Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imefanikiwa kuitumia miaka miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kufikisha umeme kwenye vijiji 5,481.
Hatua hiyo ni sehemu ya mafanikio mbalimbali ya Mamlaka hayo tangu Machi 19,2021 hadi sasa. Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Machi 19, 2024 na Kitengo cha Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano, REA ilieleza mikakati na mafanikio waliyoyapata ndani ya muda huo.
Mbali na kuvifikia vijiji hivyo vilivyoongeza idadi ya vijiji vilivyofikiwa na umeme kufikia 11,843 sawa na asilimia 96.14 ya vijiji vyote nchini ambavyo ni 12, 318 pia REA imevifikia vitongoji 5,562 na kufanya vitongoji vyenye umeme kufikia 32,750 sawa na asilimia 51 ya vitongoji vyote nchini ambavyo ni 64,760.
Vitongoji vingine 8,150 vitafikishiwa umeme kupitia Miradi ya Ujazilizi kabla ya kuisha mwaka 2025.
“Kwa upande wa nishati safi ya kupikia, hadi sasa REA imewezesha ugawaji wa Mitungi ya Gesi (LPG) na vichomeo vyake 83,500. Vilevile, ndani ya Mwaka wa Fedha 2023/24, REA itagawa kwa bei ya ruzuku, Mitungi ya Gesi takribani 450,000 pamoja na kujenga mifumo ya nishati safi ya kupikia kwa Taasisi 100 zinazohudumia watu zaidi ya 300,”ilieleza taarifa hiyo ya REA
Miradi hiyo ni endelevu na itatekelezwa kila mwaka ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hasan katika azma yake ya kumtua mama mzigo wa kuni, kulinda misitu, kuzuia mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kulinda afya za Watanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan. |
0 Comments