NA MWANDISHI WETU
Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imebainisha kuwa baadhi ya nyumba za kulala wageni na ofisi zinakusanya taarifa za watu kupitia kamera za CCTV bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Taarifa hizo baadaye hutumika kwa matumizi mengine, jambo linalokiuka Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Tume hiyo imeeleza kuwa kila taasisi, shirika, au mtu anayekusanya taarifa za watu anapaswa kuwa na sera inayoeleza wazi jinsi anavyokusanya, kuchakata, na kuzitumia taarifa hizo.
Pia, ni lazima taasisi hizo ziwe na afisa maalum anayesimamia usimamizi wa taarifa binafsi ili kuhakikisha zinatunzwa kwa mujibu wa sheria.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Tafiti za Ulinzi wa Taarifa na Teknolojia, Dkt. Noe Nnko, Machi 1, 2025, wakati wa kuwasilisha mada kuhusu teknolojia za ulinzi wa taarifa, changamoto zake, na wajibu wa afisa wa taarifa binafsi kwa wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
"Hoteli zinakusanya taarifa nyingi za wageni kwa kutumia kamera za CCTV. Ni lazima ziwe na afisa aliyethibitishwa wa kusimamia na kutunza taarifa hizo. Wasipofanya hivyo, wanavunja sheria."
Dkt. Nnko ameongeza kuwa matumizi holela ya kamera za CCTV yamefanya watu wengi kupoteza faragha zao bila kujua taarifa zao zinatumikaje.
"Unapoingia hotelini, unakuta kamera kila kona zinakurekodi. Wanakusanya taarifa nyingi bila mwongozo wa kisheria. Sheria inawataka wamiliki wa kamera hizi kusajiliwa na Tume, kuwa na sera ya kutunza taarifa, pamoja na afisa maalum anayesimamia kazi hiyo. Hata hivyo, wengi bado hawajatekeleza matakwa haya," amesisitiza.
Aidha, Dkt. Nnko amebainisha kuwa taasisi au mtu anayevunja Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi anaweza kuadhibiwa, ambapo fidia inaweza kufikia Sh milioni 100.
Tume hiyo imeendelea kuhimiza taasisi na makampuni kuhakikisha wanazingatia sheria kwa kusajili mifumo yao ya ukusanyaji wa taarifa na kuwa na sera rasmi za usimamizi wa taarifa binafsi ili kulinda haki za wananchi.
0 Comments