Ticker

7/recent/ticker-posts

TAWA KUSAKA SULUHU YA MIGONGANO BAINA YA BINADAMU NA WANYAMAPORI TUNDURU

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA, Mabula Misungwi Nyanda


NA MWANDISHI WETU- TUNDURU

Uwepo wa migongano baina ya binadamu na Wanyamapori wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, kumumfanya Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA, Mabula Misungwi Nyanda kukutana na Mkuu wa wilaya hiyo Simon Chacha ili kusaka suluhu ya pamoja.

 

Kamishna Mabula, ameongozana na  maofisa waandamizi wa Taasisi hiyo, ambapo jana Oktoba 16, 2024 alikutana na Mkuu wa wilaya hiyo  ili kujadili mustakabali wa utatuzi wa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo inayowakabili wananchi wa  wilaya hiyo.

 

Kamishna Mabula ameeleza namna Taasisi yake inavyotekeleza jukumu la kupambana na changamoto ya wanyamapori hao ili kuwaondolea adha wananchi  na namna ilivyojipanga kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa akiwa katika ziara ya kikazi  Mkoani  Ruvuma Septemba, 2024 kuhusu kukabiliana na changamoto ya wanyamapori hao katika wilaya za Tunduru na Namtumbo.

 

Mabula amesema TAWA inatarajia kuongeza vitendea kazi na katika wilaya ya Tunduru itaongeza gari moja na Pikipiki mbili zitakazotumiwa na Askari wahifadhi kwa ajili ya mwitikio wa haraka wa matukio ya tembo, ikiwa ni pamoja na mabomu baridi 250 kwa ajili ya kuwarwjwsha wanyamapori hao kwenye maeneo yao.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Simon Kemori Chacha 

Ili kuimarisha utendaji kazi, Kamishna Mabula amesema TAWA imejenga kituo cha Askari wa kudumu eneo la Chingulungulu na hivi karibuni  itaongeza idadi ya Askari wahifadhi wapatao 20 Katika kituo kidogo cha Songea ili kuwaongezea nguvu Askari nane waliopo sasa wilayani Tunduru ikienda sambamba na kuanzisha kituo cha muda cha Askari katika tarafa ya Namasakata.

 

Katika hatua nyingine Kamishna Mabula ametumia ziara hiyo kuongea na Maafisa na Askari wa uhifadhi ili kusikiliza changamoto wanazopitia Katika utekelezaji wa majukumu yao na kuhimiza utendaji kazi unaozingatia sheria, kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kusisitiza ushirikiano na vyombo vingine vya dola hususani Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

Aidha Askari wahifadhi wamebainisha changamoto mbalimbali wanazopitia katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na uchache wa Askari kulinganishwa na ukubwa maeneo yenye changamoto.

 

Pia  mashamba ya wananchi kulimwa mbali mbali kati ya shamba moja na lingine kwa umbali wa zaidi ya kilometa tano ambayo nayo  imetajwa kuwa ni mojawapo ya changamoto zinazowawia ugumu Askari wahifadhi hao kuwahudumia wananchi  hasa pale inapotokea mtawanyiko wa wanyamapori katika maeneo yao na kushauri wananchi walime mashamba yao kwa ukaribu ili iwarahisishie kuwapa huduma stahiki.


Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru Simon Kemori Chacha amepongeza jitihada zinazofanywa na TAWA na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ujumla wilayani humo katika kukabiliana  na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo na kusisitiza  kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao Kwa wananchi

 

 Pia  ametilia mkazo suala la ushirikiano baina ya Halmashauri, Taasisi za uhifadhi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na wadau wa uhifadhi katika kutekeleza mkakati wa Wizara wa kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori.


Maeneo mengi ya Wilaya za Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma kwa kiasi kikubwa yanakabiliwa na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori kutokana na eneo kubwa la wilaya hizo kuzungukwa na hifadhi.  

 


Post a Comment

0 Comments