ushiriki wa haraka wa vijana ni kuwafuata vyuoni kwa kuanza kuwapa elimu ya jambo hili mapema ili waanze kuchangamkia fursa hata kabla ya kumaliza elimu zao.
Hata hivyo ameeleza kuwa, elimu na ushirikishwaji wa vijana na makundi mengine inapaswa kutolewa na taasisi zote zinazohusika na vijana.
“Suala la ushirikishaji wa vijana si la Halmashauri pekee, tunapaswa kutoa wote, na hata PPRA tunashirikiana nao sana, na pia nilishawahi kuwaambia wawe wanakwenda vyuoni kutoa elimu hiyo kwa upande wa vijana ili iweze kuwafikia kwa haraka.
Amesema ofisi yake kwa kushirikiana na ofisi ya Maendeleo ya jamii wamekuwa wakitoa elimu kwa makundi maalum kabla hawajapewa mikopo na kuwaambia kuwa kuna fursa kwenye ununuzi wa umma.
Pamoja na kukiri kutokuwepo kwa elimu na ushirikishwaji wa kutosha kwa vijana, lakini pia Bi. Vumilia ameieleza changamoto nyingine iliyopo kwenye kufanikisha jambo hilo kuwa ni Kanuni kuyabana makundi hayo hasa yaliyopo mjini kwa kutaka wahusika wote wawe wanatoka eneo moja, jambo ambalo ni gumu.
“Unapozungumzia vijana waliopo vyuoni, maana yake unazungumzia vijana wanaoishi maeneo tofauti tofauti, kitendo cha kuwataka wote watoke eneo moja, ni wazi kinawanyima fursa ya kuungana kwa sababu wengi wao hawaishi kwenye eneo moja hasa kwa wakazi wa mijini.
“Vigezo vipunguzwe mijini, kikubwa kijana awe mkazi wa jiji au mji huo ili mradi wanakutana katika maeneo ambayo yanaweza kufikika. Kikundi kikubaliwe hata kama wanakikundi wanakaa mbalimbali na mmoja akiwa yuko maeneo hayo na wanajuana na wenzake waweze kusajiliwa.”
UMUHIMU WA KUWASHIRIKISHA VIJANA
Daglass Said ni muhimu kwa vijana kushirikishwa kwenye fursa iliyopo kwenye ununuzi wa umma na kwamba hatua hiyo itasaidia kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira.
“Takwimu zinaonesha kuwa vijana ni kundi kubwa zaidi la nguvu kazi nchini, lakini pia ndilo linalokabiliwa zaidi na tatizo la ukosefu wa ajira. “Kushiriki katika ununuzi wa umma kunawapa vijana fursa za kujiajiri kupitia vikundi au kampuni ndogo, uzoefu wa kibiashara unaotambulika kisheria, mtaji wa kuendeleza biashara na kupanua ajira kwa vijana wengine.”
Saidi aliongeza kuwa ushirikishwaji wa vijana utasaidia kukuza ujasiriamali na ubunifu, vijana wengi wana ujuzi, ubunifu na uwezo wa kutoa huduma au bidhaa kwa gharama nafuu na ubora unaokubalika.
Ununuzi wa umma unawapa soko la uhakika, linalowezesha kukua kwa biashara changa, kuimarika kwa uchumi wa ndani na kupunguza utegemezi wa wazabuni wakubwa pekee.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ambacho pia kinajumuisha vijana wanawake, Mwajuma Hamza amesema ushiriki wa vijana kwenye ununuzi wa umma utasaidia kujenga uchumi jumuishi na endelevu.
“Kwa kushirikisha vijana katika manunuzi ya Serikali, Taifa linajenga msingi wa uchumi jumuishi unaohakikisha kwamba makundi yote yanashiriki na kunufaika na rasilimali za umma, hivyo kuimarisha mshikamano wa kijamii na kiuchumi.”
