Ticker

7/recent/ticker-posts

MAENEO 7 MUHIMU YANAYOWEZA KUOKOA MAZINGIRA YA BAHARI DAR BAADA YA COP30

  

NA JIMMY KIANGO

Mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC COP30) wadau wa mazingira ya bahari wameyaanisha maeneo saba ambayo yakitekelezwa kikamilifu yanaweza kuyaokoa mazingira ya bahari yanayochafuliwa na utupaji holela wa taka za plastiki, hasa jijini Dar es Salaam.

 

Ikumbukwe kuwa mkoa wa Dar es Salaam ndio unatajwa kuwa mzalishaji mkuu wa takataka nchini, ambapo unakadiriwa kuzalisha tani 4852 za taka kila siku huku wastani wa uzalishaji wa taka nchi nzima ukiwa ni zaidi ya tani 10,000.


Kwa mwaka 2024, ripoti ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ilionesha kuwa kwa mkoa wa Dar es Salaam, Wilaya ya Temeke ndio inaongoza kwa kuzalisha tani 1,494 za taka kwa siku, ikifuatwa na Ilala inayozalisha taka tani 1,320, Kinondoni tani 982, Ubungo tani 828 na Kigamboni tani 228 na tayari serikali ilikuwa na mchakato wa kupunguza taka hizo kwa kujenga vituo vya kukusanyia taka.

 

Hata hivyo kati ya asilimia 45 hadi 55 ya taka hizo hazikusanywi, kusafirishwa na kutupwa kwenye maeneo yaliyoanishwa kwa mujibu wa kifungu cha 114 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2025.   

 

Mkurugenzi wa Green Samia Foundation, Mhandisi Yohana Matiko anaweka wazi kuwa wakati nchi ikisubiri utekelezaji wa ahadi zilizotolewa COP30, ipo haja ya kuanza kushughulika na mambo saba ambayo kwake anayaona ni ya msingi.

 

Mambo hayo ni: 1. Kuimarisha sera na utekelezaji wa sheria za mazingira ya bahari.

“Baada ya COP30, Tanzania inaweza kupitia na kuhuisha utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, 2004 (EMA 2004) na kanuni zake ili kuweka mkazo mahsusi kwenye taka ngumu zinazoishia baharini.

 

“Kuongeza adhabu kwa watu, taasisi na viwanda vinavyotupa taka kwenye mito, fukwe na bahari. Kuanzisha mahakama au vitengo maalum vya kushughulikia makosa ya uchafuzi wa bahari na kuimarisha doria za mazingira katika maeneo ya pwani na bandari.”


2. Usimamizi shirikishi wa taka kuanzia nchi kavu hadi baharini

“Kwa kuwa taka nyingi za baharini hutoka nchi kavu, mikakati inapaswa kuanzia ngazi ya jamii, Halmashauri za Pwani ziboreshe mifumo ya ukusanyaji, usafirishaji na utupaji salama wa taka ngumu.

Mkurugenzi wa Green Samia Foundation, Mhandisi Yohana Matiko
“Kuanzisha vituo vya kuchakata taka (recycling hubs) karibu na miji ya pwani kama Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Zanzibar na kukuza dhana ya “source separation” ambapo taka zinachambuliwa kabla ya kutupwa.”

3. Kupiga marufuku na kudhibiti matumizi ya plastiki hatarishi.

“Baada ya COP30, Tanzania inaweza kupanua wigo wa marufuku ya plastiki:

Kudhibiti au kupiga marufuku plastiki za matumizi ya mara moja (single-use plastics) zinazotumika kwenye ufungashaji wa bidhaa.


Kukuza matumizi ya vifungashio mbadala vinavyoharibika kirahisi (biodegradable materials).

Kuwawajibisha wazalishaji kupitia mfumo wa Extended Producer Responsibility (EPR) ili wachangie gharama za kudhibiti taka za bidhaa zao.

 

4. Kuwezesha jamii za Pwani na wavuvi kuwa walinzi wa bahari:

Jamii za pwani ni wahanga wakuu wa uchafuzi wa bahari, hivyo ni wadau muhimu kuwaanzishia programu za elimu ya mazingira kwa wavuvi, wanawake na vijana wa pwani.

