Akiwasilisha mada kuhusu matokeo ya COP30 na dhana ya mpito wa haki katika mabadiliko ya tabianchi, Anderson amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee kusukuma ajenda ya haki ya tabianchi kwa kutumia ushahidi, takwimu na uchambuzi wa kina. Anasema
mataifa yanayoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi yana mchango mdogo katika
uchafuzi wa mazingira, hivyo nchi tajiri zinapaswa kupunguza uzalishaji wa gesi
joto na kuongeza ufadhili wa kukabiliana na athari hizo. Kauli hiyo imetolewa katika mafunzo
ya uandishi wa habari za tabianchi yaliyoandaliwa na Media for Environment, Science,
Health and Agriculture (MESHA) kwa kushirikiana na International Development
Research Centre (IDRC), yakihusisha wanahabari kutoka Tanzania, Kenya, Uganda,
Zimbabwe, Zambia na Malawi kupitia programu ya Cross Border Science Café. AFRIKA NA MZIGO WA ATHARI ZA TABIANCHI Wakati Afrika ikiendelea kuwa miongoni mwa maeneo yanayoathirika zaidi kwa mafuriko, ukame na mabadiliko yasiyotabirika ya mvua, wadau wa mazingira wameona umuhimu wa kuwawezesha wanahabari kuripoti kwa kina masuala hayo. Lengo ni kuhakikisha jamii zinaelewa chanzo cha changamoto na kushiriki kikamilifu katika suluhisho. Kwa mujibu wa Anderson, uandishi wa
tabianchi lazima uweke mbele haki za jamii zilizo hatarini zaidi, na ufuatilie
kwa karibu ahadi na sera zinazotolewa katika mikutano ya kimataifa ya tabianchi
kama COP. Amesema pia kuwa kiwango cha fedha kinachotolewa kupitia Mfuko wa
Hasara na Uharibifu (FRLD) hakilingani na mahitaji halisi, akieleza kuwa dola
milioni 250 zilizotengwa ni ndogo ukilinganisha na hitaji la takribani dola bilioni
395 kwa mwaka. TABIANCHI,JINSIA NA AFYA NI MZIGO KWA WANAWAKE Mabadiliko ya tabianchi si suala la
mazingira pekee, bali pia ni la kijinsia na kiafya. Wataalamu wanasema wanawake
na wasichana huathirika zaidi kutokana na mifumo ya kijamii inayowaweka katika
hatari kubwa wakati wa majanga ya kimazingira. Uhaba wa maji bado ni changamoto kwa wanawake wengi Afrika Meneja wa Mawasiliano wa Mission
Inclusion, Audrey Masitsa, anaeleza kuwa ukame na upungufu wa mvua husababisha
wanawake kutembea umbali mrefu kutafuta maji na kuni, hali inayowaweka katika
hatari ya ukatili wa kijinsia na changamoto za kiafya. Anasisitiza kuwa mawasiliano
yenye ushahidi yanaweza kuhamasisha hatua za haki na kubadili simulizi potofu
zinazowaonyesha wanawake kama wahanga pekee.
Badala yake, wanawake pia wanaongoza
suluhisho. Katika baadhi ya maeneo, wamekuwa mstari wa mbele kusimamia mikoko
na miradi ya uhifadhi wa mazingira, hatua inayochangia kulinda fukwe,
kuimarisha kipato na kukuza uongozi wao katika jamii. Wanawake wakishiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira kwa kupanda mikoko wilayani Pangani, mkoani Tanga Kwa upande wake, Kiongozi wa Mkakati
na Masuala ya Kiufundi kutoka African Centre for Health, Climate and Gender
Justice Alliance (ACHCGA), Imali Ngusale, anasema ushirikiano kati ya wataalamu
na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha taarifa sahihi za kisayansi
zinafika kwa umma na kwamba ahadi za serikali zinatekelezwa. WAJIBU WA VYOMBO VYA HABARI Washiriki wa mafunzo hayo
wamekubaliana kuwa uandishi unaozingatia jinsia si utetezi bali ni wajibu wa
kitaaluma unaolenga kutoa taarifa kamili na zenye muktadha. Wanahabari
wametakiwa kuongeza uchunguzi kuhusu matumizi ya fedha za tabianchi, kufuatilia
utekelezaji wa sera, na kuandika simulizi zinazoonesha suluhisho pamoja na
changamoto. Katika kipindi ambacho mabadiliko ya
tabianchi yanaongeza ukosefu wa usawa, hasa kwa wanawake, vyombo vya habari
vina jukumu la kubadili mwelekeo wa simulizi kutoka kwa taarifa za kawaida hadi
habari za ushahidi, uwajibikaji na ushawishi wa kisera. Kwa kufanya hivyo, uandishi wa
habari unaweza kuwa kichocheo cha haki ya tabianchi, usawa wa kijinsia na
maendeleo endelevu barani Afrika.
|



0 Comments