Ticker

7/recent/ticker-posts

KUTOTEKELEZA SHARTI LA 30% YA UNUNUZI WA UMMA KWA MAKUNDI MAALUM NI KOSA LA JINAI


NA. JIMMY KIANGO

“Kutojua sheria si kigezo cha kuvunja sheria.” Hatua yeyote ile ya kutotekeleza matakwa ya sheria ya Ununuzi wa Umma ikiwemo kukiuka masharti yanayohusu upendeleo wa utoaji zabuni kwa makundi maalum yaliyoanishwa kisheria ni kosa la jinai na mtu huyo akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi milioni kumi au kifungo kwa kipindi kisichozidi miaka mitatu au vyote.

Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 128(2d) na(2f) cha Sheria ya Ununuzi, ambapo lengo la kuweka adhabu hiyo ni kuhakikisha watu wote wanaopaswa kuitekeleza sheria hiyo wanawajibika kikamilifu kwa kutoa upendeleo kwa kundi maalum la vijana ambalo ni sehemu ya makundi manne yaliyotajwa na sheria hiyo sanjari na Wanawake, Wazee na Watu wenye mahitaji maalum.  

Sheria ya Ununuzi wa Umma kifungu cha 64(1-3) imeweka shariti kwa taasisi nunuzi kutenga kiwango cha asilimia (30) ya ununuzi ya mwaka kwa ajili ya makundi maalum ya kijamii kwa kuzingatia taratibu zilizoainishwa katika kanuni. 

 

Sheria hiyo imejenga msingi na nyenzo madhubuti za kuhakikisha makundi maalum yanashiriki kikamilifu katika fursa za kiuchumi zinazotokana na matumizi ya fedha za umma. 

Moja ya nyenzo muhimu ni kutengwa kwa asilimia 30 ya thamani ya manunuzi ya umma kwa makundi maalum. 

 

Hata hivyo utekelezaji wa Sheria hiyo unategemea kwa kiwango kikubwa uwajibikaji na ubunifu wa viongozi wa ngazi za chini za serikali, ambao wako karibu zaidi na walengwa.


 
KUKOSEKANA KWA UFAHAMU WA FURSA

Hali ni tofauti ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni , uchunguzi mdogo uliohusu mradi wa ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara yenye urefu wa Km 7.32 ya Nyakasangwe-Bwawani unaoendelea kwenye Kata ya Wazo, Dar es Salaam umebaini kuwepo kwa udhaifu katika kutekeleza sheria hiyo na baadhi ya watu wanaopaswa kuitekeleza hawana ufahamu wa kutosha hali inayowaondolea vijana haki ya kunufaika na mradi huo.

 

Miongoni mwa watu wasio na ufahamu na sheria  hiyo ni Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Charles Lawisso, Diwani Kata ya Wazo, Grace Mkumbwa na Mwenyekiti Serikali ya Mtaa wa Nyakasangwe, Zuhura Mabewa.

 

Katika mazungumzo yake na mtandao huu, mara baada ya kuulizwa kuhusu ofisi yake kusimamia utekelezaji wa kifungu cha 64 (1-3) cha sheria hiyo, Lawisso alionesha kushangaa na kumuhoji mwandishi wa habari hii iwapo ameshawauliza PPRA, ambapo alijibiwa kuwa tayari mahojiano na PPRA yameshafanyika.

 

Mtandao huu ulitaka kupata maelezo juu ya namna ofisi ya Mwanasheria wa Halmashauri ya Kinondoni inavyosimamia utekelezaji wa sheria hiyo na changamoto zilizopo, ambapo alisema kuwa atakuwa tayari kutoa majibu mara baada ya kuisoma.

 

“Ngoja nikaisome hiyo Sheria ndio nitakujibu.”amesema kwa msisitizo. Alipotafutwa tena hakupatikana.

 

Kwa upande wake Diwani waKata ya Wazo, Bi. Mkumbwa alisema hana ufahamu wa kutosha juu ya hiyo sheria. “Niwe mkweli sina ufahamu wa kutosha juu ya hiyo sheria.”

 

Nae Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa, Bi. Zuhura Mabewa alisema moja kwa moja: Siijui hiyo fursa.

 


VIONGOZI WAAHIDI UWAJIBIKAJI

Baaada ya kubaini kuwa baadhi ya viongozi na wananchi wa Kata ya Wazo wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam, hawana ufahamu wowote juu ya fursa hiyo ya ununuzi wa umma kwa makundi maalum, mamlaka na viongozi wameeleza hatua wanazochukua ili kuziba pengo hilo la uwajibikaji.

