Daktari Bingwa wa akina mama na
mtaalam wa uzazi pandikizi Dkt Clementina Kairuki (kushoto) akitoa ufafanuzi juu
ya namna teknolojia ya kuchunguza mayai tumboni (SMART ULTRASOUND) inavyofanya
kazi
Hospitali ya Kairuki kupitia kituo
chake cha Kairuki Green IVF (KGIVF)
imefanikiwa kuanza matumizi ya
teknolojia mpya ya Smart Ultrasound inayoweza kuona na kutambua mayai
yaliyomo tumboni mwa mama katika hatua za awali za ukuaji wake.
Hatua hiyo imeanza mwishoni mwa mwezi September, 2024 ambapo mashine hiyo inawasaidia wataalam wa mambo ya uzazi kuona na kuhesabu mayai yaliyomo tumboni mwa mama kwa urahisi zaidi hali ambayo inaongeza ufanisi katika matibabu ya uzazi pandikizi
Akizungumza mara baada ya mafunzo juu ya Teknolojia hiyo kutolewa, Daktari Bingwa wa akina mama na mtaalam wa uzazi pandikizi Dkt Clementina Kairuki amesema kuwa kifaa hicho kitaongeza ufanisi katika shughuli za uzazi pandikizi.
"Smart Ultrasound hii itasaidia madaktari kufuatilia maendeleo ya mayai kwa usahihi, kurahisisha hatua za upandikizaji, kuhesabu mayai kwa muda mfupi, kugundua vimbe zilizojificha kwenye kizazi pamoja na kuongeza nafasi za mafanikio katika matibabu ya uzazi kutokana maboresho na ufanisi uliopo katika Ultrasound hiyo," alisema Dkt Clementina.
Kuhusu gharama za matibabu ya uzazi pandikizi, Dkt. Clementina amesema, “Green IVF imeandaa mpango maalumu wa malipo ambao ni rafiki kabisa, tumekuja na kifurushi ambacho tunakiita primary, kinamuwezesha mgonjwa kufanyiwa vipomo vyote angalau akajua tatizio lake ni nini, halafu baada ya hapo ndio tunaangaalia matibabu yakoje.”
Aliongeza kuwa, “Pia sisi tunaruhusu mtu kufanya malipo kidogo kidogo, ni kweli tunajua hizi teknolojia ni za gharama lakini haina maana wasiokuwa na uwezo wa kulipa moja kwa moja wasipate huduma. Hivyo mgonjwa ataweka pesa kidogo ikifikia kiwango ambacho kitatosha kufanya matibabu anatibiwa.”
Pamoja na mambo mengine, Dkt Clementina alisema kuwa kushindwa kuzaa watoto ni unyanyapaa wa kijamii unaosababisha masuala ya Afya ya Akili. Wanawake ndio waathiriwa zaidi wa unyanyapaa ingawa wanaume pia huchangia utasa kwa takriban asilimia 50.
Hivyo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza masuala ya ugumba, Hospitali ya Kairuki ilizindua Kairuki Green IVF ambayo ni hatua muhimu katika maendeleo ya huduma za uzazi nchini.
Pia kwa kutambua umuhimu wa teknolojia hiyo, hivi karibuni Hospitali ya Kairuki ilitoa mafunnzo maalumu kwa Madaktari Bingwa wa Akina Mama na Uzazi, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wataalamu kutoka hospitali mbalimbali ndani na nje ya nchi. Mafunzo hayo yaliwapa washiriki fursa ya kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa Madaktari Bobezi wa Hospitali ya Kairuki.
0 Comments