Ticker

7/recent/ticker-posts

MIAKA 3 YA RAIS SAMIA, TAWA YANUFAISHA VIJIJI 187 YATOA GAWIO LA ZAIDI YA BILIONI 8

 

Kamishna wa Uhifadhi -TAWA, Tabula Nyanda.

NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-DSM

 

Katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inayotimia kesho Machi 19,2024 imekuwa na tija kubwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

 

Katika kipindi hicho cha mwaka 2021/24 TAWA imeweza kutoa gawio la shilingi bilioni 8. 95 kwa wanufaika wa shughuli za Utalii katika Halmashauri za wilaya 32 na vijiji 187 .

 

Mbali na kuimarisha mahusiano na dhana nzima ya uhifadhi kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi, fedha hizo zinatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayoibuliwa na  wananchi.  


Hayo yamesemwa na Kamishna wa Uhifadhi wa mamlaka hiyo Mabula Misungwi Nyanda alipokuwa akiwasilisha taarifa yake ya mafanikio ya TAWA kwa kipindi cha miaka mitatu cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita  2021/22-2023/24.

Kamishna Mabula alikuwa akizungumza na Wahariri na Waaandishi wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini, leo Machi 18,2024.

Kamishna Mabula amesema TAWA imeongeza ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za uhifadhi, ambapo pia wanawezesha miradi ya maendeleo kwa Jamii.

 

“TAWA imeendelea kushirikiana na jamii katika shughuli za uhifadhi kwa kuchangia miradi ya maendeleo inayoibuliwa na jamii kwenye maeneo  mbalimbali hususan yanayozunguka Mapori ya Akiba. 

“Kati ya mwaka 2021 na 2024 TAWA imechangia miradi ya jamii yenye thamani ya Shilingi milioni  193.3 ikiwemo, ujenzi wa Soko la samaki katika mji mdogo wa Ifakara – Kilombero ( TSh. Milioni 66) na ujenzi wa darasa, ofisi ya walimu pamoja na ununuzi wa madawati katika shule ya Msingi Usinge Kaliua –Tabora ambao umegharimu shilingi Milioni 50.”

Aidha TAWA imechangia madawati  100 katika Wilaya ya Bunda, ununuzi wa mashine mbili za Kusaga katika Mkoa wa Mara, kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na darasa – Mwibara na kuchangia shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Bungo - Korogwe. 

Kwenye eneo la uvuvi na ufugaji nyuki katika Hifadhi, TAWA imesaidia kuweka utaratibu wa kuwezesha jamii kunufaika na shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki katika maeneo ya Mapori ya Akiba na Tengefu

 

Pamoja na kuimarika kwa mahusiano  na kuzalisha ajira kwa takribani wavuvi 7,511 na warina asali 2,046 na jumla ya  shilingi Bilioni 3.98 zimepatikana kutokana na shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki katika Mapori ya Akiba ya Rukwa, Ugalla, Uwanda, Moyowosi Kilombero na Inyonga. 

Maofisa wa TAWA, wakimsikiliza Kamishna Nyanda hayuko pichani.
 

“Wananchi wamekuwa wakinufaika kwa kuvua wastani wa tani 15 za samaki kwa siku katika pori la akiba Uwanda pekee. 

 

“Vilevile, kupitia uvuvi Halmashauri ya Sumbawanga imekusanya Shilingi milioni 303 kupitia leseni na ushuru  kutokana na uvuvi kwenye hifadhi  katika katika kipindi cha Julai –Desemba 2023..

 

MAFANIKIO YA TAWA NDANI YA MUDA MFUPI

 

TAWA ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009 na kutangazwa kwa amri  ya Serikali iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 135 la Mei 9, 2014, pamoja na marekebisho yaliyochapishwa katika gazeti la Serikali Na. 20 la Januari 23, 2015. 

 

Mamlaka hiyo ilianza kazi rasmi Julai 1,2016 kwa kuchukua majukumu ya kiutendaji ya Idara ya Wanyamapori kuhusu usimamizi wa rasilimali ya wanyamapori nje ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Ngorongoro. 

