Ticker

7/recent/ticker-posts

KILIMO HAI NI MLINZI MKUU WA MAZINGIRA WILAYANI MUHEZA

  

Miti ya karafuu inayohusisha kilimo hai ikiwa imepandwa katika eneo la shule ya Msingi Msasa IBC.

NA JIMMY KIANGO-MUHEZA

 Kilimo hai ni mfumo wa kilimo endelevu kinachozingatia mbinu zinazolinda na kuhifadhi mazingira, ardhi, na vyanzo vya maji huku kikilenga kuboresha maisha ya wakulima. 

 

Aina hii ya kilimo hutumia mbinu za kiasili katika kila hatua kama vile matumizi ya mbolea za asili, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kupunguza matumizi ya kemikali hatari kama vile viuatilifu na kukuza utofauti wa mazao mchanganyiko wa mimea.

 

Lengo kuu la kilimo hai ni kuleta uzalishaji wa chakula bora bila kuathiri mazingira, kwa kutunza rutuba ya udongo na kuhifadhi mfumo wa ikolojia. 

Hatua hii husaidia kuhakikisha kuwa ardhi inabaki na rutuba na kuwa endelevu kwa vizazi vijavyo.

 

Moja ya maeneo nchini yanayolima kilimo hai ni wilayani Muheza mkoani Tanga, hasa katika Tarafa ya Amani. Katika eneo hili la Amani neno kilimo hai ni kama wimbo wa Taifa kwa wakazi wake.

 

Kijiji cha Kwemhosi ndio kimebeba simulizi tamu la chimbuko la aina hiyo ya kilimo wilayani Muheza. Ni mwendo wa wastani wa kilometa tisa kutoka Muheza mjini kwenda Kwemhosi.

 

Kwa safari ya gari aina ya Landcruiser iliyo na ubora inayokata upepo kwenye lami, umbali wa kilometa tisa ni jambo la dakika chache tu.

 

Ndani ya dakika zisizozidi 15, timu ya Waandishi wa Habari za Mazingira iliyo chini ya mwamvuli wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), wakiongozwa na mkurugenzi wake, John Chikomo walifika kwenye ofisi za kiwanda cha GFP Organic Ltd cha kuchakata mazao ya viungo vya kilimo hai.

 

GFP pia inaendesha mradi wa Kilimo hai ambao uno chini ya ufadhili wa  mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili katika ushoroba wa misitu ya Amani-Nilo.

 

Msimamizi wa Mradi wa Kilimo hai wa GFP ndani ya Halmashauri wa Muheza, Bi. Magreth David, akifafanua jambo kuhusu kilimo hai.

JET ilipeleka timu ya waandishi wa Habari za Mazingira kwenye ofisi za GFP, ikiwa ni mwendelezo wa kutekeleza mradi huo wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na USAID. 

Magreth David ambae ndie msimamizi wa mradi huo wa Kilimo hai ndani ya wilaya ya Muheza ndie mwenyeji wa timu ya Waandishi wa Habari za Mazingira iliyofika ofisini kwake ili kupata taarifa za mafanikio na umuhimu wa kilimo hai kwa wananchi wa Muheza na vitongoji vyake na mazingira kwa ujumla.

 

Mazingira ya kuvutia na tulivu yaliyopo katika eneo lote la nje na ndani ya ofisi hizo yanaashiria wazi kuwa kwenye kijiji hicho umuhimu wa utunzaji wa mazingira ndio kipaumbele chao. 

 

Pasi kuchelewa Magreth aliiita timu yake ya vijana watatu Bwana shamba, Erick David, Mdhibiti ubora, Erick Joseph na kijana anaepewa mafunzo ya Kilimo hai, Ramadhani Kijazi ili kwa pamoja washirikiane kuwamegea waandishi wa Habari taarifa sahihi za umuhimu wa kilimo hai.

 

Kabla ya kuanza mazungumzo Magreth aliwaomba wageni wake kuvua viatu vyao na kuvaa viatu maalum vinavyoweza kuvaliwa kwenye eneo hilo.

