Ticker

7/recent/ticker-posts

UCHIMBAJI HOLELA WA MCHANGA WATANUA KINGO ZA MITO



NA JIMMY KIANGO
Uchimbaji mchanga katika mito ya wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam umeendelea kuwa tatizo sugu linaloathiri moja kwa moja maisha ya wananchi na usalama wa makazi yao. Uchimbaji huo ambao mara nyingi hufanywa bila uangalizi wa kitaalamu wala kufuata taratibu za kisheria, umechangia kubadilisha mikondo ya maji na kuharibu kingo za mito.


Matokeo ya vitendo hivi ni vilio kwa wananchi kwa kuwa husababisha hasara ya mali ikiwemo kubomoa makazi yao. Makumi ya wananchi wanaoishi katika Kata za Kunduchi hasa Tegeta Msufini, Kinondoni, Dar es Salaam wamepoteza makazi na mali kutokana na mafuriko ya mwaka 2024.


Mafuriko ya mwaka 2024, yaliyotokana na mvua kubwa na kusababisha hasara ikiwemo vifo, uharibifu wa makazi, mali na miundombinu ya jamii. Nyumba nyingi, hasa maeneo ya Tegeta kwa Ndevu na Jangwani, ziliharibiwa au kusombwa na maji, huku zaidi ya nyumba 40 zilibomolewa na mafuriko, na nyingine zilibaki katika hatari ya kuanguka.

 

Hatari hii kw kiasi kikubwa ilichangiwa na uwepo wa shughuli mbalimbali za kibinadamu kama uchimbaji mchanga katika mito na mabonde kinyume cha sheria. Wakati mafuriko ya mwaka 2024 yakibaki kuwa historia, nyumba zaidi ya 40 katika maeneo ya Nyakasangwe Kata ya Wazo, Tegeta Msufini Kata ya Kunduchi nazo zipo hatarini kusombwa na maji wakati wowote iwapo hatua za makusudi za kulinda mito, hazitachukuliwa.

Mmoja wa wakazi wa Tegeta Msufini aliyejitambulisha kwa jina la Victoria Aume alisema, nyumba yake ya vyumba sita ilibomolewa na mvua za mwaka 2024 kutokana na maji kuacha mkondo wa mto.

“Nilipoteza nyumba na vitu vyote vilivyokuwemo ndani vikiwemo vya wapangaji wangu, nimebaki sina mbele wala nyuma, maana nyumba ilikuwa inanisaidia kupata kipato kutokana na kodi inayolipwa na wapangaji, sasa zina kitu,” alisema.

Kwa mujibu wa Mpango wa dharura wa mafuriko wa mkoa wa Dar es Salaam, uliotayarishwa mwaka 2021, unayataja Matukio ya mafuriko ndiyo yanaongoza katika orodha ya Majanga yanayotokea mara kwa mara katika Mkoa wa Dar es Salaamu. 

 

Mafuriko yanapotokea yamekuwa yakisababisha uharibifu mkubwa na kuathiri maisha ya watu na mali zao.

Hatari kama hiyo inaweza pia kuwakuta wakazi wa mtaa wa Nyakasangwe wanaoishi jirani na mto Nyakasangwe  na mto unaotambulika kama Mto msigani ambao unapita kwenye daraja la kwa Kipira, katika eneo la Msigani, Mtaa wa Nyakasangwe, Kata ya Wazo, wilaya ya Kinondoni.


Hali hiyo inatokana na kingo za mito hiyo kutanuka katika kila msimu wa mvua kutokana na kuwepo kwa mwendelezo wa shughuli za kibinadamu hasa uchimbaji wa mchanga ndani ya mito.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 57 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na marekebisho yake ya mwaka 2025, inakataza kufanyika kwa shughuli yoyote ya kibinadamu ya kudumu ambayo kwa asili yake inaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira na utunzaji wa bahari au kingo za mto, bwawa, au miambao ya asili ya ziwa ndani ya mita 60.


Kwa upande wake Mwongozo wa Usafishaji Mchanga, Tope na Taka ngumu kwenye mito na Mabonde mkoa wa Dar es Salaam wa mwaka 2021unazitaka mamlaka kusimamia uchimbaji wa mchanga.