Kuweka motisha (fedha au vifaa) kwa vikundi vinavyokusanya taka kwenye fukwe na baharini.

 

Kuingiza usimamizi wa taka katika vikundi vya ulinzi wa mazingira ya bahari (Beach Management Units – BMUs).

 

5. Ubunifu wa teknolojia na Uchumi wa Buluu endelevu:

Matokeo ya COP30 yanaweza kutumika kuhamasisha uwekezaji katika suluhisho bunifu kwa kutumia teknolojia za kunasa taka baharini na kwenye mito kabla hazijafika baharini.

 

Kukuza miradi ya Uchumi wa Buluu inayotumia taka kama malighafi (mfano plastiki kuchakatwa kuwa bidhaa) na kushirikiana na sekta binafsi katika ubunifu wa mifumo ya taka rafiki kwa mazingira.

 

6. Ushirikiano wa kikanda na kimataifa:

Bahari haina mipaka, hivyo Tanzania inahitaji ushirikiano mpana ili kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika Mashariki kupitia mikataba ya kikanda ya bahari ya Hindi.

 

Kutumia fursa za fedha za mabadiliko ya tabianchi na mazingira zilizokubaliwa COP30 kufadhili miradi ya kudhibiti taka baharini na kushirikiana na mashirika ya kimataifa kufanya tafiti na ufuatiliaji wa uchafuzi wa bahari.

 

7. Ufuatiliaji, takwimu na uwajibikaji:

Mikakati itafanikiwa zaidi ikiwa kuna takwimu sahihi kwa kuanzisha mfumo wa kitaifa wa kukusanya na kuchambua takwimu za taka zinazoingia baharini.

Kufanya tathmini za mara kwa mara za athari za taka ngumu kwa ikolojia ya bahari, afya ya binadamu na uchumi na 

kuwasilisha taarifa za uwazi kwa umma kama sehemu ya uwajibikaji wa kitaifa na kimataifa.

 

Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Transforming life, inayojihusisha na usafi wa mazingira, Naishivai Mollel

AHADI ZA COP30 NI FURSA KWA TANZANIA

Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Transforming life, inayojihusisha na usafi wa mazingira, Naishivai Mollel anakubaliana na mapendekezo ya Mhandisi Matiku na kuongeza kuwa upo uwezekano mkubwa wa Tanzania kuzigeuza ahadi za COP30 kuwa fursa.

 

“Baada ya COP30, Tanzania ina fursa ya kugeuza ahadi za kimataifa kuwa vitendo vya kitaifa. Kupitia sera madhubuti, ushiriki wa jamii, teknolojia bunifu na ushirikiano wa kimataifa, nchi inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa bahari unaotokana na utupaji holela wa taka ngumu na kulinda rasilimali za bahari kwa kizazi cha sasa na kijacho.”

 

Mollel amesema kwa upande wao tayari wameshaanza utekelezaji wa baadhi ya mambo kwa kuendesha kampeni ya kusafisha bahari kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa Sekondari.

 

“Kampeni hii itasaidia kufanya fukwe za bahari Tanzania kuwa katika hali ya safi, na kuokoa maisha ya samaki, kuna uchafu mwingi baharini, unaofanya samaki wafikie kula vipande vya plastiki na kuhatarisha maisha yao na mazalia yao.”

 

Kwa upande wake Mratibu wa taasisi ya ya kijamii ya Sanamare inayojihusisha na ulinzi wa mazingira ya Bahari, Pius Silas anaweka wazi kuwa kwa sasa jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla haina sababu ya kusubiri utekelezaji wa ahadi za COP30, badala yake ianze kutekeleza baadhi ya mambo muhimu kama vile usimamizi madhubuti wa sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

 


SAUTI YA BAHARI

Wakati kukiwa na jitahada mbalimbali za kupaza sauti katika majukwaa ya dunia na kutolewa kwa ahadi mbalimbali za ulinzi wa bahari na kupata suluhu endelevu, bado jamii kubwa ya Pwani inaamini sauti hizo ni kama hazisikiki vema kwenye masikio ya watekeleza sheria, kwa sababu bado kuna udhaifu kwenye utekelezaji wa matakwa ya sheria.

