Kaimu Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Imani Mruma(katikati)akiwa katika picha ya Pamoja na wadau mbalimbali wakati wa
Mafunzo ya Mpango wa Utekelezaji wa Matumizi bora ya Nishati, Tanzania kwa Wadau wa Nishati, inayofanyika tarehe Oktoba, 1-3,2024, Mkoani Morogoro. NA MWANDISHI WETU -MOROGORO |
Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wameandaa yenye lengo la kuwawezesha wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kupitia nyaraka zitakazosaidia kuandaa vigezo vya kitaalam vitakavyoongoza kazi ya usimamizi na ukaguzi wa matumizi bora ya nishati nchini.
Warsha hiyo imehusisha wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Pia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi( VETA), Taasisi ya Elimu ya Juu Tanzania(TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (NACTVET).
Akizungumza katika warsha hiyo mkoani Morogoro, Oktoba 2, 2024, Kaimu Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Imani Mruma, amesema warsha hiyo imezilenga zaidi Taasisi zinazosimamia matumizi bora na sahihi ya nishati nchini.
Amesema baada ya warsha hiyo, wadau hao kwa pamoja watatoa andiko la namna bora ya kusimamia ubora wa bidhaa za nishati nchini pamoja na ukaguzi wake.
Kaimu Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Imani Mruma, akizungumza na Wadau wakati wa Warsha ya Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Matumizi bora ya Nishati Tanzania.
"Azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapata nishati kwa uhakika, kwa gharama nafuu na uendelevu hivyo mafunzo kwa wadau mbalimbali ni muhimu ili kuchagiza utekelezaji wa haraka wa ajenda ya matumizi bora ya nishati." Amesisitiza Mha.Mruma
Kwa upande wake, Meneja wa Utekelezaji wa Matumizi Bora ya Nishati kutoka UNDP, Aaron Cunningham amesema uandaaji wa vigezo vya kitaalam na ujuzi katika kusimamia na kukagua matumizi ya nishati vinalenga kuandaa Wataalam ambao watasaidia nchi kufanya ukaguzi na usimamizi wa matumizi bora ya nishati.
"Warsha hizi ni endelevu na kwa kutumia warsha kama hii ya leo, tumeweza kupata miongozo mitatu kwa ajili ya kuandaa wataalamu hao. Miongozo hii itatumika nchi nzima na kutekelezwa na wadau mbalimbali wa nishati na elimu." Amesema Cunningham.
Ameongeza kuwa, UNDP kama mdau wa Maendeleo, itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuweka mazingira rafiki na rahisi katika masuala ya matumizi bora ya nishati pamoja na upatikanaji wake.
Meneja wa Mradi wa Utekelezaji wa Matumizi bora ya Nishati Tanzania, kutoka Shirika la Maendeleo( UNDP)Aaron Cunningham.
0 Comments