Tanzania
imeendelea kupata mafanikio makubwa katika kuimarisha shughuli za uhifadhi kwa
kutokomeza ujangili wa tembo na biashara haramu ya nyara katika maeneo
yaliyohifadhiwa.
Mamlaka ya
Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema kuwa eneo la ulinzi na usimamizi wa
rasilimali za wanyamapori limeendelea kupata matokeo chanya kutokana na nguvu
kubwa na mikakati madhubuti iliyowekwa kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na
ushirikishwaji jamii katika masuala ya uhifadhi.
Hayo ni kwa mujibu wa Ofisa Wanyamapori wa
Kitengo cha Upelelezi kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Tryphone
Kanon alipokuwa akizungumza katika mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari
yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET)
kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la USAID.
“Kupungua kwa
ujangili nchini kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuendelea kuimarishwa ulinzi na
kushirikiana
na wadau mbalimbali sambamba na wananchi wanaoishi katika maeneo ya hifadhi ili kuidhibiti vikundi vya uhalifu dhidi ya wanyamapori kama tembo, faru
na wengineo waliopo katika hifadhi mbalimbali za Taifa,” alisema Kanon
Ofisa huyo alisisitiza kuwa hali sasa ni tofauti na kuwa
ripoti ya TAWA ya hivi karibuni imeonesha
kuwa mauaji ya tembo yamepungua kutoka matukio 18 mwaka 2016 hadi
matukio matatu mwaka 2023.
“Kiwango cha ujangili wa tembo kimeshuka
katika hifadhi za Taifa ukilinganisha na hali ilivyokua miaka ya nyuma. Kwa
sasa meno ya tembo yanayokamatwa mengi ni ya miaka ya nyuma, na mapya yamekuwa ni
nadra kuonekana, jambo ambalo linaonyesha kwamba mapambano dhidi ya ujangili
yanazaa matunda,” alisema Kanon
Aliongeza
kuwa kupungua kwa mizoga ya tembo iliyouawa na
majangili kwenye maeneo mengi ya hifadhi nchini ndio kumeifanya TAWA kuamini
kuwa sasa hali ni shwari. Lakini hawajaishia hapo bali wameendelea kuimarisha
ulinzi na kujitahidi kudhibiti mitandao ya kijamii ambayo inatumika kama njia
ya mawasiliano ya uhalifu wa wanyamapori.
Matokeo ya jitihada hizo za
opereheni za TAWA ni kufanikiwa kuendelea kukamata watu waliohifadhi meno ya
tembo ambapo kwa mwaka 2023 walikamatwa watu 3,700.
Pamoja
na hilo, Kanon alizungumzia mbinu mpya ya ujangili wa kutumia mapanga ambao umeshamiri hivi sasa
kuliko matumizi ya risasi kama ilivyozoeleka huko nyuma, ambapo muwindaji haramu
humkata panga mnyama miguuni ili kumfanya ashindwe kutembea ama kukimbia hivyo
inakuwa rahisi kumuua.
Risasi
hazitumiwi sana kwa sasa kwasababu ni ghrama lakini pia ni kuogopa milio yake
ambayo inaweza kuwashtua askari wanyamapori kwa haraka pia kuwashtua wanyama
wegine na kuwafanya wakimbie, kitu ambacho ni changamoto kubwa kwa wawindaji
haramu,”.
“Tawa
tumebaini mbinu hiyo, hivyo nasi tunaimarisha ulinzi kwenye hifadhi zetu
kuhakikisha kwamba hakuna majangili wanaofanikiwa katika mbinu zao za kuua
wanyama,” alisisitiza Kanon
Kwa
upande wake Dkt. Elikana Kalumanga ambaye ni Meneja wa ushirikishwaji wa sekta
binafsi, mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili alisema ili kuweza kukabiliana na
ujangili wa wanyamapori ni vyema kuwepo ushirikishwaji wa jamii na wadau
wengine wa mazingira ili kusaidia juhudi za uhifadhi wa shoroba na mazingira
kwa ujumla.
“Ushirikishwaji huo unapaswa kuwagusa wadau wote wa mazingira ili kuleta maendeleo endelevu ya malaisili zilizopo,” alisema Dkt. Kalumanga
Dkt. Kalumanga
amesisitiza kuwa ikiwa wadau hao muhimu wakishirikiana kwa pamoja katika michakato
mbalimbali ya usimamizi wa mazingira itasaidia kulinda, kuhifadhi, kutunza na
kusimamia mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Akizungumza
katika katika mafunzo hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu
ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano (SJMC), Dkt.. Abdallah Katunzi alisema kuwa
waandishi wa habari haswa wanawake wana nafaasi kubwa ya kuelimisha umma kwa
weledi juu ya masuala ya uhifadhi kwani wao ndio huguswa moja kwa moja na changamoto
za uhifadhi.
“Wanawake ni nguzo kubwa katika tasnia ya habari na italeta jita sana wakisaida katika kuripoti mambo ya ujangili wa wanyamapori kwasababu yale madhara yatokanayo na ujangili kwa namna moja au nyingine yanawakuta wao kwasababu wanahusika na hivi vitu, unakuta ni madhara kwa watoto na hata athari za kiuchumi mara nyingi zinawaumiza wanawake kwanza,” alisisitiza Dkt.. Katunzi
Pia
kwakua jukumu hilo ni la waandishi wa habari, Dkt.. Katunzi amesisitiza
iongezwe kasi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya uhifadhi na umuhimu
wake kwa maendeleo ya vizazi vijavyo na Taifa kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi wa JET, John Chikomo alisema kupitia mafunzo hayo yaliyoratibiwa na JET chini ya
ufadhili wa USAID, yanalenga kuwapa waandishi wa habari za mazingira
uelewa zaidi juu ya masula ya uhifadhi
wa wanyamapori na mazingira kwa ujumla wake ili kuandika habari kwa kina na iwe
rahisi kufikisha ujumbe kwa ufasaha kwa jamii.
0 Comments