Ticker

7/recent/ticker-posts

MSAJILI WA HAZINA, AMSONS KUJENGA KIWANDA CHA SARUJI TANGA, CHA MBEYA KUPANULIWA,AJIRA ZA UHAKIKA 12,000 KUPATIKANA


NA MWANDHISHI WETU

Mazingira Rafiki ya uwekezaji nchini yaliyotengenezwa zaidi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yameendelea kuleta tija nchini,  ambapo leo Ofisi ya Msajili wa Hazina, na kampuni ya AMSONS ya Uswisi, wameingia makubaliano ya kuwekeza zaidi ya tsh. 800 bilioni katika upanuzi wa kiwanda cha Saruji Mbeya na kuanzisha kiwanda kipya cha saruji jijini Tanga.  

Makubaliano hayo yamefikiwa leo Oktoba 15 jijini Dar es Salaam baina ya pande zote mbili na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, aliwaambia na waandishi wa habari kuwa makubaliano hayo yataleta mabadiliko makubwa kwenye biashara ya saruji nchini. 

Mchechu alisema mkataba mzima unahusisha dola za Marekani 320 milioni kati ya fedha 

hizo, dola 190 milioni (sawa na  tsh.513 bilioni) zitatumika kwaajili ya ujenzi wa kiwanda kipya jijini Tanga na dola 130 milioni (sawa na tsh.351 bilioni) ni kwaajili ya upanuzi wa kiwanda cha Saruji Mbeya.

“Hivi ninavyozungumza nanyi, tayari tumeshafanya maamuzi ya msingi. Kazi zilizobakia ni za kimenejimenti, ikiwemo kumalizia mpango wa biashara na hatua nyingine za kifedha,” alisema Mchechu.

Alisema mradi huu wa upanuzi wa kiwanda cha saruji Mbeya na ujenzi wa kiwanda kipya Tanga, unaotarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili hadi mitatu, utapelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa klinka mara 10.

Kwa kiwanda cha Mbeya, uzalishaji wa klinka, malighafi muhimu kwa utengenezaji wa saruji, unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 1,000 kwa siku hadi kufikia tani 5,000.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu

Alifafanua zaidi kuwa kwa upande wa kiwanda kipya cha Tanga, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 5,000 za klinka kwa siku.  

“Kuongeza kwa uzalishaji kutatufanya tuendelee kulikamata vizuri soko la nyanda za juu kusini ambalo tumekuwa tukilihudumia kwa zaidi ya asilimia 70 kwa muda mrefu,” alisema Mchechu.

Aliongeza: “Uwekezaji huu pia utakuwa mwanzo wa kupenye kwenye nchi jirani za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.”

Mchechu alisema uwekezaji huo ni matokeo ya uboreshwaji wa mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Uwekezaji huu ni sehemu ya mabadiliko ambayo Rais amekuwa akitamani kuyaona katika mashirika ambayo Serikali ina hisa,” alisema.

Mkurugezi wa fedha wa AMSONS, Ahmed Mhada alisema kukamilika kwa mradi wa upanuzi na ujenzi wa kiwanda kipya kutaongezeka uzalishaji wa saruji kutoka tani milioni 1.1 kwa mwaka hadi kufikia tani milioni 4.2.

“Kuongezeka kwa uzalishaji kutaongeza gawio mara 10 ya lile ambalo Serikali ilipata mwaka jana,” alisema Mhada.

Serikali, ambayo inamiliki asilimia 25 ya hisa, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, mwaka jana ilipata gawio la tsh.3 bilioni, ikiwa ni miaka 10 ipite bila kampuni hiyo kutoa gawio.

Kama ongezeko la uzalishaji linatarajiwa kuongeza gawio mara 10, tafsiri yake ni kuwa serikali inatarajia kuanza kupata tsh.30 milioni kama gawio baada ya mradi kukamilika.



Akizungumzia suala la ajira Mhada, alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutazalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja 12,000.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Saruji Mbeya, Prof. Siasa Mzenzi, alimshukuru  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji nchini.

“Anachofanya Rais, kinavutia wawekezaji kuwekeza nchini. Tuko tayari kusimamia uwekezaji huu ipasavyo kwa maslahi mapana ya Taifa letu na watu wake,” alisema Prof. Mzenzi.

Kadri siku zinavyozidi kwenda, idadi ya watu inazidi kuongezeka, na hatimaye mahitaji ya saruji yanazidi kupaa.

Mpaka kufikia Desemba 2023, uzalishaji wa saruji Tanzania ulikuwa tani milioni 11 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 7.5.

Kiwanda cha Saruji cha Mbeya kinamilikiwa kwa ubia kati Kampuni ya Amsons kutoka Holcim ya Uswisi (65%), Serikali ya Tanzania kupitia kwa Msajili wa Hazina (25%) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wenye hisa (10%).



Post a Comment

0 Comments