 


MAJUKUMU YA TAWA

Mamlaka hiyo inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007 na Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori sura 283 pamoja na kanuni zake. 

 

Aidha inatekeleza Mango Mkakati wake wa mwaka 2021/22-2025/26 ambao uliandaliwa kwakuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020 na Mpango wa Taifa wa Maendeleowa Miaka Mitano 2021/22-2025/26.

 

TAWA pia inazingatia mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa ya uhifadhi wa wanyamapori ambayo Tanzania imeridhia. 

 

Majukumu mahsusi ya TAWA Kusimamia Mapori ya Akiba, Tengefu na Maeneo ya Malikale,kusimamia maeneo yenye ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 133,276.36 yanayojumuishaMapori ya Akiba 28 (104,176.36 Km2), Mapori Tengefu 23 (29,100 Km2) na maeneo ya Malikale ya Kunduchi, Kilwa-Kisiwani, Songomnara, Sanje ya Kati na Majoma na Kisiwa cha Lundo.

 

Aidha TAWA inasimamia himasheria na kuzuia ujangili wa wanyamapori, hii inahusisha doria katika mapori ya Akiba na Tengefu, kudhibiti utoroshaji nyara kwenye maeneo ya mipaka (viwanja vya ndege, bandari na forodha), ulinzi wa Ghala Kuu la Nyara la Taifa na kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi na wadau wengine.

 

Kamishna Nyanda anasema pia TAWA inasimamia Mashamba na Bustani za wanyamapori za Serikali ambazo zinahusisha shamba la wanyamapori Makuyuni (47.2 Km2) na bustani tano  za Ikulu ya Chamwino na Dar es Salaam, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tabora na Ruhila.

 

Mbali ya shughuli hizo, lakini pia TAWA ina jukumu la kutatua migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu sanjari na kufanya doria za muitikio wa haraka kuokoa maisha ya watu na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yenye changamoto ya matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu (tembo, simba, fisi, nyati, mamba na kiboko);

Pia inaangalia maeneo 67 ya watu/kampuni binafsi ya ufugaji wa wanyamapori ambayo yanajumuisha mashamba manne, Bustani za Wanyamapori 32, Ranchi tano  na Maeneo ya uzalishaji 26.

Kwenye eneo la uangalizi wa Maeneo ya Hifadhi za Wanyamapori za Jumuiya, Kamishna Nyanda amesema wanashirikiana na taasisi nyingine za uhifadhi katika uangalizi wa wanyamapori katika hifadhi za Wanyamapori za Jumuiya (Wildlife Management Areas-WMAs) 22zenye ukubwa wa kilometa za mraba 28,891.08;

 

Aidha TAWA imekuwa ikitekeleza Mikataba ya Kikanda na Kimataifa ikiwa inahusisha Mkataba wa Biashara ya Wanyamapori na mimea iliyo katika hatari ya kutoweka- Convention on Internation Trade of Endangered Species of wild Fauna and Flora (CITES) ambao  unahusika na kudhibiti biashara ya nyara, Mkataba wa kuimarisha Bionowai (Convention on Biological Diversity – CBD), Mkataba wa kusimamia meneo ya ardhi oevu yenye umuhimu wa Kimataifa (Ramser Convention), Mkataba wa spishi za wanyamapori wahamao (Convention on the Conservation of Migratory species of wild animals). 

 

Kamishna Nyanda amebainisha kuwa TAWA imekuwa ikijenga na kuimarisha uwezo wake katika usimamizi wa wanyamapori

 


UTENDAJI KAZI NA MAFANIKIO  KATIKA KIPINDI CHA 2021/22-2023/24

 Kamishna Nyanda ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt Samia Samia Suluhu Hassan, TAWA imeendelea kutekeleza majukumu yakekwa kuzingatia Malengo Makuu matatu yaliyoainishwa katika Mpango Mkakati wa Mamlaka 2021/22 - 2025/26 ambayo ni uimarishaji wa Ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na malikale, uboreshaji wa Huduma za Utalii pamoja, na  Utendaji kazi wenye ufanisi na tija. 