 

Kutokana na changamoto ya kutokuwa na ufahamu juu ya sheria hiyo, Diwani Mkumbwa amesema ni jukumu lake sasa kukutana na vijana mara kwa mara kwenye Kata yake ili kuwahamasiaha kuanzisha vikundi na kuchangamkia fursa hiyo ya zabuni sambamba na fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.

 

“Ni jukumu langu sasa kuhakikisha kwa nafasi yangu nafanikisha jambp hilo na njia pekee nitakayoifanya ni kukutana na vijana na makundi mengine ili kuhakikisha wanaijua fursa hiyo ya asilimia 30 na kuichangamkia.”

 

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Wazo, Mante Ntonja alisema anaijua hiyo fursa na kwamba ofisi yake kwa kushirikiana na ofisi ya Maendeleo ya Jamii Kata, wamekuwa wepesi kuyasaidia makundi maalum kupata mikopo ya asilimia 10 ili kukuza mitaji yao na hatimaye kufanikiwa kuingia kwenye fursa zilizopo kwenye manunuzi ya umma. 

 

“Tutaendelea kutekeleza jukumu letu la kuwaletea maendeleo vijana na makundi yote kwa ujumla ndani ya Kata ya Wazo.”

 

Afisa Maendeleo wa Kata ya Wazo, Glory Chonjo amesema kuwa amekuwa akishirikiana kwa karibu na vijana wa kata hiyo katika kuchangamkia fursa zilizozopo kisheria na miongoni mwake ni hiyo ya asilimia 30 iliyotengwa kwenye manunuzi ya umma.

 

Hata hivyo Bi. Chonjo amesema kumekuwa na changamoto kwa vijana wenyewe kutokuwa na utayari wa kutafuta fursa hizo, badala yake wengi wao wanapenda kutafuniwa ili wao wameze tu.

 

“Sijui ni nini ila kuna kauvivu kwa vijana, unaweza kuitisha mikutano ya hadhara ili kuwapa elimu za fursa, wengi hawajitokezi ila ukiwaambia kuna elfu tanotano zinagawiwa, utawaona wengi wanakuja, lakini hawataki kupambania fursa endelevu.

 

“Kwa nafasi yangu na kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Kata, tunapambana kuhakikisha wanazifikia fursa zote zilizopo kisheria.”

 

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyakasangwe, Bi. Mabewa ameahidi kuwafikia vijana na makundi yote ili kuwapa ufahamu wa fursa hiyo iliyopo kwenye miradi inayogusa ununuzi wa umma.

 

“Nitawafikia vijana, Mtaa wangu una vijana wa kutosha tu na naishi nao vizuri, nitahakikisha sasa nawafikia ili kuwapa fursa hizo na kuwataka wazichangamkie.”

 

AFISA MANUNUZI WILAYA KINONDONI

Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Vumilia Tigwela amekiri kukosekana kwa uelewa wa fursa iliyopo kwenye manunuzi ya umma kwa vijana, hata hivyo ameahidi kuendelea kushirikiana na taasisi nyengine ndani ya wilaya hiyo kuhakikisha fursa inawafikia walengwa kila inapotokea mradi.

 

“Kulingana na tathmini mbalimbali ni kweli vijana hawachangamkii hii fursa, lakini naamini sababu kuu ni  ukosefu wa uelewa miongoni mwa vijana na pengine sisi wenye jukumu la kutoa elimu hatuifikishi ipasavyo, pamoja na jitihada zinazoendelea, ukweli ni kwamba naiona haja ya kuongeza kasi kwenye kuyafikia makundi nufaika.

 

 “Kutokuwepo kwa mafunzo maalum kwa vijana na makundi maalum, upungufu wa kampeni za kuelimisha kwa ngazi ya jamii na changamoto za kiufundi kwenye mfumo wa NeST ni changamoto, ila tutakabiliana nayo. Mimi matamanio yangu ni kuona fursa hii inawagusa wahusika moja kwa moja” amesema.

 

Bi. Vumilia amesema kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 KMC ilifanya manunuzi ya bilioni 50 kwenye miradi zaidi ya 300 na katika kiasi hicho cha fedha ni wastani wa shilingi bilioni mbili pekee ndio kimeyafikia makundi maalum.

 

Anasema pamoja na kukosekana kwa uelewa juu ya fursa hiyo, lakini pia vijana wengi hawana mitaji na hawajui namna ya kufanikisha kupata mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri.

