Ticker

7/recent/ticker-posts

USAID YAWAEPUSHA WAKULIMA WA KARAFUU NA MIKOPO YA KAUSHA DAMU MUHEZA

Mkazi wa kijiji cha Kwezitu, Emmanuel Mkufya akieleza jambo kwa Waandishi wa Habari za Mazingira (hawapo pichani)
NA JIMMY KIANGO- ALIYEKUWA MUHEZA

Mkopo wa kausha damu ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya mkopo ambao una riba kubwa sana na masharti magumu ya ulipaji.

Mkopo huu unaweza kusababisha mkopaji kujiongezea mzigo mkubwa wa madeni, masharti ya kulipa yanaweza kuwa magumu kufuatia riba inayoongezeka haraka au ada nyingi zisizotarajiwa.

 

Hali hii husababisha mkopaji kuingia kwenye mzunguko wa kulipa madeni ya kila siku, hali inayosababisha sehemu kubwa ya mapato au mali zake kuchukuliwa ili kulipia mkopo huo.

 

Mkopo huo humwacha mkopaji katika hali ngumu kifedha na wakati mwengine kiafya kwa sababu unaongeza msongo wa mawazo. 

 

Hii ndio sababu mkopo huu unafananishwa na "kukausha damu" kwa sababu ya mzigo mkubwa wa kifedha anaobebeshwa mkopaji.

 

Adha hiyo iliwafika wakulima wengi wa mazao ya viungo kwenye tarafa ya Amani wilayani Muheza mkoani Tanga.

 

Waathirika wakuu walikuwa ni wakulima wa Karafuu, Hiliki, pilipili manga na mdalasini waliopo kwenye kata za Kwezitu, Zirai, Misarai, Amani na kisiwani zinazohusisha vijiji vya Kwezitu, Kambai, Kizerui, Zirai, Kazita, Shambangeda, Antakae, Msasa IBC, Magoda Msasa,Kwemdimu, Mgambo miembeni na Kwemsoso.

 

Mkopo huu unatajwa kuwatesa wakulima wengi na kujikuta wakishi Maisha ya kimasikini ingawa mazao wanayolima yana thamani kubwa.

 

Walichokuwa wakifanya wakopeshaji ni kununua maua ya mazao hata kabla ya msimu wa mavuno kuanza, ununuzi huo unamfanya mkopeshaji kuwa na uhuru wa kuvuna kwa muda mrefu zao alilokubaliana na mkulima bila kizuizi na kama ikitokea mkulima akalalamika, anaweza kujikuta anapoteza hata vitu vyake vya ndani kama televisheni, redio n ahata godoro.

 

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kwezitu, Endrew Kalaghe akifafanua jambo. 

Kwa kuliona hilo USAID  kupitia mradi wake wa Tuhifadhi Maliasili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameamua kuwajengea uwezo wakulima katika kuweka na kukopeshana wenyewe kwa wenyewe.

 

Hatua hiyo imewasaidia wakulima wengi kuondokana na mikopo ya kausha damu,katika kuupata ukweli wa hili na namna wakulima walivyonufaika, chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) ambacho kinatekeleza mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na USAID,kilipeleka timu ya Waandishi wa habari kwenye Kijiji cha Kwezitu. 

 

SAFARI YA KWEZITU

Ni mwendo wa wastani wa kilomita 35-40  kutoka Muheza mjini hadi katika kijiji cha Kwezitu kilichopo katika Kata ya Kwezitu, tarafa ya Amani, wilayani Muheza, mkoani Tanga.

 

Kijiji hicho ni moja ya vijiji vya Amani vinavyobeba sifa ya kuwa walimaji wakubwa wa viungo kama vile Hiliki, Karafuu, Mdalasini na Pilipili manga.

 

Safari ya kutoka Muheza mjini hadi katika Kijiji cha Kwezitu inanogeshwa na hali mbaya ya barabara iliyopo mara baada ya kumaliza lami.

 

Eneo kubwa la barabara inayoelekea huko imetawaliwa na udongo, mawe na zege lililomwagwa kwenye maeneo korofi hasa yale yenye miinuko mikubwa na kona kali na hatari kama ile maarufu iliyopewa jina la kona ya Simba.

