Afisa wa TAWA akieleza jambo kwa wananchi wa kijiji cha Kahunda, baada ya kufanikiwa kumuua mamba aliyekuwa akisababisha madhara kwa wananchi.
NA. MWANDISHI WETU-TAWA
Furaha, utulivu, amani na imani vimerejea kwa idadi kubwa ya wakazi wa Kijiji cha Kahunda, Kata ya Katwe, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza baada ya maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini - TAWA kwa kushirikiana na wananchi kufanikiwa kumuua mamba aliyezua taharuki kwa takribani wiki nzima kwenye Kijiji hicho.
TAWA kwa kushirikiana na wananchi walitekeleza takwa hilo la kisheria Oktoba 3, 2024, lengo likiwa ni kuhakikisha madhara hayatokei kwa binadamu.
Wananchi wa kijiji hicho walitoa taarifa kwa maofisa wa TAWA Kanda ya ziwa katika kituo kidogo cha Mwanza na haraka walifika katika eneo la tukio na kufanikiwa kumdhibiti mnyama huyo kwa kumuua kwa mujibu wa Sheria.
Sheria namba 5 ya Wanyamapori ya Mwaka 2009 inafafanua masuala ya uhifadhi, usimamizi na matumizi ya wanyamapori, ambapo kifungu cha 71 sheria hiyo ndio kinatoa uhalali na mwongozo wa kuua Wanyama hatari au waharibifu na mamba anahesabiwa kama miongoni mwa Wanyama hao.
Sheria inaruhusu kuua mamba pale ambapo wanasababisha hatari kwa Maisha ya binadamu au wanapoharibu mali, hata hivyo hatua hiyo inatekelezwa baada ya kupata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori au mamlaka husika.
Kwa kuzingatia sheria hiyo TAWA ilitekeleza matakwa ya kisheria kutokana na mamba huyo kuibua taharuki na kutishia usalama wa binadamu na mifugo yao.
Wananchi wa Kahunda wamesema mamba huyo alikuwa akileta taharuki kwa wiki nzima na alifikia hatua ya kukamata mifugo ikiwemo bata, kuku na mbwa katika mwalo wa kijiji hicho na kijiji cha Zabaga hali ambayo ilikuwa ikiwafanya waishi kwa wasiwasi mkubwa na kushindwa kufanya shughuli za kibinadamu kwa amani katika ziwa hilo.Afisa habari wa TAWA, Beatus Maganja akiwapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa ushirikiano wao.
Baada ya TAWA kufanikisha zoezi hilo, Mwenyekiti wa kijiji cha Kahunda, Athumani Wambura alitoa pongezi kwa Serikali kupitia maofisa wa TAWA kwa kufanikisha zoezi la kumuua mamba huyo ambae alikuwa ni hatari kwa masiaha ya binadamu na mali zao.
"Niseme tu nawapongeza hawa ndugu zangu wa maliasili (TAWA) jambo walilolifanya ni kubwa kwa wananchi wetu, kwa namna moja au nyingine tumepata amani kwa kumdhibiti huyu mnyama ambaye ni tishio kubwa sana.
“Kwa miaka ya hivi karibuni wanyama hawa wameweza kuua watu wetu zaidi ya watatu katika Kijiji cha Kahunda," amesema Wambura
Kwa upande wake Afisa habari wa TAWA, Beatus Maganja aliwapongeza wananchi wa Kijiji hicho kwa ushirikiano walioutoa mpaka kufanikisha zoezi la kumdhibiti mamba huyo na kuwataka waendelee kuchukua tahadhari wanapofanya shughuli zao katika ziwa hilo pamoja na kuzingatia elimu inayotolewa na watalamu hao huku akiwahakikishia kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuongeza vizimba viwili katika halmashauri ya Buchosa ili kupunguza changamoto ya wanyamapori hao.
0 Comments