 

Kwa haraka viatu vilitolewa na kila mwandishi alikabidhiwa avae ili awe na uhuru wa kuingia katika eneo hilo, ambalo limebeba meza nane kubwa  zinatumika kukaushia mdalasini, hiliki, karafuu na pilipili manga. 

 

Mara baada ya kukamilisha zoezi la kuvaa viatu, Afisa Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Muheza, Issa Msumari  alifanya utambulisho wa pande zote mbili na kisha kumpa nafasi Chikomo aeleze dhamira ya JET kuwa pale.

 

Chikomo alifanya hivyo na kisha kutoa nafasi kwa GFP, kueleza umuhimu wa kilimo hai na jinsi kinavyoweza kutunza mazingira.

 

Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata mazao ya kilimo hai cha GFP, wakiingiza zao la mdalasini kiwandani.

KILIMO HAI NI MLINZI WA MAZINGIRA

 

Magreth alisema kuwa moja ya mambo wanayojivunia ni namna walivyofanikisha kuwajengea uwezo wananchi katika kuendeleza mradi wa kilimo hai.

 

“GFP Organic Ltd, ilianza kazi Muheza mwaka 2014, kabla ya ujio wetu hali ya utunzaji wa mazingira haikuwa nzuri ingawa kilimo cha viungo kilikuwepo.

 

“Huku Muheza hasa ukanda wa milimani (Amani), kilimo cha viungo ndio shughuli kuu ya wakazi wake na hili limekuwa likifanyika kwa miaka mingi, hata hivyo walikuwa wakilima kimazoea.

 

“Haikuwa ajabu kwao kuchoma na kukata misitu hawa wanapokuwa wanapanda mimea yao hiyo, lakini pia walikuwa wakitumia dawa zenye kemikali. Hali hiyo iliwafanya kukosa soko la uhakika kwa sababu wanunuzi wakuu wa mazao hayo wanataka bidhaa iliyolimwa kiasili.”

 

Magreth anasema mara baada ya GFP kufika Muheza walianza kazi ya kutoa elimu kwa jamii juu ya kulima kilimo hai na lengo kubwa lilikuwa ni kuwasaidia kujitengenezea kipato kikubwa na cha uhakika, lakini pia kutunza mazingira.

 

Anasema wakulima wa Amani walikuwa hawajui kutunza mazingira, walilazimika kuifanya kazi hiyo katika mazingira magumu kwa sababu wengi hawakuwa wakielewa umuhimu wake zaidi waliona ni kama wanapotezewa muda.

 

Hata hivyo GFP hawakukata tamaa, waliendelea kutoa elimu pamoja na kuwahakikishia soko la uhakika ambalo hapo kabla halikuwepo, lakini pia waliwafundisha namna ya kutumia mbolea na dawa za asili za kumwagia kwenye mimea yao.

 

Magreth anasema elimu ya kilimo hai ilianza kuwaingia na hatimae taratibu wengi wa wakulima walianza kuachana na kilimo cha mazoea kisichojali mazingira na kujikita kwenye kilimo hai.

 

Afisa Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Muheza, Issa Msumari, akielezea jambo kwa waandishi wa Habari za Mazingira.

“Kwa ukanda wa juu, GFP inafanya kazi na vijiji vya Antakae, Kwezitu, Zirai , Kizeru, Kazita, Msasa IBC, Magoda na Shambangeda.

“Kwa ukanda wa chini tunashughulika na wakulima wa vijiji vya Kwemhosi, Bombani, Tongwe, Mangubu, Mashewa na Magoroto, tunao wakulima 654 wanawake na wanaume.”

 

Anasema GFP imesaidia kuwaongezea uzalishaji wakulima kutoka tani zisizozidi 50,000 hadi tani 80,000 za karafuu, huku pilipili manga uzalishaji wake ukifikia tani 150,000 na kipato cha wakulima wengi kimeongezeka ingawa bado kuna changamoto za baadhi yao kuuza maua kwa madalali hali inayowafanya wakulima kuambulia pesa kidogo wakati wa msimu.

 

“Pamoja na jitihada hizi, lakini bado wapo wakulima wasiowaaminifu ambao wanatumia kemikali kwenye mimea yao, lakini pia matumizi ya vyandarua vyenye dawa nayo yanayaathiri mazao hayo,”alisema Magreth.

