Ticker

7/recent/ticker-posts

MA MC NI MARUFUKU KUSAMBAZA PICHA NA VIDEO ZA WATU KWENYE MITANDAO YA KIJAMII

 


 

NA MWANDISHI WETU

 

TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), imesema washereheshaji wanaosambaza picha za washiriki wa sherehe mbalimbali wanapaswa kuwa makini kwa kuwa wanavunja sheria kwa kuwa hawajapata idhini ya mtu kusambaza picha zake akiwa anacheza au jambo lolote.

 

 

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia, ameyasema hayo Machi 1,mwaka huu mjini Morogoro wakati wa warsha na wahariri wa vyombo mbalimbali nchini kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi.

 

Amesema maisha ni mchezo wa kuigiza, hivyo kuna maisha mtu anapenda yaonekane na mengine ni siri lakini baadhi ya watu bila kujua wanasamabza taarifa za watu jambo ambalo ni kosa kisheria.

 

“Unakuta umeenda kwenye sherehe wale MC wanakupiga picha mnato au video baadaye unaonekana mtandaoni ukiwa umejiachia, ni muhimu kupata ridhaa ya mtu kabla ya kutumia taarifa zake kama majina, picha, namba za simu, makazi, anuani,taarifa za kifedha na afya.

 

Amesema kila binadamu ana faragha yake, hivyo ni muhimu kulinda haki za kila mmoja kwa kuwa ni haki za kibinadamu, hakuna anayependa kuona taarifa za kifedha au kiafya ziko kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii bila ridhaa yake.

 

“Linatuhusu sote na linawahusu Watanzania, hatuwezi kulikwepa teknolojia ipo kwa ajili ya kuturahisishia kufanya kazi, taarifa za msingi utu, hakuna ambaye angependa taarifa zake, siri zake ziandikwe au kusambazwa kila mahali,”amesema.

 

“Sheria inawataka wanaotakiwa kuhudumiwa walinde taarifa binafsi na kwamba lazima muhusika aridhie kutumika kwa taarifa hizo. Taarifa zinagusa maisha ya kila mtu, Ibara ya 16 (1&2) imetamka kila Mtanzania anastahili kuwa na faragha jambo ambalo linalinda ubinadamu wetu,”amesema.

 

Amesema tekonolojia imekuwa na kwamba mtu anaweza kufanya jambo dogo likasambaa kila mahali na kuleta madhara.

 

“Mfano kama mtu kaiba taarifa za kifedha za watu na kuziweka mtandaoni inaweza kupelekea watu kuibiwa, Tanzania bado tupo kwneye kujenga mifumo ya teknolojia ambayo itatutambulisha kwa urahisi. Mtu akidukua taarifa zako anaweza kuzifanya na ankra ikaenda kwa aliyechukua,”amesema Dkt. Mkilia.

 

“Maisha ni mchezo wa kuigiza hakuna anayeoenda taarifa zake zikatolewa hadharani, kwenye uhuru wako na faragha zako unaweza kufanya mambo ambayo wengi hawaamini.Si kila mtu anapenda mambo yake yajulikane, na usiri huo ndio utu wa mtu husika,”amefafanua.

 

Amesema zana ya taarifa binafsi ni muhimu inahusisha kila mmoja kuwa na udhibiti wa taarifa zake, bila kufanya hivyo ni rahisi kuingia kwenye mzozo kwa uvunjaji wa taarifa binafsi, kutokuelewa kunaweza kusababisha madhara ya wizi, unyanyapaa, unyanyasaji na kuumiza watu.

 

Kwa mujibu wa Dkt. Mkilia taarifa binafsi linagusa usalama wa nchi, kwa kuwa adui akishajua ni taarifa binafsi atajua namna ya kuzitumia vibaya.

 

 

Post a Comment

0 Comments