 

BAADHI YA MASHARITI KWENYE SHERIA YAPUNGUZWE

Bi. Vumilia amesema sheria zinazotoa fursa hiyo ni nzuri, lakini zinapaswa kurekebishwa kwenye baadhi ya maeneo hasa eneo la kutaka wanufaika watoke eneo moja la mradi.

 

Amesema kwa maeneo ya mijini sheria hiyo inawanyima wigo vijana hasa ambao wako vyuoni kujiunga vikundi kwa sababu wanalazimika wote kuishi kwenye eneo moja.

 

“Binafsi yangu natamani vijana na makundi yote yanufaike na fursa hii iliyopo kwenye manunuzi, lakini shida iliyopo ni sheria kuweka taratibu ngumu kidogo zinazowezesha vijana kuungana hasa kwa maeneo ya mijini, hapa sheria ingelegezwa kidogo hasa kwa wakazi wa mijini, sheria iangalie sehemu waliyojisajili kisha maeneo wanayoishi yasingekuwa kigezo.

 

“Lakini pia naona kuna haja ya kuwa na utendaji wa moja kwa moja kati ya Ofisi ya Manunuzi Wilaya na ofisi ya Maendeleo ya Jamii, ili kurahisha mchakato wa kuwawezesha vijana na makundi mengine kupata mikopo na wakati huo huo kupata miradi ya maendeleo ndani ya Halmashauri.”

 

Ameongeza kuwa, ili suala hilo liwe endelevu kwa makundi yote hasa vijana, ni vema elimu ya fursa hiyo ikatolewa vyuoni kuanzia mwaka wa kwanza, hatua ambayo itawaondolea vijana fikra za kuajiriwa na kufikiria kujiajiri kwa kufanya kazi na serikali kupitia Manunuzi ya Umma.

 

Aidha Bi. Vumilia amesema vijana hawapaswi kuwa na fikra potofu kuwa miradi ya serikali haiwahusu na kwamba serikali ina watu maalum wa kufanya nao kazi.

 

“Miradi ya Serikali ni ya wananchi, vijana wajiunge na kujisajili kisha waje kuomba fursa, hata hivyo wanapaswa kujua kuwa si lazima waje na mawazo ya kutaka kuendesha miradi mikubwa, badala yake wanaweza kuomba zabuni za kusafisha barabara, kuzoa taka na kazi nyengine zisizohitaji mtaji mkubwa.”


 
PPRA YAZIOMBA HALMASHAURI KUTOA ELIMU

Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kupitia kwa Meneja wa Kanda ya Pwani, Bi. Vicky Mollel amekiri kuwepo kwa udhaifu wa utoaji wa elimu kwa jamii na kwamba wao wanafuatilia utolewaji wa elimu ya mfumo wa NeST kupitia Halmashauri zote.

 

“Sisi wenyewe PPRA tunatoa elimu kwenye Halmashauri mbalimbali, kwa kupitia Wakurugenzi na tunafuatilia kwa kuhudhuria semina hizo, ambazo Halmashauri zinawaalika wafanyabiashara na wajasiriamali wa eneo husika kuja kuhudhuria mafunzo hayo.

 

“Tunashirikiana na NGO’s, na Tanzania Chamber of Commerce katika utoaji wa elimu ya mfumo wa NeST na taratibu zake zikiwemo sheria. Mfano Desemba 19, 2025 tulitoa mafunzo hayo, ikiwemo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Hata ukiangalia katika mitandao yetu ya kijamii, ingia Instagram, Youtube utaona,

 

“Pia Januari 10, 2026 tulitoa elimu Katika mikoa minne ya Mbeya, Tabora, Mwanza na Dar es Salaam na Januari 26,2026 tulitoa mafunzo ndani ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani.” 

 


CHANGAMOTO ZILIZOPO

Bi. Vicky amesema miongoni mwa changamoto zilizopo ni kukosekana kwa muitikio na mahudhurio hafifu: Muitikio wakati mwingine unakuwa mdogo, wanaotakiwa kupata elimu hiyo hawajitokezi.

 

Changamoto nyengine ni kukosekana kwa ufuatiliaji, ambapo wahusika hawafuatilii na hata baadhi ya wanaopata elimu hiyo pia, hawafuatilii fursa hizo wala kuyachukulia mafunzo hayo kuwa ni fursa kwao. Wengi wao wanaweka dhana potofu kuwa kufanya kazi na serikali ni shida.