 

Magreth aliongeza kuwa kilimo hai ni mlinzi mkuu wa mazingira kwa sababu sasa wakulima hawachomi misitu na pia hawakati miti hovyo tofauti na ilivyokuwa awali kwani kilimo hai kinawalazimisha kuhakikisha wanatumia vitu vya asili zaidi na vitu vya asili huwezo kuvipata kama unaharibu mazingira.

 

“Ukichoma msitu maana yake unaondoa uasili wa eneo, lakini pia huwezi kupata majani mazuri ya kulishia mifugo ambayo kinyesi chake ni mbolea, nathubutu kusema kilimo hai ni mlinzi mkuu wa mazingira.” 


UMUHIMU WA MRADI WA USAID

Magreth anasema wameupokea mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili mwaka 2023, ambapo mara baada ya kuanza kazi ulisaidia katika maeneo mengi yakiwemo ya kuongeza uzalishaji baada ya kupewa elimu zaidi.

 

“Mbali na kuongeza uzalishaji, lakini pia USAID wamesaidia katika kuotesha vitalu vya miti ya karafuu na pilipili manga ambapo miche 60,000 iligawiwa kwa wakulima wa ukanda wa juu bure.

 

“Hatua hii itasaidia kuongeza zaidi uzalishaji, tuna uhakika baada ya miaka mitatu, tutakuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji, lakini pia USAID wamesaidia wakulima kuunda vikundi vya kuwezeshana hatua inayowaondoa kwenye utaratibu wa kuuza maua ya mazao yao kabla ya msimu kufika,” alisema Magreth.  

 

Kwa upande wake Erick, alisema katika kuhakikisha ubora wa mazao yanayonunuliwa na GFP unakuwa endelevu, wamekuwa wakiwafundisha wakulima kutumia mbolea na dawa za asili katika kupambana na wadudu wanaoshambulia mazao.

 

Erick amesema kuwa wamefanikiwa kudhibiti ubora wa bidhaa zao kwa muda mrefu ingawa waliwahi kupata changamoto ya kuingiza sokoni bidhaa yenye sumu, hali iliyosababisha kupokonywa cheti cha ubora, lakini wamefanikiwa kukirejesha na watahakikisha wanabaki kwenye ubora wao.

 

Erick ambae ndie mdhibiti ubora, alitaja vitu wanavyotumia kutengeneza mbolea na dawa za kufukuza wadudu wanaoshambulia mimea kuwa ni mkojo wa sungura, unga wa magimbi, mbegu na mafuta ya Mwarubaini, unga wa vitunguu swaumu, Hamira, pilipili kichaa na sabuni ya maji ambayo nayo hutengenezwa kwa bidhaa za asili.

 

Magreth (wa kwanza kulia) akiwa na Erick (mwenye flana ya njano), Baraka (mwenye kofia) na Kijazi (wa mwisho kushoto) wakielezea umuhimu wa kilimo hai katika kutunza mazingira.

Nae Baraka ambae ni Bwanashamba, amesema GFP inashirikiana kwa karibu na wakulima waliopo kwenye maeneo mbalimbali ya Muheza, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wa ukanda wa Amani wanafaidika na kilimo cha viungo.

 

Akizungumza na Waandishi wa Mazingira Emmanuel Mkufya ambae ni mwenyekiti wa kikundi cha Kilimo hai kutoka Kijiji cha Kwezitu, aliwashukuru GFP pamoja na USAId kwa kuwapelekea mradi wa Tuhifadhi Maliasili ambao umewasaidia kujua namna ya kulima kilimo hai, kutunza mazingira na kujipatia kipato cha uhakika, ambapo sasa wanauhakika wa kuuza mazao yao kwa GFP. 


Mafanikio yaliyopatikana katika kilimo hai kuwa mlinzi mkuu wa Mazingira yanapaswa kuenezwa kwenye maeneo mengi ya nchi hasa yale yaliyopembezoni mwa hifadhi za misitu, kilimo hai kinaweza kuliondoa taifa kwenye athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi zinazotokana na uharibifu wa Mazingira hasa uchomaji na ukataji wa miti.



Post a Comment

0 Comments