NI WAJIBU WA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA
Licha ya uwepo wa sera, sheria na nia njema ya Serikali, bado kumekuwepo na changamoto ya uelewa mdogo miongoni mwa vijana kuhusu fursa hizi, hata hivyo, Meneja wa Kanda ya Pwani kutoka PPRA, Bi. Vicky Mollel anasema vijana wanalo jukumu la kuzitafuta na kuzichangamkia fursa hizo.
Anasema ni wajibu wa vijana kujifunza misingi ya sheria ya ununuzi wa umma, kuelewa haki na wajibu wao kama wazabuni wa makundi maalum, kuachana na dhana potofu kuwa zabuni ni kwa watu wakubwa pekee.
“Kutoitumia fursa ya asilimia 30 ni sawa na kuacha rasilimali ya kisheria ipite bila manufaa kwa kundi lililokusudiwa.”
CHANGAMOTO ZILIZOPO
Bi. Vicky amesema miongoni mwa changamoto zilizopo ni kukosekana kwa muitikio na mahudhurio hafifu: Muitikio wakati mwingine unakuwa mdogo, wanaotakiwa kupata elimu hiyo hawahudhurii.
Changamoto nyingine ni kukosekana kwa ufuatiliaji, ambapo wahusika hawafuatilii na hata baadhi ya wanaopata elimu hiyo pia, hawafuatilii fursa hizo wala kuyachukulia mafunzo hayo kuwa ni fursa kwao. Wengi wao wanaweka dhana potofu kuwa, kufanya kazi na serikali ni shida.
MBINU ZINAZOHITAJIKA
Ili vijana vijana kupata taarifa sahihi na kushiriki kikamilifu kwenye fursa hiyo wanapaswa kujiunga na kuanzisha vikundi au kusajili biashara.
Sheria ya ununuzi wa umma inaruhusu vijana kushiriki kupitia vikundi vilivyosajiliwa kisheria
kampuni au biashara ndogo zilizosajiliwa BRELA,
Ushirika au SACCOS za vijana.
Ni muhimu vikundi hivi viwe na nyaraka halali, ikiwemo cheti cha usajili, TIN, Akaunti ya benki ya kikundi au kampuni, kujisajili na kutumia mfumo wa NeST.
NeST (National e-Procurement System of Tanzania) ni mfumo rasmi wa kielektroniki unaotumika kusimamia manunuzi yote ya umma.
Vijana wanapaswa kujisajili kama wazabuni kwenye mfumo huo na kuhakiki taarifa zao mara kwa mara. Kwa kufuatilia matangazo ya zabuni yaliyotengwa kwa makundi maalum, kupitia NeST, vijana wanaweza kupata taarifa sahihi, kwa wakati, na kwa uwazi bila kutegemea watu wa kati.
Aidha, vijana wanashauriwa kushirikiana na Taasisi za Serikali na Asasi za Kiraia kama vile PPRA kwa mafunzo na miongozo, Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri), Asasi za kiraia zinazotoa elimu ya ununuzi wa umma. Ushirikiano huo, unasaidia kuongeza uelewa, kuondoa hofu na kujenga uwezo wa kushindana kibiashara.
USHIRIKISHWAJI WA VIJANA SI HISANI
Bi. Vumilia anasema ushirikishwaji wa vijana katika ununuzi wa umma si hisani, bali ni haki ya kisheria na mkakati wa maendeleo ya Taifa.
Sheria ya ununuzi wa umma na kanuni za PPRA zimeweka mazingira rafiki kwa vijana kushiriki, lakini mafanikio yake yatategemea kwa kiasi kikubwa uelewa, utayari na ujasiri wa vijana wenyewe.
Kwa kujiunga kwenye vikundi halali, kutumia mfumo wa NeST, na kufuatilia taarifa sahihi, vijana wanaweza kugeuza fursa ya asilimia 30 kuwa suluhisho la kudumu la changamoto ya ukosefu wa ajira na kuwa sehemu hai ya uchumi wa Taifa.
0 Comments