Ticker

7/recent/ticker-posts

MRADI WA ECO SCHOOL RAFIKI WA MAZINGIRA KWA JAMII YA MUHEZA

 


NA JIMMY KIANGO-ALIYEKUWA MUHEZA

Waswahili wanayo methali isemayo ‘Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.’ Methali hii inawiana na ile insemayo ‘samaki mkunje angali mbichi.”

 

Methali hizi mbili zinabeba maana ya kuikumbusha jamii kulea mtoto katika malezi sahihi na bora ambayo yatakuwa na tija kwa jamii.

 

Wilaya ya Muheza iliyopo mkoani Tanga, imezibeba methali hizi kwa uzito wa hali ya juu na inazisimamia kwa vitendo kwa kuwafundisha wanafunzi wa shule za msingi umuhimu wa kutunza mazingira kuanzia ngazi ya chini kabisa.

 

Mradi wa Eco School ndio umebeba dhamana  ya kumlea mtoto wa tarafa ya Amani katika kuujua umuhimu wa kutunza mazingira.

 

Ieleweke kuwa mradi wa Eco School ni mpango unaolenga kukuza elimu ya mazingira kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla. 

 

Lengo kuu ni kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kutunza na kuhifadhi mazingira kupitia mbinu za kiikolojia, kama vile matumizi endelevu ya rasilimali, uhifadhi wa nishati, upandaji miti na usafi wa mazingira.

 

Mradi huu unalenga kuwa na shule zinazojali mazingira, ambazo wanafunzi wanajifunza kwa vitendo juu ya uendelevu wa mazingira, uzalishaji wa chakula bora kwa njia ya kilimo hai, pamoja na mbinu za kisasa za matumizi ya nishati safi kama vile nishati ya jua.

 

Kupitia mradi huu, shule zinashirikishwa katika mipango ya kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuongeza uelewa wa athari za mabadiliko ya tabianchi na kutekeleza miradi midogo midogo kama bustani za shule, vituo vya kuchakata taka na teknolojia rafiki kwa mazingira. 

 

Mradi wa ECO SCHOOL unawaandaa wanafunzi kuwa mabalozi wa mazingira katika jamii zao.

 

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye shule ya Msingi Kwezitu iliyopo katika Kijiji cha Kwezitu, Kata ya kwezitu, Tarafa ya Amani wilayani Muheza ikiwa na takribani wanafunzi 497.

 

Timu ya waandishi wa Habari za Mazingira wakiongozwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) chini ya mkurugenzi wake John Chikomo ikiwa katika mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na USAID, ilifika kwenye shule hiyo na kuzungumza na wanafunzi wa waalimu wanaosimamia mradi huo wa Eco School.

 

Mwalimu wa mazingira wa shule ya Msingi Kwezitu, Gladness Masonda (kulia) akielezea umuhimu wa mradi wa Eco School katika shule ya Msingi Kwezitu.

Mwalimu wa mazingira wa shule ya Msingi Kwezitu, Gladness Masonda aliwaambia waandishi wa Habari kuwa moja ya mambo wanayoyafurahia kwenye shule hiyo ni kupaya mradi wa Eco School.

 

Mwalimu Masonda anaweka wazi kuwa, kabla ya ujio wa mradi huo ambao unatekelezwa na Nature Tanzania chini ya udhamini wa USAID, hali ya mazingira kwenye shule yao ilikuwa mbaya.

 

“Kulikuwa na mmomonyoko wa udongo kwenye maeneo yetu mengi, lakini pia wananchi waliligeuza eneo la shule kuwa njia, lakini baada ya kupata mradi hu una kupatiwa elimu ya utunzani wa mazingiras, hali imebadilika kabisa, tumeweza kupanda majani na nyasi zinazozuia mmomonyoko pamoja na kuweka mazingira ya shule katika ubora.

 

“Kwa sasa hakuna mtu anaeweza kupita katika eneo la shule maana mazingira yamekuwa mazuri hali inayomfanya mtu kuona aibu kuyavuruga, lakini pia tumeweka taratibu za kuwajibishana hasa pale mtu anapokwenda kinyume na tunachokifanya,”alisema Msonda.

 

Kwa upande wake Mwalimu Ramadhani Issa, alisema mradi wa Eco School una maana kubwa kwa jamii na anatamani uelekezwe kwenye shule za msingi nyingi nchini kwa sababu unasaidia kumuandaa mtoto kuujua umuhimu wa kutunza mazingira tangu akiwa mtoto.

 

Mradi wa Eco School unaunganisha wanafunzi, waalimu na jamii ya eneo husika, ambapo makundi hayo yanapata nafasi ya kujumuika pamoja kwenye vikao rasmi vinavyolenga namna ya kuendeleza mradi.

 

“Kila darasa linatoa wanafunzi wawili ambao hawa wanawawakilisha wenzao, jamii nayo inatoa watu wawili ambao wanaungana na waalimu wawili ambao kwa pamoja wanaunda kamati maalum (bunge) ambayo inabeba jukumu la kukutana kwa ajili ya kuujadili mradi huo,” alisema Issa.

 

Mwalimu Masonda, alisema mbali ya kupata elimu ya kutunza mazingira, lakini pia mradi huo umewasaidia kupata elimu ya kufuga nyuki pamoja na kuwezeshwa mizinga na tayari wana mizingia 20 na kati ya hiyo 17 imejaa nyuki.

