Ticker

7/recent/ticker-posts

HISTORIA YA JESHI LA POLISI TANZANIA

HISTORIA YA JESHI LA POLISI TANZANIA. 

Jeshi la Polisi la Tanzania lilianzishwa rasmi 25 August 1919 kwa tangazo la Serikali ya Kiingereza lililotoka Gazeti la Serikali No.Vol.1 No.21-2583 kwa wakati huo likaitwa Jeshi la Polisi Tanganyika. Lakini jeshi lilianzishwa kisheria kwa Sheria ya uanzishaji wa Jeshi la Polisi ya mwaka 1939 [THE POLICE FORCE AND AUXILIARY SERVICES ACT OF 1939) PRINCIPAL LEGISLATION. Sheria hii ndiyo inatumika hadi sasa japo imekua ikifanyiwa marekebisho ya mara kwa mara.

Makao Makuu ya Jeshi hilo kulingana na tangazo hilo yalikuwa Wilayani Lushoto Mkoani Tanga chini ya uongozi wa Major S.T Davis. 

Baadae Mwaka 1921 Kundi la Wakaguzi Polisi kutoka Ulaya lilifika nchini Tanganyika na kuanzisha Shule ya Mafunzo maalumu ya upolisi huko Mkoani Morogoro ili kukidhi mahitaji yao na kuwa na Askari wenye weledi wa kutosha. Pamoja na kuwa na Askari weusi waliofunzu mafunzo lakini bado Askari hao walibaki na vyeo vya chini vya kipolisi kwani vyeo vya juu vyote walipewa Askari wazungu.

Jeshi la Polisi la kikoloni lilikuwa na Wanaume peke yao, hakuna mwanamke aliyepewa nafasi ya kujiunga na Jeshi, siyo tu kwa Watanganyika hata Askari wa kikoloni wote walikuwa wanaume. 

Mafunzo yalilenga kumpa Askari mbinu za kumkandamiza Mwafrika, kuwaminisha kuwa kila walichosema wakoloni ndicho sahihi, ukandamizaji na udhalilishaji kwa mwafrika ulikuwa mkubwa na ndiyo ilichukua sehemu kubwa ya mafunzo kwa Askari wa Kikoloni. Askari walifundishwa utii kwa viongozi wa kikoloni na ukatili dhidi ya waafrika hasa viongozi wa kikoloni pamoja na machifu. Lengo lilikuwa ni kumtawala Mtanganyika kirahisi. 

Watanganyika walitumia silaha za jadi kukabiliana na Askari wa kikoloni, silaha hizo zilikuwa marungu, panga, mikuki, na mishare, pamoja na silaha zilizotengenezwa kwa mawe yaliyochongwa vyema.

Wakoloni waliona ni vyema waanzishe vituo vingi vya Polisi na mwaka 1925 Kituo cha kwanza rasmi cha Polisi nchini kilifunguliwa huko Lupa, Tingatinga Mbeya. 

Mwaka 1930 Makao Makuu ya Polisi yalihamishwa kutoka Lushoto Mkoani Tanga kwenda Dar es Salaam. Lengo lilikuwa kuwa na ngome imara ambayo ilisimamia utendaji wa vituo vingine vyote vya Polisi, mawasiliano na maelekezo ya nini kifanyike vituoni yalitolewa kila siku kwa vituo vyote vya Polisi. Radio na barua za kipolisi zilitumika kufikisha ujumbe vikosini. 

Baadaye Mwaka 1949 kikosi cha kutuliza ghasia, Motorized Company sasa Field Force Unit (F.F.U) kilianzishwa nchini na lengo la kikosi hicho ni kurejesha amani penye vurugu. 

Vijana wa kitanganyika walianzakupinga ukandamizaji wa Mkoloni dhidi yao, vijana hao waliongozwa na baadhi ya Askari waliotoka katika vita ya kwanza na ya pili ya Dunia. Hivyo basi iliwalazimu wakoloni kuanzisha kikosi maalum cha kutuliza ghasia, pia mwaka huo wa 1949 kwa kuzingatia weredi, Vijana mbalimbali wa Kiafrika toka shule mbalimbali za Sekondari Tanganyika walichaguliwa kujiunga na Jeshi la Polisi na kuwa Wakaguzi wa Polisi chini ya uangalizi wa muda maalum (Probation Inspectors). 

Mwaka 1952 Kikosi maalum cha Mawasiliano (Signals Branch) kilianzishwa Polisi bila kutumia nyaya za simu. Lengo la kikosi hicho ni kuhakikisha Jeshi la Polisi linawasiliana muda wote. Mawasiliano yalisaidia kutoa na kusambaza taarifa kwa haraka zaidi na utekelezaji wake kufanyika na mwaka huo pia Askari wa kikie (Women Police) walijiunga na Jeshi la Polisi chini ya uongozi wa Ms. Payee. Ms. Payee ndiye alikuwa kiongozi wa askari wa kike kwa kipindi hicho.

Tanganyika ilipopata uhuru wake mwaka 1961 tarehe 9 Desemba, baada ya uhuru, Jeshi la Polisi lilianza kubadili mwelekeo wake toka katika kutumikia Wakoloni na kuanza kuwatumikia wananchi kwa mujibu wa sera za Serikali ya Wananchi wa Tanganyika japo kwa kidogo bado lilikuwa na mfumo wa kikoloni, ilichukua muda kulibadilisha na kulifanya Jeshi la Polisi lenye kumlinda Mtanganyika na mali zake.

Wakuu wa Jeshi la Polisi (IGP) toka Tanganyika hadi sasa. 

Toka uhuru mpaka sasa Jeshi la Polisi limeongozwa na MaIGP  kumi:- 

1. Elangwa N. Shaidi (1964 – 1970 ), 

2. Hamza Azizi (1970 – 1973)

3. Samweli H. Pundugu. (1973 – 1975) 

4. Philemon N. Mgaya. (1975 – 1980)

5. Solomon Lyaani (1980-1984)

6. Haroun Mahundi (1984 -1996)

7. Omar I. Mahita. (1996 – 2006) 

8. Saidi A. Mwema. (2006 – 2013)

9. Ernest J. Mangu (2014-2017) 

10. Simon N. Sirro (2017-sasa) 

Historia inaonyesha kuwa IGP Mahundi ndiye aliyeongaza Jeshi hilo kwa muda mrefu kuliko wengine wote, alishika nyadhifa hiyo toka mwaka 1984 hadi 1996, takribani miaka kumi na tatu, akifuatiwa na IGP mstaafu Omar I. Mahita, aliyeliongoza Jeshi la Polisi toka Mwaka 1996 hadi 2006, takribani miaka kumi. 

Samweli H. Pundugu ndiye IGP ukilinganisha na Ma IGP wengine, aliongoza kwa muda mfupi wa miaka miwili tu, kuanzia 1973 hadi 1975 akifuatiwa na IGP Ernest Mangu(Ameongoza kwa takribani miaka 3) , Kwa sasa IGP Mangu anasubiri kupangiwa kazi nyingine baada ya nafasi yake kuchukuliwa na IGP Sirro hivi karibuni.

Imendaliwa na 

Francis Daudi

Vidhana Soudha.

Post a Comment

0 Comments