Mratibu Mshauri wa GIZ katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Chrian Zimbaiya |
NA JIMMY KIANGO- ALIYEKUWA NAMTUMBO
Moja ya changamoto zinazosumbua watu wengi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hasa ukanda wa Kusini mwa Tanzania ikiwemo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ni migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori.
Kimsingi chanzo cha migongano hii kinatajwa kuwa ni ongezeko la binadamu linalochangia pia ongezeko la shughuli zao mbalimbali za kujitafutia kipato na wakati mwengine kujenga makazi huku eneo la ardhi likibaki kama lilivyo.
Takwimu zinaonesha baada ya Uhuru wa Tanganyika na baadae muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania, ukubwa wa eneo ulikadiriwa kuwa kilomita za mraba 947,303.
Wakati eneo likisalia kuwa hivyo hivyo idadi ya watu kabla na hata baada ya Uhuru imekuwa ikiongezeka kila mwaka kutoka watu milioni 12.3 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 1967 hadi kufikia watu milioni 61.7 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Ongezeko hilo la watu linasababisha uhitaji wa eneo kubwa zaidi la ardhi, hali hiyo inamsukuma binadamu kuingia ndani ya eneo la kilometa za mraba 361,594 ambazo zimetengwa kwa ajili ya uhifadhi wa mbuga za Taifa, hifadhi ya wanyamapori, misitu ya hifadhi na maeneo ya urithi wa dunia.
Kwakuwa ardhi haiongezeki ila watu wanazidi kuongezeka kama ilivyo kwa Wanyama, ni wazi jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori inaepushwa.
Katika kulifanikisha hili, Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya serikali ya Ujerumani (BMZ) na Serikali ya Tanzania wameiona haja ya kutekeleza mradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori unaogusa vijiji nane vya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Septemba 16,2024, Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kwa ufadhili wa Mradi huo unaotekelezwa na GIZ kwa niaba ya BMZ na serikali ya Tanzania, kilipeleka waandishi wa habari wilayani Namtumbo ili kuzungumza na watu mbalimbali wakiwemo GIZ wenyewe ili kujua ni kwa kiasi gani mradi huo umesaidia kupunguza migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori.
Timu ya waandishi wa Habari za Mazingira walizungumza na Mratibu Mshauri wa GIZ katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Chrian Zimbaiya ambae alisema hali sasa ni nzuri tofauti na ilivyokuwa kabla mradi haujaanza:-
Fuatilia mahojiano haya:
JET/AFRINEWS: GIZ inaendesha mradi huu katika vijiji vingapi vya wilaya ya Namtumbo?
ZIMBAIYA: Tunafanya kazi kwenye vijiji nane ambavyo ni Mtelawamwahi, Ligunga, Kilimasela, Mtonya, Likuyu, Likuyumandela Nambecha pamoja na Kitanda.
JET/AFRINEWS: Mradi huu ni wa muda gani nap engine kwa Namtumbo umeanza lini?
ZIMBAIYA: Tunatekeleza mradi wa miaka mitatu ambao ulikuwa unaanza mwaka 2022 mpaka Juzi 2025 na wahusika wakuu ni Serikali ya Ujerumani na Serikali ya Tanzania.
Kwa upande wa Tanzania mradi huu unasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kwa upande wa Ujerumani mradi unasimamiwa na Shirika la GIZ.
JET/AFRINEWS: Kazi za GIZ hapa Namtumbo ni zipi kwenye mradi huu?
ZIMBAIYA:Kwenye Halmshauri ya Namtumbo GIZ inafanya shughuli tatu:-
1. Tunaijengea uwezo Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa kuwapa mafunzo ya jinsi ya kupambana na wanyama waharibifu au kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori.
2. Tunawawezesha kupata ruzuku kiasi ambacho wanakitumia kuweka mafuta kwenye magari, posho za wale maaskari wanaokwenda kushughulikia kufukuza tembo.
3. Tunatoa vifaa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo.Vifaa tunavyotoa ni pamoja na Pikipiki, Kompyuta, Printa na vifaa vingine ambavyo vinahitajika hasahasa wakati wa kufukuza tembo.
Sisi hatutoi vilipuzi kwa sababu sheria za GIZ haziruhusu, hivyo viko kwenye utaratibu wa serikali ya Tanzania.
JET/AFRINEWS: Kwa hapa Namtumbo mradi huu una muda gani?
ZIMBAIYA: Tumekuwa tukitekeleza shughuli hizi kwa mwaka mmoja na nusu sasa na mradi unaendelea na kuna malengo manne tunayoyafanya apia kama ifuatavyo:-
1. Kuboresha ukusanyaji wa takwimu za mashamba yanayoharibiwa kwa kuanzisha mfumo wa kidigitali unaojulikana kama (PAIS) ambao unatumia simu janja.
Maofisa ugani wa vijiji nane watafundishwa jinsi ya kutumia huo mfumo na watapewa simu kwa ajili ya kukusanya data.
Hizo simu zitakuwa zinatuma taarifa moja kwa moja kwenye Halsmashauri na wakijiridhisha na ukweli wa taarifa hizo, nao watatuma moja kwa moja wizarani kwa ajili ya kushughulikia kifuta jasho cha waathirika.