 

Mwanafunzi wa dares la sita Jackline Shetui (kushoto) akiwa na mwanafunzji mwenzake Dastan Kajembe ambao ni wajumbe wa kamami ya maradi wa Eco School.

Jackline Shetui ni mwanafunzi wa darasa la sita wa shule ya Msingi Kwezitu ambae ni mjumbe wa kamati ya Eco School anasema elimu ya mazingira aliyoipta imemsadia kuwa balozi mzuri wa mazingira kuanzia shuleni hadi nyumbani.

 

Dastan Kajembe nae ni mjumbe wa kamati hiyo ambaye anawakilisha darasa la nne, ameonekana kufurahia mradi huo na kuahidi kuhakikisha anaitumia nafasi yake kuwaeleza wanafunzi wenzake umuhimu wa Watoto kutunza mazingira.

 

Nature Tanzania na USAID wameupeleka mradi huo pia kwenye shule ya Msingi Msasa IBC iliyopo katika Kijiji cha Msasa IBC.

Mwanafunzi wa dares la sita wa smule ya Msingi Msasa IBC, Upendo Sangoda.
Shule hiyo iliyopo barabara ya Madizini, ilikuwa moja ya shule zinazokabiliwa na mmomonyoko wa ardhi, hali iliyosababisha eneo kubwa la shule hiyo kutawaliwa na makorongo.

Mwalimu George Luena ambae ndie msimamizi mkuu wa mradi wa Eco School katika shule hiyo, anasema kama wasingefanikiwa kupata mradi huo mwaka 2022 bila shaka eneo hilo la shule lingekuwa limekwisha kwa mmomonyoko.

 

“Huku suala la mvua ni la mara kwa mara, hali hiyo ilikuwa inachangia ardhi ya eneo la shule kumomonyoka mara kwa mara, lakini ujio wa Eco School umetusaidia kupanda nyasi zilizosaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo.”

 

Luenda amesema mradi huo pia umewasaidia kupata mradi wa ufugaji nyuki na tayari wanayo mizinga 20 na 16 kati ya hiyo imeshaanza kujaa nyuki.

 

ECO SCHOOL NA UTALII WA NDANI

Mwalimu wa Mazingira wa shule ya Msingi Msasa IBC, Mariam Shekuamba amewaambia waandishi wa Habari kuwa ameamua kuutumia mradi huo kuwafundisha wanafunzi wake utuzani wa mazingira, lakini pia utalii wa ndani.

Msimamizi mkuu wa Mradi wa Eco School, smule ya msingi Msasa IBC, Mwalimu George Luena. 

 “Nimeanzisha mpango wa kuwahamasisha wanafunzi wang una mna ya kufanya utalii wa ndani, nimekuwa nikizitumia siku za Ijumaa kuchukua wanafunzi wa darasa la kwanza au darasa la pili na kwenda nao milimani kwenda kuangalia ndege miti na viumbe hai vingine vilivyoko huko.

 

“Mpango wangu huu umewafanya wanafunzi wangu wengi kuachana na tabia ya kwenda kuwinda ndege na badala yake wamekuwa wakiujua umuhimu wa ndege kwenye utalii.

 

“Sasa hivi hawawindi tena ndege, badala yake wamekuwa walinzi wa ndege hao nah ii ni kwa sababu nimekuwa nikiwaambia kuwa viumbe hai jamii ya ndege ni muhimu kwa Maisha ya bidamu, zamani walikuwa wanaacha kuja shule wanakwenda kuwinda ndege, hali ni tofauti kwa sasa, badala ya kwenda kuwinda wamekuwa wakiomba kwenda kufanya utalii,” alisema Shekuamba.

 

Ushuhuda wa utalii wa ndani na umuhimu wa mradi wa Eco School, umetolewa na mwanafunzi wa darasa la sita Upendo Sangoda na Mohamed Mussa ambao pia ni wajumbe wa kamati ya mradi huo shuleni hapo.

 

Mwalimu wa Mazingira wa Smule ya Msingi Msasa IBC, Mariam Shekuamba.

Mwanafunzi Upendo Sangoda ambae anauwezo mkubwa wa kujieleza na kuchambua umuhimu wa mazingira, amesema kuwa dhamira yake kuu ni kuwa Rais wa nchi na pamoja na majukumu mengine, lakini atahakikisha wananchi wake wanaujua umuhimu wa kutunza mazingira.

 

“Hamu yangu ni kuja kuwa Rais, sio jambo rahisi ila naamini inawezekana na ikitokea nikafanikisha ndoto yangu hiyo, nitahakikisha suala la utunzani wa mazingira linakuwa kipaumbele change kwa sababu mazingira ni Maisha.” 

 

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Msasa IBC, Barnaba Mloka alisema pamoja na kuwa na changamoto za vyoo, madarasa, madawati, vitabu na ofisi ya Mwalimu Mkuu na walimu wengine, suala la mazingira ya shule kuharibika lilikuwa likimsumbua sana.

 

“Angalau sasa nina amani kwenye eneo la mazingira, kama mlivyoona hali sio mbaya kama ilivyokuwa huko nyuma, sasa napambana na hizi changamoto za madawati, vyumba vya madarasa, vitabu, matundu ya vyoo na ofisi za waalimu,kwenye maeneo haya kiukweli pia tunahitaji msaada,” alisema  

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Msasa IBC, Barnaba Mloka



Post a Comment

0 Comments