 

Mtendaji wa Kijiji cha Kwezitu, Agness Mpwapwa.

Ukiwa unatokea Muheza mjini kwenda Kwezitu kuna kipande kidogo cha Kilomita zisizozidi 12 zinazohusisha vijiji vya Mbalamo, Msangazi, Njiapanda ya Magila,Kilimatengwe, Kwa mgobe, Ubembe, Mianzini, Kilometa saba, Kwemhosi, Kwematindi, Bombani na Timba ndio zimewekwa lami.

 

Hali ya hewa kwa muda mwingi ni tulivu, hakuna jua, hakuna mvua, ukubwa wa misitu unazalisha ukungu ambao umefunika safu ya milima ya usambara iliyotandawaa katika eneo kubwa la mji wa Amani.

 

Kila gari inavyokata kilomita za barabara ndivyo unavyooyaona mandhari ya kuvutia ya mji huo kwa upande wa kulia na kushoto, misitu minene iliyosheheni kijani mwanzo hadi mwisho inaipamba barabara ‘vyedi’.

 

Safari ya kuelekea Kwezitu haina afadhali, kwani kila unavyozidi kwenda mbele ndivyo unavyozidi kuikwea milima iliyobeba miti mikubwa.

 

Dereva asiye na uzoefu wa kutosha wa mikikimikiki ya barabara mbaya na zenye kona kali, anaweza kuwafupishia safari kwa kuamua kurudi alikotoka au kuwatupa makorongoni.

 

Ugumu wa safari unalazimisha tuliomo ndani ya gari kutafuta namna ya kujifariji, mizaha,utani na vicheko vinasaidia kuiona safari ni fupi, hata hivyo ziko nyakati ukimya unatawala hasa pale mnapomwona dereva amekaza kila kiungo cha mwili wake, huku akiongeza umakini zaidi. Ni safari ya kikazi haswa.

 

Pamoja na ugumu wa safari, lakini haibadili ukweli kuwa mazingira ya njiani ni mazuri na yenye kuvutia.

 

Uzuri wa mwonekano wa mazingira ya njia nzima unadhihirisha kuwa wakazi wa tarafa ya Amani wanajua umuhimu wa kutunza mazingira.

 

Ndio, hilo liko wazi na Afisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Issa Msumari alilithibitisha hilo, kwa kusema kuwa wamejiwekea mikakati ya kuhakikisha kila mtu anaeishi kwenye wilaya ya Muheza anatunza mazingira.

 

“Huku kila mmoja ni mlinzi wa mwenzake kwenye kutunza mazingira, hakuna kuchoma moto hovyo wala kukata miti, ukikutwa na yeyote yule, ujue kazi unayo.”

Afisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Issa Msumari 

 
JET NDANI YA KWEZITU

Safari ya zaidi ya saa moja inatamatika katikati ya Kijiji cha Kwezitu zilipo ofisi za Kata na mwenyeji wetu ni mwenyekiti wa Kijiji hicho Christopher Shemainde ambae alishindwa kutupokea kutokana na kutingwa na majukumu mengine na kisha kulikabidhi jukumu hilo kwa mwenyekiti wa Kitongoji Endrew Kalaghe.

 

Kalaghe, anaipokea timu ya JET na kuiingiza kwenye ukumbi wa mikutano uliomo ndani ya soko, tayari baadhi ya wananchi walishaketi kwenye mabenchi ya mbao.

 

Ukarimu wa wananchi wa Kwezitu unatoa faraja kwa JET iliyoongozwa na Mkurugenzi wake, John Chikomo na waandishi kwa ujumla.

 

Bila kuchelewa Kalaghe, anaanza kwa kueleza namna USAID ilivyowasaidia kwenye mambo mbalimbali likiwemo hilo la mikopo ya kausha damu.

 

Kalaghe anasema mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, umewaondoa kwenye mikopo ya kausha damu kwa kuwapa elimu ya namna ya kuweka na kukopeshana wao kwa wao bila kuweka dhamana ya mazao yao kabla ya msimu.

 

“Tulikuwa tunataabika sana, maana wakopeshaji walikuwa wakituvizia kipindi kile cha uhitaji wa fedha, wao wanakuja na kutupa mashariti magumu, ambayo yalikuwa ni mateso kwetu, lakini ujo wa USAID umetusaidia kuondokana na mikopo ya kausha damu,”alisema.