2. Tunawezesha Haslmashauri kupata vifaa vya kupambana na Wanyama waharibifu ambavyo ni magari, pikipiki na vifaa vingine vidogovidogo, tutatoa gari moja kwa TAWA na jengine tutatoa kwa TANAPA na kwa Halmashauri tutatoa pikipiki tatu.
3. Tunawezesha jamii kujenga uwezo wa wao wenyewe kupambana na hii changamoto na katika eneo hili tunafanya shughuli tatu.
a. Kufundisha kulima mazao ambayo hayaliwi na tembo kuanzia kulima mpaka kuvuna na kuwapa mbegu kwa vikundi.
b. Kufundisha njia mbadala za kuzuia tembo ambazo ni pamoja na kutumia uzio wa dawa ya harufu, tunatoa malighafi zote za kutengeneza hizo dawa pamoja na namna ya kuzitumia.
c. Kuanzisha vikoba kwa lengo la kumsaidia mkulima ambaye shamba lake limeharibiwa na tembo kupata namna ya kujikimu na kila kikundi kinapewa mtaji kidogo wa kuanzia na baadae wanaendelea kuweka na kukopa wao wenyewe.
4. Kuboresha mitaala kwenye vyuo vya maliasili ikiwa ni pamoja na kwenye chuo cha Likuyu, ambapo tunaboresha mbinu kwa Askari Uhifadhi wa Kijiji (VGS) kujua namna bora ya kukabiliana na Wanyamapori wakali na waharibifu.
Tumefundisha VGS 50 na tumeanza na vijiji ambavyo havikuwa na VGS na jukumu lao ni wao kuwa wa kwanza kushughulika na tembo wanapotoka hifadhini na kuingia kwenye Kijiji sisi sheria yetu ni lazima tutumie watu ambao wamepewa mafunzo ya kufukuza tembo.
JET/AFRINEWS: Kumekuwa na vilio kutoka kwa VGS wakilalamikia kutokuwa na posho pamoja na vifaa muhimu vya kutekeleza majukumu yao, hili GIZ inalijua na imechukua hatua gani?
ZIMBAIYA: Changamoto hii ni kubwa na tunaijua ni kweli hawa VGS hawaajiriwi ni maaskari wa akiba ambao hawalipwi chochote jambo linaloshusha morali wakati wanapotekeleza majukumu ya kurudisha tembo hifadhini.
GIZ tumeliona hilo na kwa sasa tunafikiria kuwatafutia namna ya kuwaweka kwenye vikundi vya ujasiriamali na kuwapatia mitaji kidogo kwa ajili ya kuzalisha kipato ili iwe kama motosha wakati wanashughulikia hizi changamoto zinazoendelea.
JET/AFRINEWS: GIZ imesaidia kupunguza migongano?
ZIMBAIYA: Ndio kwa kiasi fulani ujio wa GIZ umesaidia mambo mengi ikiwemo Halsmashauri kuboresha upatikanaji wa data za mashamba yanayoharibiwa na tembo, tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo kulikuwa hakuna upatikanaji wa data wa uhakika.
Changamoto zimepungua kwa vijiji vitano vya mradi, ukiondoa Likuyu, Mandela na Nambecha, ambavyo kwa mwaka huu bado vina changamoto kubwa ya tembo kuingia kwenye maeneo ya binadamu.
Na kwa kuliona hilo GIZ wametoa kiasi cha fedha kwa maskari ili kuweka kambi kwa zaidi ya miezi minne ambazo zilikuwa zikitumika kulipa posho na kuweka mafuta kwenye gari na pikipiki, hatua ambayo imesaidia kupunguza kidogo matukio tofauti na awali na kama kusingekuwa na jitihada hizo huenda hali ingekuwa mbaya.
Japokuwa tulipata changamoto ya kifo kimoja kwenye Kijiji cha Likuyu, lakini afadhali inaonekana, lakini pia vijiji viko mbali na taasisi zetu hizo.
Mfano Kijiji cha Ligunga hadi kukifikia kutoka hapa Halmashauri ni zaidi ya kilomita 120, hata wakipiga simu kuwa tembo wameingia kijijini, kumtoa askari hapa halmashauri hadi huko, inakuwa ngumu kufika eneo la tukio kwa haraka.
Lakini pia idadi ya askari wa uhifadhi ni ndogo kwa hapa Halmashauri na vitenda kazi ni changamoto na hata bajeti yenyewe ni ndogo kwa ajili ya kukabiliana na migongano hiyo.
Pia GIZ imeliona hilo na imetoa ruzuku ya zaidi ya milioni 120 kwa ajili ya kupata mafuta, mahema, posho na sare na hii ni kwa mwaka mmoja, lengo likiwa ni kuwaongezea nguvu baada ya hapo serikali itapaswa kuendelea yenyewe.
JET/AFRINEWS: Je, changamoto hizi za migongano ziko kwenye vijiji nane pekee hapa Namtumbo?
ZIMBAIYA: Hapana changamoto ziko kwenye zaidi ya vijiji 40, lakini GIZ inashghulika na vijiji nane, hivyo kunahitajika nguvu zaidi katika kukabiliana na changamoto hizo za migongano.
0 Comments