NA MWANDISHI WETU
TUME ya Ulinzi wa Taarifa (PDPC) imewataka watumiaji wa nyumba za kulala wageni kutoandika taarifa za mahali walipotoka na wanapokwenda, kufanya hivyo ni ukiukwaji wa Sheria ya Taarifa Binafsi.
Hatua hii inalenga kulinda faragha ya mtu binafsi na kuzuia matumizi mabaya ya taarifa hizo.
Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji wa PDPC, Stephen Wangwe amesisitiza umuhimu wa wananchi kufahamu sheria ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza.
Ameeleza kuwa taarifa kama mahali mtu alikotoka, anakokwenda, au hata kabila lake, hazihusiani na sababu za kufikia kwenye nyumba za kulala wageni, hivyo hazipaswi kuandikwa.
“Unakwenda nyumba ya kulala wageni unaambiwa andika ulikotoka na unakokwenda, kabila lako lakini haya yote ni taarifa binafsi na wanavunja sheria.
Akiongelea utangazaji wa matokeo ya wanafunzi, amesema kipindi cha nyuma matokeo ya mitihani yalikuwa yanatangazwa kwa majina, sasa ni marufuku na badala yake inatakiwa kuweka namba ili kulinda taarifa za mtu,” amesema Wangwe.
Kwa mujibu wa PDPC, ni muhimu kwa wamiliki wa nyumba za kulala wageni na taasisi nyinginezo kuzingatia sheria hii ili kuepuka kuvunja haki za faragha za watu.
Serikali inaendelea kuhamasisha uelewa wa umma kuhusu matumizi sahihi ya taarifa binafsi kwa mujibu wa sheria.
0 Comments