Ticker

7/recent/ticker-posts

KUELEKEA MIAKA 20 YA UDHIBITI WA HUDUMA ZA NISHATI NA MAJI, EWURA YAAHIDI HUDUMA BORA ZAIDI

Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Lorivii Long’idu, akifungua warsha ya tathmini ya kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya EWURA.

NA. JIMMY KIANGO

Ikiwa katika safarai yake ya kutimiza miaka 20 ya huduma kwa Watanzania, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeahidi kuendelea kuboresha huduma zake zaidi ili kuhakikisha watoa huduma ya Nishati na Maji wanatoa huduma bora. 


Hayo yamesemwa na Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Lorivii Long'idu Februari 27,2026 alipofungua warsha ya siku moja ya tathmini ya kuwajengea uwezo Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusu majukumu ya taasisi hiyo.


Lengo la warsha hiyo lilikuwa ni kuimarisha uelewa wa Wanahabari hao juu ya  majukumu, mipaka ya kisheria na utendaji wa mamlaka hiyo katika sekta za Nishati na Maji nchini.

 

"Tangu tuanze kutoa huduma ya udhibiti kwenye eneo la Nishati na Maji, mambo yamekuwa mazuri, hakuna ukataji wa maji au umeme usio na sababu, lakini hata bei sasa zimekuwa na usawa tofauti na ilivyokuwa kabla na tunawaahidi Watanzania EWURA itasimama kidete kuhakikisha taasisi tunazozidhibiti zinafanya kazi inayotakiwa,"amesema.


 Long’idu, ambae alifungua warsha hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuelimisha umma kuhusu majukumu ya EWURA, ikiwemo udhibiti wa bei, utoaji leseni, na usimamizi wa ubora wa huduma za nishati na maji.

 

Amesema kuwa kuwajengea uwezo waandishi ni sehemu ya mkakati wa EWURA wa kuhakikisha taarifa zinazotolewa kwa umma zina usahihi, uwiano na zinaakisi hali halisi ya majukumu ya mamlaka hiyo. “Mnapoelewa vizuri tunachokisimamia, mnakuwa daraja sahihi kati ya EWURA na wananchi,” amesisitiza.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema warsha hiyo ni muendelezo wa ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo mbili, akibainisha kuwa mafunzo yaliyopita yalizaa matunda ambapo jumla ya habari 103 zilichapishwa zikihusu shughuli za EWURA.

 

Ameongeza kuwa lengo la warsha za tathmini ni kuibua waandishi mahiri (“champions”) watakaoweza kuandika kwa weledi, kuzingatia maadili ya taaluma na kusaidia kujenga uwajibikaji katika sekta ya nishati na maji.

 

Soko ametoa wito kwa waandishi kuendelea kuandika kwa weledi, kufanya uchambuzi wa kina na kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi zinazochochea uwazi, uwajibikaji na maendeleo endelevu ya Taifa.

 

Post a Comment

0 Comments