NA MWANDISHI WETU
Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imesisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kukataa taarifa zake kutumika kwenye matangazo ya biashara bila idhini yake.
Aidha, ipo taratibu maalum ya kuwasilisha malalamiko kwa Tume endapo taarifa za mtu zitatumiwa kinyume cha sheria, ambapo hatua za kisheria huchukuliwa dhidi ya wahusika.
Hayo yamesemwa Machi 1, 2025, na Wakili Humphrey Mtuy wakati akiwasilisha mada kuhusu Sheria za Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini katika warsha iliyofanyika mjini Morogoro.
Mtuy amebainisha kuwa ni kosa kisheria kutumia picha au taarifa za mtu kwenye matangazo ya biashara bila ridhaa yake. Pia, waajiri wanapaswa kumjulisha muombaji wa kazi endapo taarifa zake zitachakatwa na mifumo maalum ya kuhifadhi au kuchambua data, na iwapo taarifa hizo zitavuja, muhusika ana haki ya kuwasilisha malalamiko.
Haki za kimsingi za mtu kuhusu taarifa binafsi
Mtuy ameeleza kuwa kila mtu ana haki ya:
Kufuta au kuharibu taarifa zake – Mtu anaweza kuomba taarifa zake ziondolewe kwenye kumbukumbu za taasisi yoyote, haki inayojulikana kama Right to be Forgotten.
Kujulishwa madhumuni ya ukusanyaji wa taarifa, taasisi zinapaswa kueleza kwanini zinakusanya na kuchakata taarifa binafsi za mtu.
Kuzuia matumizi ya taarifa binafsi endapo yanaweza kusababisha madhara ikiwa ukusanyaji wa taarifa unaweza kumdhuru mtu, ana haki ya kuzuia matumizi yake.
Hata hivyo, Mtuy ameeleza kuwa kuna mazingira fulani ambapo taarifa binafsi zinaweza kufikiwa bila idhini ya mhusika.
Ikiwa kuna sheria inayoruhusu upatikanaji wa taarifa hizo.
Kama inahitajika kulinda maslahi ya taifa.
Endapo kuna amri ya mahakama kusaidia uchunguzi wa uhalifu au matumizi mabaya ya fedha.
Kwa viongozi wa umma, ambapo upekuzi wa taarifa hufanyika kabla ya uteuzi wao.
Usafirishaji wa taarifa nje ya nchi
Kwa mtu anayehitaji kusafirisha taarifa binafsi nje ya nchi, lazima apate kibali kutoka PDPC kwa kutumia Fomu Namba 7. Kibali hiki kinaweza kukataliwa ikiwa kuna sababu za msingi za kisheria.
Utaratibu wa kuwasilisha malalamiko
Mtu yeyote anayehisi haki zake zimevunjwa anaweza kuwasilisha malalamiko kwa Tume kupitia:
Kujaza fomu maalum inayopatikana mtandaoni.
Kuandika barua rasmi au kutuma barua pepe kwa Tume.
Mlalamikiwa anapewa siku 21 kujibu malalamiko hayo. Kulingana na Kanuni ya 13 ya uchunguzi wa malalamiko, Tume hufanya uchunguzi ndani ya siku 30 na kutoa nafasi ya kusuluhisha mgogoro huo.
Iwapo suluhisho halitapatikana, Tume huunda kamati maalum yenye wataalamu watatu mmoja wa masuala ya taarifa binafsi, mtaalamu wa TEHAMA, na mwanasheria kwa mujibu wa Kanuni ya 14.
Baada ya kusikiliza malalamiko, kamati inaweza kutoa adhabu au faini kulingana na uzito wa kosa. Ikiwa mlalamikiwa hakulenga kuharibu jina la mtu, Tume inaweza kuamuru marekebisho badala ya adhabu.
Mtuy amehitimisha kwa kusema kuwa endapo mhusika hataridhika na maamuzi ya Tume, ana haki ya kukata rufaa katika Mahakama Kuu. Pia, mahakama inaweza kuamuru fidia au gharama za shauri kulipwa kwa mlalamikaji.
0 Comments