 

Juma Athumani mvuvi wa Pwani ya Kigamboni anasema wazi kwua ahadi nyingi zinazotolewa kwenye mikutano ukiwemo wa wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Kitaifa wa Tabianchi na Jukwaa la Suluhu, pamoja na ahadi ya kuwasilisha Mpango wa Kitaifa wa Tabianchi baada ya COP30, zinazotolewa hadharani, hazibadilishwi kutoka kwenye maneno na kuwa katika  vitendo vinavyoonekana.

 

Mjumbe wa Kikosi cha Majadiliano cha Afrika (African Group of Negotiators, AGN), Dkt. Richard Mayungi

Hoja ya Juma inarandana na kauli ya Mjumbe wa Kikosi cha Majadiliano cha Afrika (African Group of Negotiators, AGN), Dkt. Richard Mayungi wakati akizungumza kuhusu mwelekeo wa Tanzania katika majadiliano ya tabianchi, alinukuliwa akieleza kuwa nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania, zinahitaji mifumo madhubuti ya ndani ili ahadi za kimataifa ziweze kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi. 

 

Dkt. Muyungi alisisitiza kuwa bila utekelezaji wa kitaifa, maazimio ya COP yanabaki kuwa kauli za kisiasa.

 

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Makamu wa Rais, Sarah Kibonde 

UTEKELZAJI WA AHADI ZA COP30 UNAENDELEA

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Makamu wa Rais, Sarah Kibonde alipozungumza na Afrinewsswahili hivi karibuni, amesema kimsingi Tanzania imeendelea kufuatilia ahadi zilizotolewa na wadau mbalimbali ambao Tanzania ilikutana nao katika kuimarisha jitihada za kitaifa na kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

 

Aliongeza kuwa ingawa masuala ya plastiki na uchafuzi wa bahari ilikuwa ni ganeda tofauti na COP30, alakini ujumbe wa Tanzania ulioshiriki kwenye mkutano huo ulifanya kazi ya ziada ili kuhakikisha suala la bahari linajadiliwa kwenye vikao vya pembeni.

 

“Hili suala halikuwa rasmi, lakini jitihada zilifanyika, zimefanyika na zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha bahari inakuwa salama, tumekuwa tukiendelea kupokea maoni, mawazo, mapendekezo na ushauri wa wadau juu ya kuilinda bahari na serikali haijapuuza, inayafanyia kazi na mengine mengi utekelezaji umeanza.”


Bi. Sarah amesema katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira ya Bahari unaosababisha na utupaji holela wa taka ngumu, utekelezaji wa maoni ya wadau umekuwa ukifanyiwa kazi ambapo tayari nchi inaelekea kukamilisha Mpango wa Udhibiti wa Uchafuzi wa Bahari (Marine Litter Action Plan-MLAP).


Kazi hii ya kukamilisha MLPA inafanywa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, lengo likiwa ni kuhakikisha bahari inakuwa salama.  

Bi. Sarah, amesema hatua hiyo inatarajiwa kukamilika mwaka huu na dhamira kuu ni kuhakikisha mazingira ya bahari yanakuwa salama.

“Ofisi ya Makamu wa Rais inakamilisha Mpango wa Udhibiti wa Uchafuzi wa Bahari (Marine Litter Action Plan) naamini MLAP itasaidia katika harakati za kuilinda bahari,”amesema Bi. Sarah.

MATUMAINI ZAIDI ANTALYA
Pamoja na mambo mengine bado Tanzania inayo nafasi ya kuilinda bahari kwa mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho na wadau wanaamini sehemu pekee ambayo inaweza kubeba tumaini la bahari endelevu ni kwa mamlaka kusimamia sheria kikamilifu.

 

Aidha Mkutano wa COP31 nao unatazamwa kama mgongo wa tembo uliobeba matumaini ya kuikoa bahari ya ya Tanzania na duniani kwa ujumla, kwani mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 9-20 mwaka huu kwenye jiji la Antalya, Uturuki unatazamwa kama sehemu ya kwenda kuhitaji vitendo zaidi ya maneno.

 

Post a Comment

0 Comments