“Malengo hayo yalitekelezwa ambapo mafanikio makubwa yaliyofikiwa ni pamoja na kupungua kwa  ujangili. Amesema ujangili wa tembo umepungua kutoka mizoga ya tembo sita mwaka 2021/22 hadi mizoga watatu mitatu Februari 2024.

 

“Mafanikio haya yanatokana kuimarika kwa ulinzi kulikochangiwa na kuongezeka kwa vitendea kazi, morali ya watumishi, mtandao kwa kiitelijensia, doria za mwitikio wa haraka matumizi yateknolojia na kufunga visikuma mawimbi ili kufuatilia mienendo ya wanyamapori katika kuhakikisha wanyama wanakuwa salama.”

 

KUPUNGUA KWA MIGOGORO 

Kamishna amesema kuwa TAWA imeendelea kushirikiana na wananchi katika kutatua migogoro kwenye maeneo ya hifadhi kwa kutekeleza maelekezo ya Serikali yaliyotolewa kupitia Kamati ya Mawaziri nane  wa Wizara za Kisekta.  

“Kwa kushirikiana na wananchi migogoro ya mipaka katika Mapori ya Akiba saba  ya Swagaswaga, Mkungunero, Wamimbiki, Igombe, Liparamba, Mpanga Kipengere na Selous kati ya nane yaliyotolewa Maelekezo na Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta imemalizika ambapo jumla ya vigingi 1,681 vimesimikwa kuzunguka mipaka ya hifadhi.  

“Aidha katika utatuzi wa migogoro hiyo eneo lenye ekari 103,544.48  limemegwa  kutoka kwenye hifadhi  na kuwapatia wananchi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.  Sambamba na hilo, Serikali kupitia TAWA inaendelea kukamilisha zoezi la kulipa fidia kaya 145 zilizo katika Pori la Akiba Mkungunero.”

DORIA NA MWITIKIO WA HARAKA

 Kutokana na ongezeko la matukio ya wanayapori wakali na waharibifu kati ya mwaka 2021-2024 TAWA imefanya jumla ya doria siku watu 58,818 kukabiliana na matukio 8,001 yaliyotokea katika Wilaya 73 nchini. 

 

Jitihada nyingine zilizofanyika ili kupunguza madhara kwa maisha ya watu na mali  zao ni pamoja na kujenga vituo vituo 16 vya askari katika Wilaya 16 ili kuitikia kwa haraka matukio  ya wanyamapori wakali na waharibifu pia wamenunua pikipiki 50, kutoa mafunzo na kushirikisha  Askari wa wanyamapori wa vijiji -Village Game Scout na jeshi la akiba wapatao 184. “Askari waliopata mafunzo ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wanafanya kazi kwenye maeneo sugu ya matukio (Bunda, Busega, Meatu, Same, Lindi, Korogwe,Itilima, Liwale, Nachingwea, Mwanga, na Tunduru.

 

“Kuongeza vituo vya muda vya askari (ranger stations) kutoka 46 hadi 55, Kuongeza idadi ya askari wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kutoka 139 hadi 237, ujenzi wa mabwawa 10 katika mapori ya akiba Kizigo-09 (lililopo Manyoni) na Mkungunero - 01 (katika Wilaya ya Kondoa).”

Aidha TAWA imetoa elimu ya uhifadhi na mbinu rafiki za kujikinga na madhara ya wanayapori wakali na waharibifu kwa wananchi 764,438 katika vijiji 1,319 nchini.

Pia imeimarisha vikundi 179 vya wananchi vya kufukuza tembo na kutoa vifaa vya kufukuza tembo ikiwemo Roman candles 1,320, thunder flashes 1,310, vuvuzela 548, filimbi 288, tochi 524, mbegu za pilipili, mabomu ya pilipili.

TAWA imefunga visukuma mawimbi kwa viongozi wa makundi ya tembo 8 katika Wilaya za Same, Tunduru, Liwale na Nachingwe; na kuimarisha mawasiliano kwa kutoa namba ya kupiga simu bure ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa mapema. 

“Kufuatia juhudi hizi, madhara hasi ikiwemo idadi ya vifo imepungua kutoka vifo 318 kati ya mwaka 2017-2020 hadi vifo 259 kati ya mwaka 2021-2024 licha ya kuongezeka kwa matukio.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments