Ticker

7/recent/ticker-posts

MABILIONI YA COP30, TANZANIA YAPEWA KIPAUMBELE KUWA WA KWANZA KUPOKEA RUZUKU

  

Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) Dkt. Richard Muyungi,(Picha kwa hisani ya mitandao) 

NA. JIMMY KIANGO

Baada ya Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaofanyika kwenye jiji la Belem nchini Brazili, kuzindua mpango wa kuwasilisha mapendekezo ya kupata msaada wa kifedha kutoka kwenye Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu (FRLD) kwa nchi zinazoendelea, Tanzania imepewa kipaumbele cha kuwa nchi ya kwanza kupata fedha hizo.


Mfuko wa FRLD ulianzishwa rasmi mwaka 2022 kwenye mkutano wa COP27, uliofanyika nchini Misri, tangu kuanzishwa kwake haukuwahi kukaribisha mapendekezo kama ilivyofanya sasa, ambapo kiasi cha dola milioni 250 za Marekani (takriban shilingi bilioni 625) kimetengwa, huku kila mradi ukitengewa kiasi cha dola milioni 20.


Hii inamaanisha kuwa endapo Tanzania itafanikiwa kuandaa mradi utakaokidhi matakwa ya FRLD ya kupewa fedha hizo ambazo si mkopo bali ni ruzuku, itapokea kiasi cha dola milioini 20 (takribani shilingi bilioni 48).


Ruzuku hiyo ambayo inatarajiwa kutolewa mwaka 2026,itaelekezwa kwenye miradi mbalimbali inayogusa makundi tofauti tofauti ya wananchi yaliyoathiriwa na mabadiliko tabia nchi kulingana na shughuli zao, iwe uvuvi, kilimo na nyengine zinazohusiana na mazingira.


Akizungumzia uamuzi huo nchini Brazili, Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) Dkt. Richard Muyungi amesema, kazi kubwa iliyofanywa na Tanzania katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko tabianchi Tanzania inatarajia kuwa nchi ya kwanza kupata ruzuku hiyo.

 

“Kusema ukweli kwa kazi tuliyoifanya mwaka huu na Mkuu wa huu mfuko ameliona hilo, kipaumbele tumepewa Tanzania.”

 

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa COP30,Brazili.
Katika mkutano wake na Watanzania walioshiriki kwenye mkutano huo unaoendelea nchini Brazili Dkt.Muyungi pia alieleza mambo mbalimbali muhimu ikiwa ni pamoja na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na mabadiliko tabianchi.

 

“Hadi sasa kuna mambo yamejitokeza na nataka tuyafuatilie, tukiwa katika Uenyekiti wetu tumezindua awamu ya utekelezaji wa mfuko wa ‘loss and demage’, awamu hii tumeizindua siku tatu zilizopita na nchi sasa zitaanza kupata fedha, sio nyingi ni hadi dola milioni 20 kwa mradi mmoja.

 

“Na natamani tuwe wa kwanza kwa sababu hili jambo limezinduliwa chini ya Uenyekiti wetu, tuwe nchi ya kwanza kupata hizi fedha, nawaomba sana, ili kufanikisha hili kinachohitajika ni kuwa na mtu maalum atakaelisimamia hili, Mheshimiwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais mtusaidie kutupatia mtu mmoja tu anaeitwa ‘focol point’ wa ‘loss and demage fund’.

 

“Akishakuwepo na kusema kweli kwa kazi tuliyoifanya mwaka huu na Mkuu wa hii ‘Fund’ kipaumbele tumepewa Tanzania, na ningeomba sana hii iwe ni fursa, tukitoka hapa tuwe na mradi mmoja au miwili na miradi inapitia kwenye taasisi zilizokuwa ‘acredited’ na tuna benki ya CRDB na niseme kwa mara ya kwanza hizi fedha ni ‘grant’ sio mkopo, zimetengwa dola milioni 250 ambazo nchi zinaweza kutumia kuanzia mwaka ujao,lakini bado tunashinikiza nchi ziweke fedha nyingi hadi kufikia angalau dola bilioni moja ya kuanzia.

 

“Tunayo mifuko ambayo inafanya kazi tayari, nimeomba watu wetu wa NEMC (Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira) wafuatilie kwa karibu mfuko wetu wa ‘adaptation’ ambao tayari walikuwa na changamoto ya ‘reactation’, nimeogea na wahusika wako tayari kufungua njia ili twende na hilo.

 


TANZANIA KUWA KITUO CHA AFRIKA- SANTIAGO NETWERK

 Pamoja na Tanzania kuwa na nafasi kubwa ya nchi ya kwanza kupokea ruzuku hiyo, lakini pia Dkt. Muyungi amesema kuwa pia nchi imeteuliwa kuwa Kituo cha Afrika kwa ajili ya miradi ya Usaidizi katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.

 

“… lakini kubwa zaidi niliwafahamisha kabla kuwa mwaka huu Tanzania imeteuliwa kuwa kituo cha (santiago netwerk) kituo cha Afrika kwa ajili ya miradi na usaidizi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi (Santiago Network Loss and Demage).

 

“Jana tulikuwa na kikao na Mkuu wa Taasisi hii ambayo iko Geneva, bahati nzuri wamekamilisha masuala yote ya ajira na Tanzania ndio kituo na sisi kama Serikali tumeshawapa ofisi katika jengo la Umoja wa Mataifa (UN) na wameshukuru sana na wako tayari kufanya uzinduzi na tayari kuna fedha ndogo ndogo zitaanza kutolewa.”


Uamuazi huo ni hatua muhimu kwa mataifa yanayokabiliana na kupanda kwa kina cha bahari, ukame, mafuriko na madhara mengine yaliyosababishwa na mabadiliko tabianchi.


Tanzania ni miongoni mwa nchi waathirika wakubwa wa mabadiliko tabianchi, na athari zake zinaonekana wazi wazi hasa kwenye eneo la bahari na pwani, ambapo kiwango cha uvuaji wa samaki kimepungua, joto limeongezeka na kina cha bahari kimepanda, huku moja ya sababu ikitajwa kuwa ni kukithiri kwa taka ngumu ndani na nje ya bahari.

Post a Comment

0 Comments