Ticker

7/recent/ticker-posts

UCHIMBAJI MCHANGA KINONDONI NI JANGA

 



NA JIMMY KIANGO

KILA mvua kubwa zinaponyesha, maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, wanapoteza furaha na kutawaliwa na hofu, sababu kubwa ya kukumbwa na hali hiyo ikiwa ni kuifikiria hatari inayokuja mbele yao.

 

Uhalifu wa kimazingira unaofanywa mbele ya macho yao na macho ya mamlaka, unawafanya kuyakimbia makazi yao kwa muda. 

 

Uchimbaji haramu wa mchanga katika mito ya wilaya hiyo umekuwa donda sugu, kingo za mito zinaharibika na kusababisha kubadili uelekeo wa maji, jambo ambalo ni sawa na kuandaa mazingira ya mafuriko yanayoweza kusababisha maafa makubwa ikiwemo vifo.

 

Kinachoshangaza ni kwamba, pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kukiri waziwazi kufahamu tishio hili, na kuahidi kuchukua hatua, kila siku iendayo kwa Mungu, mito iliyopo wilayani humo inangaamia kutokana na biashara haramu ya uchimbaji mchanga kwa ajili ya shughuli za ujenzi.

 

Ukipita katika baadhi ya maeneo kama vilke  Kawe, Wazo, Goba, Nyakasangwe, Mwenge na Tegeta ya wilaya ya Kinondoni, utashuhudia marundo ya mchanga uliochimbwa katika mito yakiwa pembeni ya barabara yakisubiri wateja.

 

Wahusika wa biashara hiyo wanayaita maeneo yanayouza mchanga kuwa ni migodi ya nchi kavu, ambapo kuanzia alfajiri hadi usiku biashara hiyo hufanya bila kizuizi wala hofu yoyote.

 

Kwa mujibu wa Rehema Ayo mkazi wa Nyakasangwe Kata ya Wazo, wilaya ya Kinondoni, mamia ya vijana wamejiajiri kwa kazi ya kuchimba mchanga katika mito na kusababisha madhara hasa wakati wa mvua, ikiwemo mito kubadilisha uelekeo wake na kwenda katika makazi ya watu hivyo kusabababisha mafuriko.

 

Anasema viongozi kuanzia ngazi ya mtaa hadi wilaya wanaijua biashara hiyo, hata hivyo hakuna jitihada za makusudi zinazofanyika ili kukabiliana nayo.

 

Rehema anabainisha kuwa, kuna uwezekano wa viongozi wa mitaa kuzidiwa nguvu na makundi ya wachimbaji mchanga au nao kuwa sehemu ya biashara hiyo, hivyo kushindwa kuchukua hatua.

 

Mjumbe wa mtaa  wa Kwamangitu, Ashura Mbaruku anasema wamejitahidi kuwazuia wachimbaji, lakini vijana wanaochimba mchanga ni wakorofi.

 

“Kuna siku alyekuwa Mwenyekiti wa mtaa wetu wa Nyakasangwe ndugu Mwandege, alienda kuwazuia lakini hawakumsikiliza sijui kiburi hiki wanakitoa wapi,” alihoji.

 

Alisema kuwa, wao waliwahi kutaka kupigwa na wachimbaji hao ambao pia walipiga marufuku wanawake kwenda kuwafuatilia.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakasangwe, Zuhura Mabewa anakiri uwepo wa shughuli hiyo na kwamba yuko katika mchakato wa kukutana na wachimbaji ili kuwaondoa kwa amani.

 

Alisema kwa mfano katika eneo la mto Nyakasangwe pekee kuna watu kati ya 100 hadi 200, wengi wao wakiwa vijana wanaochimba mchanga kazi ambayo hufanywa mchana na usiku.

 

Mmoja wa wachimba mchango katika eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Ally Kidulo alisema anafahamu kwamba wanachofanya ni kinyume na sheria, lakini wao wanafanya hivyo ili kusafisha mazinjgira ya mto.

 

Kwa upande wake Ramadhani Mgala mchimbaji mchanga katika mto Nyakasangwe, haamini kama uchimbaji mchanga katika mito unasababisha madhara ikiwemo mafuriko badala yake anaamini kukosekana kwa miundombinu ya kusafirisha maji ya mvua ndiyo sababu ya mafuriko.

 

Kifungu cha 57 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na marekebisho yake ya mwaka 2025 inakataza kufanyika kwa shughuli yoyote ya kibinadamu ya kudumu ambayo kwa asili yake inaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira na utunzaji wa bahari au kingo za mto, bwawa, au miambao ya asili ya ziwa ndani ya mita 60.

Mbali na hayo Mwongozo wa Usafishaji Mchanga, Tope na Taka ngumu kwenye mito na Mabonde mkoa wa Dar es Salaam wa mwaka 2021 unazitaka mamlaka kusimamia uchimbaji wa mchanga, hata hivyo katika wilaya ya Kinondoni bado shughuli hizo zinaendeshwa kiholela na kinyume cha taratibu.


KAULI YA WATAALAMU

Watalaamu wa mazingira wanaeleza kuwa uchimbaji mchanga katika maeneo ya mabondeni, mito na vijito husababisha kupoteza asili yake jambo linalofanya baadhi ya mito ihame mara kwa mara hasa wakati wa mvua.

 

Mshauri wa mradi wa kuwezesha vijana kujiajiri unaojulikana kama Opportunities for Youth Employment (OYE) ambao pia unaangazia utunzaji wa mazingira, John Chinguku anaeleza kuwa uchimbaji mchanga unaharibu kingo za mito na uelekeo wa mto.