 

Mbali na kupewa elimu ya namna ya kujiwekea akiba wao wenyewe, pia USAID imesaidia kuwapangia Kijiji chao kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi.

 

Kalaghe anasema, mpango wa matumizi bora ya ardhi umewasaidia kuondokana na migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa ikiwatesa kwa miaka mingi.

 

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji hicho, Agnes Mpwapwa, alisema yeye ni miongoni mwa wanufaika wa elimu ya kuweka na kukopa iliyotolewa na USAID na GFP.

 

“Hawa wenzetu wametusaidia sana kuondokana na unyonyaji kutoka kwa madalali ambao walikuwa wakituletea mikopo yenye mashariti magumu, ilikuwa inatutesa hasa maana mtu anakukopesha ths. 300,000 lakini huwezi kuamini, huo mkopo hausihi mpaka atakapotaka yeye.

 

“Anaweza akavuna viungo kw ahata misimu mitatu, yaani wewe unaishi kuona mazao yako yakichukuliwa kila msimu nah una pa kulalamikia maana ni kweli umekubali mwenyewe kukopa,”alisema.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kwezitu.

 
Joseph Mkufya ambae ni mkazi wa Kijiji cha Kwezitu anasema kuwa ujio wa USAID na GFP umewasaidia kuongeza kiwango cha uvunaji wa mazao yao hasa pilipili manga na Karafuu, kwani wamepewa miche pamoja na kufundishwa namna sahihi ya kulima kilimo hai.

 

OMBI LA MIKOPO NAFUU KWA RAIS DKT. SAMIA

Mpwapwa alitoa ombi kwa serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa mikopo yenye mashariti nafuu zaidi kwa wakulima wa viungo waliopo Kwezitu na Amani kwa ujumla.

 

“Tunaiomba serikali nayo ishiriki katika kutoa mikopo yenye mashariti nafuu kwa wakulima ili isaidia kuepukana kabisa na mikopo ya kausha damu ambayo bado ipo na kuna wakulima wenzetu wanaendelea kuumizwa.”

 

Mwenyekiti wa MJUMITA, Ester Mzalia, Emmanuel Mkufya Jonathan Mshihiri na  Emanul Chamungwana, pia ni miongoni mwa wakulima walioungana na Mpwapwa katika kuiomba serikali kuangalia namna ya kuwafikishia mikopo nafuu wakulima.

 

Kwa upande wake Mtandaji wa Kata ya Kwezitu Esther Kilua, alisema ujio wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa Tuhifadhi Maliasili umewasaidia wakulima kujitambua na kuiona thamani ya kilimo.

 

Kuhusu ombi la serikali kutoa mikopo kwa wakulima, Kilua alisema tayari serikali imeshatoa nafasi hiyo na watu walio kwenye vikundi wameshaanza kukopeshwa.

 

Kwa upande wake Afisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Issa Msumari, alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wake imekuwa ikijitahidi kutoa elimu kwa wakulima kuachana na mikopo ya kausha damu, lakini wakulima wengi ni wajeuri.

 

Mwenyekiti wa MJUMITA, Ester Mzalia,

“Wakulima wengi ni wajeuri na wabishi, wanapenda wenyewe kujitia kwenye umasikini kwa kukopa mikopo yenye mashariti magumu na wanakopa sio kwa ajili ya kwenda kulimia au kupeleka Watoto shule au kufanya maendeleo, wanakopa ili kutunisha makwapa mitaani kwa kuongeza wake, kulewea na kufanya vitu visivyo vya maana.”

 

Msumari alisema, serikali inatoa mikopo na haina mashariti yeyote zaidi inahitaji nidhamu tu katika kuirejesha na mikopo hiyo imeshafika kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya ya Muheza.

 

Katika kuwataka wakulima waondokane na mikopo isiyo na tija kwao, aliwataka kuhakikisha wanajiunga na vikundi mbalimbali vya kuweka na kukopa, lakini pia wachangamkie fursa za mikopo ya serikali pale inapowafikia.

Moja ya manejo ya kijiji cha Kwezitu.


Post a Comment

0 Comments