 

USHAURI WA PPRA KWA HALMASHAURI

Bi. Vicky amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo kunahitajika elimu ya kutosha na uhamasishaji zaidi katika maeneo yote, na kwamba Halmashauri zote zinapaswa kutoa elimu kwa kuzingatia fursa ya asilimia 30 kwa makundi maalum hususani.

 

“Halmashauri zinapaswa kuibua vikundi na kuvisajili baada ya kutoa elimu. Wanapotoa elimu ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi, watoe pia elimu ya fursa mbalimbali ikiwemo ya mfumo wa NeST

 

“Vijana wanatakiwa waelimishwe zaidi kuwa, wanaposajili vikundi, waangalie ni biashara gani wanaweza wakafanya na serikali. Waangalie katika taasisi za serikali kuna uhitaji gani au ni vitu/huduma gani serikali inanunua kutoka kwa wananchi, ili nao waweze kujisajili kwa kusudi la kupata fursa za zabuni kupitia ununuzi wa umma. 

 

“Ikiwa kikundi cha vijana kimejisajili katika biashara ambayo serikali hainunui hususani kwa kupitia mfumo, lazima fursa hiyo itawapita.”amesema.

 


TARURA KINONDONI: FURSA BADO ZIPO

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Kinondoni, Mhandisi Edwin Kabwoto anasema bado vijana wa Kata ya Wazo wanayo nafasi ya kufanyakazi kwenye miradi inayosimamiwa na TARURA ikiwa ni pamoja na ulinzi wa vifaa vya miradi, miundombinu na usafi wa barabara.

 

“Nafasi bado wanayo vijana, sisi tuna miradi mara kwa mara na mengine inaendelea, kama wanakidhi vigezo na wamepatiwa zabuni, sisi tutafanya nao kazi wakati wowote.

 

“Kimsingi tunashirikisha jamii kwa ngazi zote ikiwemo ngazi ya sasa ya ujenzi na hata baada ya ujenzi. Sisi ni chombo cha serikali na tunatekeleza matakwa ya serikali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.”

 

MKURUGENZI PPRA ATAKA SHERIA ITEKELEZWE

Mkuu wa PPRA nchini, Dennis Simba ametaka mamlaka husika kuhakikisha zinatekeleza sheria ili kuyawezesha makundi maalum na kwamba kutokufanya hivyo ni kosa la jinai kama sheria inavyoeleza.

 

Akiwa katika ziara yake kwenye Mamlaka ya Maji mkoani Tanga, Desemba 15,2025 alisisitiza kuwa kutotekelezwa kwa shariti linayohusu upendeleo wa manunuzi ya umma ikiwemo upendeleo wa asilimia 30 ni kosa la jinai.

 

“Kwenye kifungu cha sheria cha 128 (2d) kutotekeleza mashariti ya sheria jii ikiwemo yanayohusu upendeleo wa makundi maalum ni kosa la jinai na hiyo ni kwa mujibu wa sheria ya ununuzi wa umma.

 

“Sheria inatuambia kwa mujibu wa kifungu tajwa mtu anaekiuka shariti tajwa atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi milioni 10 au kifungo cha kipindi kisichozidi miaka mitatu, hili ni suala la kisheria kabisa na ndio maana sisi mamlaka katika kampeni zetu tunazungumza vijana, wanawake, wazee na walemavu.”

 

SERA YA TAIFA YA MAENDELEO YA VIJANA

Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya maendeleo ya vijana na Mkakati wa Kukuza Uchumi Jumuishi, serikali ina wajibu wa kuweka mifumo inayowezesha vijana na makundi maalum kunufaika na fursa za kiuchumi ikiwemo ununuzi wa umma.

 

Aidha Sheria na kanuni za ununuzi wa umma zinaelekeza kuwa taasisi za umma mbali na kutenga zabuni kwa makundi maalum, lakini pia zinatakiwa kuhakikisha kunakuwa namazingira wezeshi ili makundi hayo yaweze kushiriki kikamilifu.

 

 KENYA NA RWANDA ZIMEFANIKIWA

Ipo mifano hai ambayo Tanzania inaweza kuiiga kutoka nchi za Kenya na Rwanda ambako inaonesha kuwa pale ambapo elimu ya manunuzi jumuishi imepelekwa moja kwa moja kwa walengwa kupitia ngazi za jamii, ushiriki wa makundi maalum umeongezeka na athari chanya za kiuchumi hzimeonekana kwa haraka.  

 

 

 

Post a Comment

0 Comments