 

“Shughuli hii si salama kwa mazingira, inachangia mmomonyoko wa kingo za mito na kuharibu muundo asilia wa mito na kuifanya iwe na kona kona nyingi, au kupoteza uelekeo wake,” alisema.

 

Chinguku aliongeza kluwa, “Kuwepo kwa kona kona kunasababisha mito wakati mwingine kuhama na kuelekea katika makazi ya watu au kingo kushindwa kuhimili wingi wa maji”.

 

Alifafanua kuwa, uchimbaji mchanga katika mito au kingo za mito unaharibu ardhi oevu na vichaka vya asili hivyo kuathiri bayoanuai na unaongeza athari za mafuriko kwa kuwa maeneo hayo husaidia kupunguza kasi ya maji yanapokuwa mengi na kupunguza madhara kwa wakazi wa maeneo husika.

 

TAKWIMU ZA UCHIMBAJI MCHANGA 

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Kamati ya Wataalamu iliyoundwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Februari 2019, jumla ya mita za ujazo milioni 6.7 za mchanga huchimbwa kila mwaka katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

 

Kiasi hiki cha mchanga ni sawa na wastani wa tani milioni 10 kwa mwaka na kikiwekwa katika muktadha wa usafirishaji, inamaanisha kuwa takribani malori milioni moja (kwa kutumia lori moja linalobeba wastani wa tani 10) yanatoka katika maeneo hayo kwa mwaka mmoja, jambo ambalo ni sawa na wastani wa malori 2,782 kwa siku.

 

MATUMIZI YA ARDHI 

Shughuli haramu ya uchimbaji mchanga inafanyika katika maeneo oevu, ambayo ni sehemu ndogo ya ardhi iliyopo mkoani Dar es Salaam, huku Wilaya ya Kinondoni ikiwa mojawapo ya maeneo yanayoathirika zaidi.

 

Takwimu za matumizi ya ardhi, zilizotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mei, 2017, zinaonyesha kuwa maeneo oevu (yanayojumuisha mabonde, vijito na mito) ni hekta milioni 4.59, sawa na asilimia 2.8 ya ardhi yote yam koa huo.

 

Takwimu hizo, zilizorejea Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa mwaka 2012, zinabainisha kuwa, kati ya eneo lote la Dar es Salaam ambalo ni hekta milioni 161.8, Jiji hilo lina hekta 319,416 pekee zilizotengwa kwa ajili ya kilimo mjini na hekta 516,273 kwa ajili ya shughuli za machimbo.

 

Hata hivyo, kuna kila dalili kuwa iwapo mamlaka husika hazitachukua hatua za haraka, mabonde ya mito ya Dar es Salaam yataharibiwa zaidi kutokana na ongezeko la watu na pia kuwa kitovu cha biashara.

 

Kulingana na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Dar es Salaam inakua kwa kasi huku ikikadiriwa kuwa hadi kufikia Desemba 2022, mkoa huo ulikuwa na watu milioni 5.3, ikilinganishwa na watu milioni 4.3 mwaka 2012, idadi ambayo ni asilimia 11 ya watu wote nchini.

 

Pamoja na ongezeko la watu, Dar es Salaam ndiyo kitovu kikuu cha biashara nchini, hivyo kuvutia shughuli za ujenzi kwa ajili ya biashara na makazi. Hili linasababisha mahitaji ya mchanga kuongezeka sana, hivyo kuwashinikiza wachimbaji haramu kuvamia maeneo oevu.

 

KAULI ZA VIONGOZI

Afisa Madini wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni anayeshughulikia masuala ya mchanga, Awadhi Jambo, amekiri uwepo wa uchimbaji haramu wa mchanga, hata hivyo amebainisha kuwa Halmashauri inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inakabiliana na jambo hilo.

 

“Ni suala ambalo tunalijua, jitihada za kukabiliana nalo zinaendelea kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali,” amesema Jambo.

 

Kwa upande wake Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linasema kuwa linafahamu uwepo wa tatizo hilo na kwamba limekuwa likishirikiana na halmashauri za jiji la Dar es Salaam kulitokomeza.

 

Mratibu wa Kanda ya Mashariki wa NEMC, Jafar Chemgege anasema sheria inakataza shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 ya vyanzo vya maji ikiwemo mabonde ya mito na maofisa wa mazingira wa ngazi zote nchini wanajua wajibu wao wa kuisimamia na kutoa elimu kwa wananchi kukabiliana na uharibifu huo.

 

Chemgege anasema licha ya kuwa usimamizi katika maeneo unatakiwa ufanywe kwa kiasi kikubwa na Halmashauri, NEMC bado huwa inafanya operesheni za kukamata wanaojihusisha na uchimbaji mchanga haramu na kukamata malori yote yanayotumika kuubeba.

 

“Kwa bahati mbaya baadhi ya shughuli za usafirishaji mchanga huo zinafanywa usiku lakini tukiwakamata tunawatoza faini inayoanzia 50,000 na kuendelea kulingana na kosa na wengine wanapelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.”

MITO NA MABONDE YALINDWE KWA VITENDO SIO MANENO

Mito na mabonde ya Kinondoni si mali ya wachimbaji haramu, bali ni urithi wa vizazi vya sasa na vijavyo. Hivyo, uwajibikaji wa viongozi haupaswi kuwa maneno matupu bali vitendo vinavyolinda maisha na mali za wananchi. 

Ikiwa hatua hazitachukuliwa sasa, Dar es Salaam inaweza kuamka siku moja ikajikuta imekumbwa na mafuriko makubwa ambayo yangeweza kuepukika.

 

 

Post a Comment

0 Comments