Ticker

7/recent/ticker-posts

UKATAJI WA MITI WAPUNGUZA SOKWE HIFADHI YA TAIFA GOMBE

NA. ADELA MADYANE-KIGOMA

Ukataji wa misitu ndani na pembezoni mwa hifadhi za taifa umeendelea kuwa changamoto kubwa ya kimazingira nchini, huku athari zake zikionekana moja kwa moja kwa viumbe hai wanaotegemea misitu hiyo kwa uhai wao.

Katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe na maeneo ya jirani, ukataji wa miti umekuwa moja ya sababu zinazoendelea kuhatarisha uwepo wa sokwe, mnyama adimu na mwenye mchango mkubwa katika mfumo wa ikolojia.


Takwimu za setilaiti kutoka Global Forest Watch zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2001 na 2023, Tanzania imepoteza zaidi ya hekta milioni mbili za misitu ambayo ni muhimu kwa uhifadhi wa sokwe.


Kwa mujibu wa picha na video za setilaiti za NASA, mkoa wa Kigoma, hususan Milima ya Gombe na maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo, unakumbwa na kupungua au kutoweka kwa misitu asilia hali inayochangia kupungua kwa makazi na chakula cha sokwe.


SABABU ZA UHARIFUMU WA MISITU

Akitaja sababu za uharibifu katika maeneo hayo afisa wanyamapori wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma, Alfred Msangi, anasema ongezeko la idadi ya watu ambalo limeongezeka kwa asilimia 37 ya mwaka 2012 na 2022 katika ukanda wa ziwa Tanganyika limechochea kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukataji miti haramu wakitafuta eneo la kilimo na makazi na hivyo kujikuta wakiingia hifadhini.


“Wanapoingia msituni, huingia katikati ya msitu ambako kuna rutuba ya kutosha, na huko huanzisha makazi yasiyo rasmi, kufanya shughuli za kilimo na kukata mkaa jambo hili linaumiza mno maisha ya wanyama pori hussuan sokwe,” anasema Msangi.


Kwa mujibu wa afisa huyo anasema takribani asilimia mbili ya korido ya sokwe ya Gombe–Burundi yenye ukubwa wa hekta 10,030 tayari imeharibiwa kutokana na shughuli za kilimo, uzalishaji wa mkaa na uanzishaji wa makazi ya watu.


Kwa upande wake Magdalena Philipo mkulima kutoka kijiji cha Zashe anasema misitu hukatwa zaidi ili kupata mahitaji ya msingi ya kupata nishati ya kupikia ikiwemo kuni na mkaa kwakuwa wananchi wengi wa kijiji honcho zaidi ya asilimia 80 hutumia.


Naye Christine Ntabhonye anasema sababu nyingine ni umaskini na ukosefu wa vyanzo mbadala vya kipato kwakuwa wananchi wengi wanaozunguka hifadhi ya Gombe ni wakulima na wavuvi na hivyo ili kupata njia mbadala ya kupata kipato hulazimika kukata miti kwaajili ya kupata mkaa na kuuza.


Aidha, Joshua Swalehe anasema mabadiliko ya tabianchi yamezidisha tatizo nalo ni tatizo linalosababisha uharibifu wa misitu kwakuwa sasa mvua hazitabiriki, na kumekuwa na ukame wa mara kwa mara akitaja kwamba ili upate eneo lenye rutuba kwaajili ya kilimo lazima uende sehemu za msitui.


Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Alfred Msangi, anakiri kuwa ukataji wa misitu katika maeneo ya hifadhi na yale ya akiba umeongezeka kutokana na shinikizo la kijamii na kiuchumi, huku uwezo wa usimamizi ukiwa mdogo.


Kwa upande wake afisa maliasili wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma, Vicent Muhazi, anasema halmashauri imejiwekea mipango mbalimbali ya kuboresha mazingira ikiwemo kuwaondoa wavamizi katika misitu hifadhi ili kurejesha uoto wa asili na kuongeza idadi ya wanyamapori, hususan nyani wakbwa.


Muhezi anakiri kuwa kwa sasa sokwe wanakabiliwa na tishio la kutoweka kutokana na kuendelea kupungua kwa makazi na vyanzo vya chakula katika Hifadhi ya Milima ya Gombe, pamoja na hatari ya magonjwa ya kuambukiza kutoka kwa binadamu kwenda kwa wanyama (magonjwa ya zoonotiki).