Afisa Madini wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni anayeshughulikia masuala ya mchanga, Awadhi Jambo, amekiri uwepo wa uchimbaji haramu wa mchanga, na kueleza kuwa halmashauri inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inakabiliana na jambo hilo.


Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kwa nyakati tofauti walisema maisha yao yako hatarini hasa nyakati za mvua, huku wakiwataja watu wanaochimba mchanga katika mito ndiyo wanaosababisha hatari hiyo kwa kiasi kikubwa.

Mkazi wa Nyakasangwe, David Malunde amesema, uchimbaji wa mchanga unatishia usalama wa nyumba yake ambayo imeambatana na mto uliopita kwenye daraja la kwa Kipira.

Kwa upande wake mkazi wa eneo la  Kipira aliyejitambulisha kwa jina la Mama Salha, alisema amelazimika kuhama kwenye nyumba yake kutokana na sehemu ya nyumba hiyo kusombwa na maji wakati wa mafuriko ya mwaka 2024.

“Nimelazimika kuhama kwenye nyumba yangu niliyoijenga kwa gharama kubwa kwa sababu ya mafuriko, naamini hali hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na kufanyiuka kwa shughuli za kibinadamu zisizoruhusiwa kwenye maeneo ya mito,” amesema.

Akizungumzia suala hilo Mjumbe wa Shina Na. 05 katika eneo hilo, Nasibu Kabeya, amesema uchimbaji huo ulianza takribani miaka mitatu  iliyopita na kwamba jitihada za kuwazuia wachimbaji zimekwama kwa sababu wanafanya shughuli hizo kwa kujificha, huku wakiutumia usiku mwingi kufanikisha shughuli hiyo.


Kwa upande wake Mjumbe wa Shina Na. 11 katika eneo la Tegeta Msufini, Modest Francis, alisema uchimbaji mchanga katika mito ulianza takribani miaka 10 iliyopita na kwamba jitihada za kuwazuia wachimbaji zimekwama.


Alisema kwa siku, malori ya mchanga kati ya matano hadi 10 yanaingia eneo hilo kubeba mchanga, hali inayotishia makazi ya wakazi wa Msufini.

“Kwa upande wangu zimeathirika nyumba 35, ikiwamo yangu mwenyewe. Tunaiomba serikali itusaidie kwa sababu hapa kuna wananchi wengi ambao hawana eneo mbadala,” alisema.

Alisema ili kuzuia mmomonyoko, wakazi wa eneo hilo wameamua kutupa taka kama njia ya kunusuru nyumba zilizosalia.


“Tumejaribu kutupa taka lakini hazifui dafu, zaidi tunaona ni uchafuzi wa mazingira, hivyo tunaomba msaada kwa serikali yetu na mbunge wetu,” alisema. Mjumbe wa Shina Na. 10, Edward Sungura, alisema uchimbaji huo unasababisha uharibifu wa mazingira na kuna hatari ya kuharibu pia miundombinu.


“Kwenye shina langu zimeathirika nyumba 13 pamoja na mimi mwenyewe kwani vyumba vinne vya wapangaji vimeanguka hivyo nipo hatarini kufukuzwa na adha hii na sijui nitaelekea wapi,” alisema. Alisema vijana wanaoingiza malori ya kubeba mchanga katika eneo hilo, hawazuiliki kwa madai kuwa ni wakorofi na kila wakielezwa uharibifu wanaousababisha huishia kuwatukana wananchi.


Zainabu Barinyandi a,mbae ni mkazi wa eneo hilo, alisema athari za uchimbaji huo zimevunja nyumba yake ya vyumba vinne na kulazimika kwenda kuhifadhiwa kwa rafiki yake tangu mwaka jana. Wataalamu wa mazingira wanasema kuwa uchimbaji mchanga holela hasa katika mito unachangia kupungua kwa kina cha mito, kuziba njia za maji, na kuongeza kasi ya mmomonyoko wa ardhi. Hali hii si tu inahatarisha maisha ya watu, bali pia inaharibu miundombinu ya jamii na kuathiri uchumi wa kaya zinazopoteza makazi na mali zao.


 




Post a Comment

0 Comments