Hali halisi

Takwimu za Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) zinaonyesha kuwa idadi ya sokwe katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe imepungua kwa kiasi kikubwa, kutoka sokwe wapatao 300 mwaka 1980 hadi kufikia 85 pekee mwaka 2024, huku wataalamu wakieleza kuwa kupungua huku kunahusishwa moja kwa moja na upotevu wa misitu inayozunguka hifadhi hiyo.


Kwa mujibu wa utafiti wa uhifadhi, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 7.5 ya makazi ya sokwe hupotea kila mwaka katika ukanda wa Gombe.

USHAHIDI WA KIMAZINGIRA

Akizungumza juu ya upungufu wa viumbe hivyo, Moshi Batumunwa, diwani wa kata ya Mwamgongo, anasema kuwa hapo awali walikuwa wakisikia sauti za sokwe kila asubuhi kutoka vilimani lakini sasa inapita miaka bila kusikia sauti hizo.


Anasema kipindi cha nyuma alikuwa akishuhudia sokwe wakipita katika mashamba ya wanakijiji, ambapo wakazi walipewa maelekezo ya kuwafukuza taratibu warudi msituni bila kuwadhuru jambo ambalo halipo kwa nyakati hizi au hutokea mara chache.


Naye ssa Tumuza (70), mkazi wa kijiji cha Kilemba, anasema misitu iliyokuwa minene miaka ya nyuma sasa imebakia vipande vipande akikiri kuwa shinikizo la maisha limechangia wananchi kuharibu misitu bila mipango.

“Watu wanakata misitu si kwa sababu hawajui madhara, bali kwa sababu wanahitaji kuishi,” anasema.

 

WAJIBU WA VIONGOZI

adau wa mazingira wanasema kuwa suluhu ya kudumu iko katika kushirikisha jamii kikamilifu katika uhifadhi, upanuzi wa matumizi ya nishati mbadala, kuboresha kilimo endelevu, kutoa elimu ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi huenda ikawa mwarobaini wa kutibu janga hilo.


Kwa upande wake, Alfa Haga (65), mkazi wa Kijiji cha Nyarubanda mkoani anakiri kuwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali, sera za mazingira kwa sasa zinatoa nafasi kubwa kwa ushiriki wa wananchi japo ushiriki wao bad oni mdogo.


Anasema kuwa kutokana na ushirikiano uliopo kati ya mamlaka za uhifadhi, serikali za mitaa, watafiti wa wanyamapori pamoja na wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi za taifa, uhifadhi shirikishi umeanza kuzaa matunda, japokuwa dhana hiyo imeanza kutekelezwa baada ya uharibifu mkubwa tayari kutokea.


Naye, Kasogota Emmanuel ameziomba mamlaka zinahosika na mabadiliko ya tabia nchi kuendelea kutafuta fedha za hasara na uharibifu unaoendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali ili wananchi waweze kujikita katika shughuli nyingine za kujiingizia kipato badala ya kuendelea kuharibu mazingira.


Afisa Maliasili wa Wilaya ya Kigoma, Bw. Vincent Mhezi, amesema kuwa Halmashauri imepanga kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka sambamba na kuwaondoa wavamizi katika misitu hifadhi, hata hivyo changamoto ya upungufu mkubwa wa fedha bado ni kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa mipango hiyo.


Amesema uamuzi wa hivi karibuni wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa kusitisha misaada ya kigeni kwa nchi nyingi pamoja na miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Shirika la USAID, ni miongoni mwa hatari zinazozojitokeza katika kuendeleza shughuli za uhifadhi.


“Shughuli nyingi za urejeshaji wa mazingira zimesimama, sasa tunategemea mapato ya ndani ya halmashauri, ambayo hayawezi kabisa kukidhi ukubwa wa tatizo lililopo,” anasema Mhezi.


Mhezi anawaomba wananchi kuendelea kujitolea ki fedha pamoja na kiuchumi ili kukabiliana na tatizo la uhifadhi linaoendelea zaidi unaoendana na uharibifu wa mazingira.

Post a Comment

0 Comments